Hafla ya mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Absa Tanzania Kwa kiasi cha shs milioni 50, imefanyika eneo la kisima na kuhudhuriwa na viongozi wa RUWASA, serikali ya kijiji, huku mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dk. Batilda Burian, aliyewakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Aron Luhanga, alieleza kwa msisitizo dhamira ya mradi huu: “Huu si mradi wa miundombinu tu, bali ni stori ya matumaini, utu na fursa, kwa muda mrefu maji salama yamekuwa kikwazo kwa mustakabali wa watoto wa Kwedizinga, leo, tunatekeleza kusudi letu: Kuiwezesha Africa ya kesho, pamoja… stori moja baada ya nyingine. Tunajivunia kuwa nguvu ya wema katika jamii hii kwasababu stori ya kila Mtanzania kwetu ina thamani.”
Alisema mradi huo ulioanza miezi michache iliyopita, sasa unawawezesha zaidi ya wakazi 3,800 kutoka vitongoji saba kupata maji safi kwa uhakika ambao hapo awali, jamii hii ilitegemea mabwawa ya msimu ambayo hukauka wakati wa kiangazi, hali iliyowalazimu wanawake na watoto kutembea zaidi ya kilomita 2 kila siku kutafuta maji yasiyo salama.
“Kisima hiki, chenye kina cha mita 180, kinatumia pampu ya umeme wa jua na kuhifadhi maji kwenye tanki la lita 50,000 lililojengwa juu kwa mfumo wa mvuto wa asili (gravity-fed), ambao mtandao wa bomba na vituo 10 vya kuchotea maji vimesambazwa katika vitongoji vyote vya kijiji.
Naye Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, Bw. James Anditi, alisema: “Ni tamanio letu kuu kama World Vision Tanzania kuona kila mtoto akistawi na kuishi maisha yaliyojaa matumaini na fursa, maji safi siyo tu hitaji la msingi kwa uhai, ni msingi wa ulinzi wa mtoto, afya, elimu, na ustahimilivu wa kiuchumi, mradi huu, ambao ni sehemu ya mkakati wetu katika sekta ya Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (WASH), unaakisi maono hayo kwa kuunda mazingira salama na yenye afya ambapo watoto wanaweza kustawi.
“Tunatoa shukrani za dhati kwa Benki ya Absa kwa kushirikiana nasi kuhakikisha kuwa watoto wa Kwedizinga sasa watatumia muda mwingi darasani badala ya kutafuta maji, na familia zitakingwa dhidi ya magonjwa yanayozuilika kama kuhara na homa ya matumbo, huu ni mfano wa matokeo chanya ya kudumu tunayolenga kuleta mabadiliko katika jamii yetu," aliongeza Bw. Anditi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dk. Batilda Burian, alisema kinachoshuhudiwa hapo ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma jinsi wanavyoweza kuungana kwa pamoja katika kutatua mahitaji na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
“Mradi huu unaonesha kuwa tukishirikiana kwa malengo ya pamoja, tunaweza kutatua changamoto kubwa kabisa katika jamii, Natoa pongezi za dhati kwa Benki ya Absa na World Vision kwa kuonesha mfano wa kuigwa nchini kote,” alisema.
Imeelezwa kuwa mradi huo unaunga mkono moja kwa moja Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) Awamu ya Tatu na malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hasa SDG 3 (Afya Njema), SDG 4 (Elimu Bora) na SDG 6 (Maji Safi na Usafi wa Mazingira).



Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Arona Luhanga (kushoto), akizungumza katika hafla ya makabidhiano rasmi ya mradi wa kisima chenye pampu ya umeme wa jua na mtandao wa usambazaji maji kwa wakazi 3800 wa Kijiji cha Kwedizinga, wilayani Handeni,uliofadhiliwa na benki hiyo. Hafla hiyo ilifanyika kijijini hapo, Handeni, Mkoani Tanga jana

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, akizungumza katika hafla ya makabidhiano rasmi ya mradi wa kisima chenye pampu ya umeme wa jua na mtandao wa usambazaji maji kwa wakazi 3800 wa Kijiji cha Kwedizinga, wilayani Handeni, uliofadhiliwa na Benki ya Absa Tanzania. Hafla hiyo ilifanyika kijijini hapo, Handeni, Mkoani Tanga, jana. Wa pili kushoto ni, Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, Bw. James Anditi.
No comments:
Post a Comment