HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 3, 2025

ALAF yazindua rasmi mtambo wa mabati ya rangi

 




*Yathibitisha umakini wake katika ubora na viwango Tanzania

KAMPUNI ya ALAF Limited, imezindua rasmi mtambo wake wa mabati ya rangi uliogharimu mabilioni ya shilingi Jijini Dar es Salaam

Mtambo huo, uliogharimu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 25, unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya ujenzi nchini na kuiokolea serikali zaidi ya Dola Milioni 190 ndani ya miaka mitano ijayo.

Akizindua mtambo huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo ameipongeza ALAF kwa hatua hiyo na kusema kuwa haya sio mafanikio kwa kiwanda hicho tu, bali kwa nchi nzima kwa ujumla kwani bidhaa inayozalishwa hapo itatumiwa na Wanzanania wote.

“Hii ni hatua kubwa sana na sisi kama serikali tutafanya kila linalowezekana kulinda uwekezaji huu mkubwa na kuhakikisha unazaa matunda yanayotakiwa hasa kwa kuzingatia serikali pia ina hisa katika kampuni ya ALAF,” alisema.

Aliahidi kuwa serikali itaendelea kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya bidhaa za bei rahisi na ubora wa chini zinazoagizwa kutoka nje ya nchi huku akiagiza vyombo kama TBS kuhakikisha wanamarisha operesheni zao mbalimbali. “Hatuwezi kuwa na uwekezaji mkubwa kama huu halafu tuendelee kuruhusu uingizaji wa bidhaa za bei rahisi ambazo ni hatari kwa ustawi wa viwanda vyetu,” aliongeza.

Aliupongeza uongozi wa ALAF kwa kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliotarajiwa na kwa kuwaajiri mainjinia vijana wa kitanzania ambao wanaendesha mtambo huo mpya. “Huu ni uamuzi mzuri na wa kizalendo kwani unaendana na azma ya serikali kuwawezesha vijana , kuongeza ajira na kujenga Tanzania ya viwanda.”

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa SAFAL Group Anders Lindgren aliipongeza serikali kwa kuweka mazingira madhubuti ya uwekezaji. “Hii imetufanya sisi kuendelea kuwekeza zaidi nchini Tanzania kupitia kampuni yetu ya ALAF Limited,” alisisitiza.

Aliendelea kusema ujenzi wa mtambo huo wa aina yake na wa kisasa, umekuwa ni safari ya kusisimua na kuishukuru serikali kwa kufanya safari hiyo iwe nyepesi kwa ushirikiano walioipa kampuni hiyo kwa kipindi chote cha ujenzi ili kuhakikisha wanafanikiwa.

“Sisi kama SAFAL Group, tunazingatia sana ubora, viwango , usalama na thamani ya fedha kwa mteja popote tunapowekeza ndio maana hatuuzi tu bidhaa bali tupo kutoa suluhisho mbalimbali za ujenzi,” aliongeza.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited. Ashish Mistry, alisema kwa mtambo huo kuanza uzalishaji, Tanzania haihitaji tena kuagiza mabati kutoka nje ya nchi kwani inajitosheleza kabisa kuzalisha zaidi ya tani 130,000 zinazohitajika kwa mwaka. Kwa mtambo huu mpya ALAF itaweza kuzalisha tani 75,000 kwa mwaka ambazo ni zaidi ya asilimia 50 ya mahitaji ya soko.

“Tunawaasa Watanzania wazingatie ubora kwani tunachozalisha sisi kinakupa uhakika wa ubora kwa vizazi vijavyo. Tujiepushe za bidhaa za bei ya chini zisizo na ubora na kuhitaji kubadilishwa mara kwa mara,” alisema huku akisisitiza kwamba wataendelea kushirikiana na wadau mblimbali kupiga vita bidhaa bandia.

Alisema mradi huo unalenga kuimarisha miundombinu ya kiwanda kilichoko sasa ili kiwe na mwonekano wa kisasa.

"Lengo kuu la mradi huu ni ujumuishaji mradi wa kuweka nakshi bidhaa za chuma zinazozalishwa hapa nchini ikiwa ni sehemu ya mpango kabambe wa kampuni yetu”, alisema na kuongeza, mradi pia umelenga kutoa huduma za kuweka nakshi ya rangi kwa bidhaa za chuma zikiwemo zile zinazotumika kwenye vyombo vya majini kwa kuzingatia changamoto za kimazingira yaliyoko maeneo ya pwani ya Tanzania.

Alisema kabla ya uzinduzi huu, ALAF imeshafanya majaribio ya kutosha ya mabati hayo ya rangi kabla kuanza uzalishaji rasmi. “Tunafanya kazi kwa karibu sana na CTI, TBS, TRA na wadau wengine,” alisema.

ALAF, ambayo ilianza kufanya shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1960, imekuja na suluhisho kamili kwa ajili ya shughuli za ujenzi ambazo hujumuisha bidhaa za kuekeza kwenye paa zilizopakwa rangi, Pamoja na bidhaa zingine kama yakiwemo mabomba aina mbalimbali yanayotumika kwenye shughuli za ujenzi.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad