HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 26, 2025

MPANGO WA "BREATHING FOR BABIES" WALENGA KUOKOA MAISHA YA WATOTO WACHANGA

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana  Dkt. Bryson Kiwelu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi wa kupunguza  vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0 hadi 28. 

Dkt. Martha Mkonya Daktari bingwa mbobezi wa watoto wachanga ambaye ni mtafiti Mkuu msaidizi wa mradi wa kusaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi wa kupunguza  vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0 hadi 28.
Mkurugenzi Msaidizi katika Wizara ya Afya anayeshughulikia Afya ya Mtoto na Vijana Dkt. Felix Bundalana akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi wa kupunguza  vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0 hadi 28.



SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa imeweka lengo la kupunguza kiwango cha vifo vya watoto wachanga (wenye umri wa siku 0 hadi 28) kutoka vifo 24 hadi 12 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai ifikapo mwaka 2030.

Dkt. Felix Bundala, Mkurugenzi Msaidizi katika Wizara ya Afya anayeshughulikia Afya ya Mtoto na Vijana, alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki baada ya kupokea gari maalum la kubeba watoto wachanga (ambulance) kwa ajili ya huduma za dharura.

Amesema kuwa mpango huo bunifu unaojulikana kama Breathing for Babies (BfB) unalenga kufidia mapungufu makubwa katika huduma ya upumuaji kwa watoto wachanga nchini Tanzania.

Changamoto zinazotokana na kujifungua kabla ya wakati, hasa tatizo la upungufu wa hewa (Respiratory Distress Syndrome), ni miongoni mwa sababu kuu zinazopelekea vifo vya watoto wachanga nchini.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 12 ya watoto wachanga mijini hupata shida ya kupumua mara tu baada ya kuzaliwa, jambo linaloonesha uhitaji mkubwa wa huduma maalum za upumuaji.

“Ili kufidia pengo hili, Wizara ya Afya imeshirikiana na taasisi kubwa kama Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), na Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI),” alisema Dkt. Bundala.

Kwa kutumia majukwaa ya kisasa kama NEST360 na m-mama, pamoja na ushirikiano wa karibu na wadau wa kimataifa, alisema utafiti wa BfB unabadilisha kabisa namna huduma kwa watoto wachanga zinavyotolewa nchini.

Dkt. Bryson Kihwelu, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, alieleza kuwa mpango huo unajikita katika nguzo kuu tatu:

1. Kuhakikisha uhusiano mzuri kati ya mama na huduma za afya wakati wa kujifungua,


2. Kuimarisha huduma za kulaza watoto wachanga, na


3. Kubadilisha mfumo wa usafiri kwa watoto wachanga kupitia magari maalum ya dharura.

“Hatufanyi tu matibabu kwa watoto wachanga—tunabuni upya safari ya huduma kuanzia wakati wa kuzaliwa,” alisisitiza.

Mradi huu tayari umeanza kuonesha mafanikio katika hospitali kuu za mikoa ya Dar es Salaam—Amana, Temeke na Mwananyamala—na umefikia pia hospitali za wilaya za Kivule, Yombo Vituka, na Mabwepande.

Ukifadhiliwa na Taasisi ya Bill & Melinda Gates, mpango huu wa miaka mitatu (2024–2027) unatoa vifaa muhimu, mafunzo maalum kwa watoa huduma, na mifumo imara ya ukusanyaji wa takwimu ili kufuatilia maendeleo na matokeo ya utekelezaji wake.

Dkt. Martha Mkony, Daktari Bingwa Mbobezi wa Watoto Wachanga na Mtafiti Mkuu Msaidizi wa mradi huo, alisema kuwa mradi huo unalenga kupambana moja kwa moja na vifo vya watoto wachanga nchini.

“Mradi huu utampa mtoto huduma stahiki mara tu baada ya kuzaliwa, kuanzisha matibabu ya upumuaji kwa wakati, na kutoa mafunzo kwa watoa huduma wa watoto wachanga pamoja na wale wanaohudumu kwenye magari ya dharura ya watoto,” alieleza Dkt. Mkony.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad