*Asisitiza nafasi ya kuwa na rasilimali watu wenye Maarifa kufikia lengo
*Achambua hoja za wasomi akieleza nafasi ya PPP katika kutekeleza miradi
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MKURUGENZI Mkuu wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi David Kafulila amesema ili kufikia malengo ya Dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, Kuna kila sababu ya kuwa na rasilimali watu wenye maarifa ya kushindana katika dunia.
Pia amezungumza kuhusu umuhimu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika kutekeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kuipa Serikali nafasi ya kufanya mambo mengine yenye umuhimu kwa wananchi yakiwemo kutoa elimu bora,lishe na kuwajengea uwezo wa maarifa.
Kafulila amesema hayo katika kongamano lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambalo limeandaliwa na PPPC na REDET kujadili nafasi ya ubia kati ya uwekezaji na sekta binafsi kuelekea dira ya Tanzania ya 2050 ambapo wasomi wa kada mbalimbali wameshiriki na kutoa mtazamo wao.
Wakati anaeleza kuhusu umuhimu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi,Kafulia ametumia kongamano hilo kueleza hatua kwa hatua umuhimu wa ubia katika kuleta maendeleo ya nchi na kusisitiza umuhimu wa kuwa rasilimali watu yenye maarifa ya ushindani ili kufikia malengo ya Serikali kufanikisha dira ya Tanzania ya 2050.
"Tunafahamu kwamba shida kubwa ya ushindani iko katika maarifa na leo duniani wanasema maarifa ndio sarafu ya duniani.Nchi nyingi duniani zinashindana kwa maarifa lakini unawekezaje kwenye maarifa kama unakabiliwa na majukumu ya kujenga barabara , majukumu ya ujenzi wa bandari, majukumu ya reli na miradi mingine
"Kwahiyo tunapozungumza ubia tafsiri yake unaipa Serikali nafasi iwekeze katika hayo maeneo ambayo yatasaidia kujenga rasilimali watu ,tusipojenga huko tukajenga mengine hatuwezi kufanikiwa.Hivyo PPP inatoa nafasi kwa Serikali kuwekeza katika kutoa elimu bora na kujenga jamii yenye maarifa.
"Serikali ambayo inapresha ya barabara ,reli na kila kitu inakuwa changamoto ya kujikita kujenga jamii yenye maarifa kwahiyo tunapokuwa na PPP tunapata nafasi ya kuwekeza katika eneo ambalo ni muhimu na tukifanikisha hili la kujenga rasilimali watu kwa kuwekeza katika maarifa tutakuwa tumefanya jambo jema kama nchi."
Hata hivyo Kafulila amesema matarajio yao Kituo cha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi kuelekea mwaka 2050 ni kuwa na ubia katika uwekezaji badala ya Serikali kutumia kodi na mikopo kutekeleza miradi iliyopo.
Kwa upande wake Profesa Anna Tibaijuka, alipokuwa akichangia maoni yake amesisitiza uwekezaji ni muhimu lakini utahitaji kujipanga vizuri zaidi kwa namna ya uwazi na ukweli, akisema migogoro ya PPP na uwekezaji haitaisha bila kuwa na uwazi.
“Hatutaweza kufanikiwa kama hatutaweka mambo yetu sawa, kwa kukubali sheria na uwazi, pia nisisitize na katika hilo sikopeshi kama ukiona mkataba umefichwa uwe PPP au wowote ule ujue ni mbovu, huna haja ya kuhangaika nao, umefichwa kwasababu haukidhi viwango na hauwezi kutusaidia,” ameongeza Prof. Tibaijuka.
Wakati huo huo Dk. Jamal Msami, Mtafiti Mkuu na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti Sera na Uchumi (REPOA), ameeleza kwamba bado kuna changamoto kubwa ya mifumo ya kodi, na vikwazo visivyo vya kikodi, na vya kitaasisi kwamba mitazamo ya sekta binafsi bado ni hasi nchini.
Ameshauri ili kupambana na udanganyifu katika utekelezaji wa miradi ya ubia, serikali inatakiwa iwe ni kituo cha kuratibu upatikanaji na usambazaji wa taarifa.
Kwa upande wake Dk. Kafigi Jeje ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Usimamizi wa Biashara katika Taasisi ya Uhasibu Arusha, alisema bado nafasi ya PPP ipo katika halmashauri kwasababu zinakusanya mapato na kufanya vizuri.
Amesisitiza kwamba miradi ya maendeleo katika ngazi hiyo haiwezi kufanyika kwa asilimia 100 kama wataendelea kutegemea serikali kuu kwa asilimia 75 ndani ya halmashauri.













No comments:
Post a Comment