HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 28, 2025

USHIRIKIANO WA MST NA SERIKALI WAZIDI KUIMARISHA HUDUMA ZA UZAZI WA MPANGO TANZANIA

Mkurugenzi Mkazi wa Maria Stopes Tanzania, Patrick Kinemo (kulia) akizungumza na Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii (katikati, aliyevaa sweta nyekundu) pamoja na wafanyakazi wengine wa MST katika moja ya ziara zake katika huduma Mkoba.
Goryo Kitege muhudumu wa Afya ngazi ya Jamii kutoka MST kijiji cha Wotta akitoa elimu ya afya ya uzazi wa mpango kwa wanawake wa kijiji cha Kikuyu hivi karibuni katika moja ya ziara za MST za Mkoba, anayeaikiliza (kushoto) Mwenye tisheti ya bluu ni Shukuru Mtegule Muhudumu wa Afya ngazi ya jamii kutoka kijiji cha Kikuyu Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma.

TANZANIA imeendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika juhudi za kuboresha huduma za afya ya uzazi, hasa kwa wanawake, vijana na makundi yaliyo pembezoni mwa jamii. Hatua hii imetokana na jitihada shirikishi kati ya serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali kama Marie Stopes Tanzania (MST).

Marie Stopes Tanzania ni mojawapo ya mashirika yanayoongoza kwa kutoa huduma za uzazi wa mpango kupitia mfumo wa outreach au huduma za mkoba.

Kwa mujibu wa Patrick Kinemo, Mkurugenzi Mkazi wa MST, shirika hilo linafanya kazi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kwa kushirikiana na serikali

“Tunaweka mkazo kwa maeneo ya vijijini na yasiyofikika kirahisi ambapo huduma hizi hazipatikani kwa urahisi. Timu zetu hutoa huduma kwa ubora wa hali ya juu kwankushirikiana na serikali,” alisema Kinemo.

MST pia huwalenga kwa makusudi vijana na watu wenye ulemavu kwasababu ni makundi ambayo mara nyingi husahaulika katika upatikanaji wa huduma za afya.

Takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa watu 1,554,913 walihudumiwa na MST kupitia huduma za mkoba, ambapo asilimia 21 kati yao walikuwa vijana walio chini ya umri wa miaka 20.

Hii ni hatua muhimu katika kupunguza mimba za utotoni na vifo vitokanavyo na uzazi. Huduma hizi zimepelekea kufikia alama za muda wa uzuiaji mimba (Couple Years of Protection) 5,593,855 , kuepuka utoaji mimba usio salama 752,156 na vifo vya uzazi 2,934.

Kinemo aliongeza kuwa MST hutoa pia njia za muda mrefu za uzazi wa mpango (Long-Acting Reversible Contraceptives – LARC) kwa kushirikiana na watoa huduma wa serikali. Huduma hizi huambatana na elimu sahihi kwa mteja, upatikanaji wa vifaa salama, na ufuatiliaji wa karibu.

Mbali na huduma vituoni, MST huendesha kampeni za uhamasishaji kupitia magari yenye vipaza sauti, pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuwa mabalozi wa afya ya uzazi katika maeneo yao. “Wahudumu hawa wamekuwa chachu ya mabadiliko kwa kuvunja ukimya na kupambana na imani potofu,” alisisitiza Kinemo.

Kwa mujibu wa Specioza Mahinila, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, ushirikiano kati ya MST na serikali umeleta mafanikio makubwa kwa jamii. “Wilaya yetu ina vituo 74 vya afya, na kati ya hivyo, 67 vinatoa huduma za uzazi wa mpango. Ushirikiano wetu na Marie Stopes Tanzania ni wa muda mrefu na umeimarika zaidi kupitia huduma za mkoba,” alisema Mahinila.

Ameeleza kuwa huduma hizo zimeratibiwa kwa awamu mbalimbali, zikiambatana na mafunzo elekezi
(mentorship) kwa watoa huduma wa serikali kutoka kwa timu za MST. Pia, kupitia usimamizi shirikishi (supportive supervision), MST imetoa vifaa tiba, na vitendea kazi vingine muhimu.

Katika uboreshaji wa huduma, watoa huduma 45 wa ngazi ya vituo na 25 wa ngazi ya jamii tayari wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu uzazi wa mpango. Mafunzo haya yameongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya afya ya uzazi vijijini.

Mahinila anasema juhudi hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa vifo vitokanavyo na uzazi. “Tulifika hadi kuwa na vifo 12 vya kina mama kwa mwaka, lakini hadi sasa mwaka huu tumeshuhudia vifo viwili tu. Vifo vya watoto wachanga pia vimepungua sana,” alisema.

Aidha, vituo vinavyotoa huduma rafiki kwa vijana vimeongezeka kutoka 17 hadi 35. Pia, ushiriki wa wanaume katika huduma hizi umeongezeka kupitia uhamasishaji wa wahudumu wa afya wa jamii. “Awali wanaume walikuwa wakisita kushiriki, lakini sasa wameanza kuwa sehemu ya safari ya uzazi wa mpango, wakisindikiza wake zao na kuonyesha ushirikiano wa wazi. Hii imeboresha maelewano ya kifamilia na kupunguza migogoro nyumbani,” aliongeza.

Hata hivyo, Mahinila ametaja changamoto mbili kuu zinazoikabili wilaya ya Mpwapwa: upungufu wa wataalamu wapya waliofunzwa katika afya ya uzazi, pamoja na jiografia ngumu ya maeneo ya milimani ambayo hayafikiki kirahisi.

Anatoa wito kwa Marie Stopes na wadau wengine waendelee kushirikiana na serikali kuhakikisha maeneo hayo yanapewa kipaumbele katika mipango ijayo.

Mahinila anasisitiza kuwa uzazi wa mpango si tu suala la kiafya bali pia kiuchumi. “Akina mama wanapokuwa na afya njema, wanakuwa na muda wa kushiriki kikamilifu katika kilimo, biashara, na shughuli nyingine za maendeleo. Hii inasaidia familia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.”

Ushirikiano kati ya Marie Stopes Tanzania, serikali, na jamii umeonyesha wazi kuwa mabadiliko makubwa yanawezekana katika sekta ya afya ya uzazi. Huduma bora, elimu sahihi, na ushirikishwaji wa watu wote wakiwemo wanaume na vijana ni hatua muhimu kuelekea Tanzania yenye jamii yenye afya bora na inayojitegemea kiuchumi.

Katika maeneo kama Mpwapwa, huduma hizi si tu tiba. Ni mkombozi wa maisha, ni matumaini, na ni dirisha la mabadiliko ya kweli kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad