WAKULIMA wa zao la Karanga wameeleza utayari wao kutumia Mbegu bora za Karanga zilizofanyiwa Utafiti ambazo wanakiri kuwa zinatija kubwa kulinganisha na Mbegu za kienyeji ambazo wamekuwa wakitumia.
Hayo yamesemwa Leo Juni 08, 2025 na Wakulima wa Karanga Kijiji cha Kiru six, Kata ya Kiru Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara katika siku ya Mkulima wa Karanga iliyofanyika Kijijini hapo ikiratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo cha TARI Naliendele.
Akizungumza kuhusu Mbegu zilizofanyiwa Utafiti, Mkulima Halima Nada ameitaja Mbegu ya TARIKA1, kuwa inamfaa zaidi kutokana na alivyoiona imefanya vizuri kwenye shamba darasa lililowekwa Kijijini hapo ni tofauti na Mbegu ambazo amezoea kutumia.

Halima ametaja utofauti wa Mbegu hiyo ni kutoshambuliwa na magonjwa, radha tamu, inawahi kukomaa huku tija ikiwa kubwa.
"Hii Mbegu ya TARIKA1 imechelewa kupandwa kulinganisha na hizi Mbegu zetu za kienyeji lakini imewai kukomaa na imezaa zaidi ya hizi Mbegu zetu hivyo binafsi msimu ujao nitalima zaidi hii Mbegu ambayo pia inaonesha haishambuliwi na magongwa" amesema Halima.
Pia Mkulima na Mwenyekiti wa Baraza la Wakulima Tanzania, Jitu Vrajilal Son, amesema Mbegu za Karanga zilizofanyiwa Utafiti zina tija katika mnyororo mzima wa thamani kutokana kuwa zinajibu mahitaji ya wadau kama vile Karanga za kwaajili ya Siagi.
Mkulima JituSon, ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Babati amesema alipata mafunzo ya uzalishaji Mbegu kutoka Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) hivyo kutokana na Ubora wa Mbegu za TARI na mwitikio mzuri wa Wakulima ataanza kuzalisha Mbegu hizo kwa wingi ili kukidhi hitajio la Wakulima ambao wameeleza utayari kuzitumia.
Kwaupande wa Watafiti, Mtafiti wa zao la Karanga kutoka TARI Naliendele, Anthony Bujiku, amesema lengo lao kufika Kijiji hapo ni kufanya siku ya Mkulima wa Karanga ambapo wamefundisha kanuni bora za Kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na utambuzi na Uthibiti wa visumbufu katika zao la Karanga.
Mtafiti Bujiku amewashauri Wakulima kuzingatia matumizi ya Mbegu bora pamoja na kufuata kanuni bora ili kujiongezea tija.
Aidha, Mtafiti ametoa wito kwa Wakulima kushirikiana na Maafisa ugani walioko katika maeneo yao ili kupata msaada wa kitaalamu katika mambo mbalimbali ya Kilimo ili waweze kuongeza tija.
No comments:
Post a Comment