HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, November 10, 2024

SERIKALI YAWEKEZA MIUNDOMBINU YA TAFITI ZA BIOTEKNOLOJIA NCHINI

 

Na: Calvin Gwabara – Dodoma.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara yake ya Kilimo imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4 kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa maabara za kisasa za Bioteknolojia ya kisasa na kuziendeleza kwa manufaa ya Taifa.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Deusdedith Mbanzibwa wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Chama cha Wataalamu wa Sayansi ya mazao Tanzania (CROSAT) wakati wa mjadala uliokutanisha jopo la wataalamu wa Bioteknolojia kutoka Tanzania, Kenya na Ubelgiji wakiangalia nafasi ya teknolojia hiyo kwenye uboreshaji wa mazao nchini.

“Wizara ya kilimo imekuwa ikitenga fedha nyingi kila mwaka kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya tafiti za bioteknolojia na teknolojia nyingine lakini Bioteknolojia imekuwa ikitumika nchini kwenye kufanya kazi mbalimbali ikiwemo utambuzi wa magonjwa, Wadudu na uzalishaji wa miche kwa njia ya chupa, hivyo ujenzi wa maabara hizo kubwa pale kwenye kituo cha utafiti wa Kilimo Mikocheni utasaidia kuimarisha utumiaji wa teknolojia hiyo nchini”, alieleza Dkt. Deusdedith.

Amesema sambamba na hilo Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo wamewezesha watafiti kwenye kila kituo cha TARI nchini kwenda kusomea na kupata utaalamu wa teknolojia hiyo na hivyo kusaidia kuwa na wataalamu wa kutosha na wengi wao wapo kwenye kituo cha TARI Mikocheni ambapo ndiyo tafiti zinazotumia teknolojia hiyo zinafanyika.

Kwa upande wake Mtafiti Mkongwe wa Bioteknolojia nchini kutoka Chama cha Wataalamu wa Bioteknolojia Tanzania (BST) Dkt. Nicholous Nyange amesema kuwa kikwazo kikubwa cha kutosonga mbele kwa teknolojia hiyo nchini ukilinganisha na nchi zingine na Kanuni iliyowekwa kwenye sheria ya Mazingira ambayo inatoa nafasi kwenye kufanya tafiti lakini inawafunga watafiti mikono kufikisha bidhaa za teknolojia hiyo sokoni.

“Tanzania imeweka kanuni, miongozo na sera za kusimamia matumizi ya teknolojia hii hapa nchini lakini kifungu kimoja kwenye kanuni ya sheria ya mazingira ndiyo kikwazo cha ubiasharishaji hivyo tunaiomba Serikali kufikiria upya kanuni hiyo ili iwezeshe wanasayansi kusaidia kwa haraka kutatua changamoto nyingi zinazowakabili wakulima na kwenye sekta nyingine kutumia teknolojia hiyo wakati ikijiandaa na ujenzi wa maabara hizo”, alieleza Dkt. Nyange.

Naye mtaalamu kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa Mimea na Mazao ambaye amebobea kwenye masuala ya Sera, kanuni na miongozo ya bioteknolojia kutoka nchini Kenya Dkt. Anne Muia amesema kuwa ni muhimu teknolojia za kisasa zitumike kwenye kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na kwenye sekta zingine.

 

“Mimi kama jirani wa Tanzania lakini mmoja wenu hapa Afrika nasema kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha wananchi wetu wanakula wanashiba na nchi kujitosheleza kwa chakula utaona teknolojia tulizokuwa tukizitumia miaka 100 iliyopita kwa sasa zinaanza kushindwa kufanya kazi vizuri hivyo ni muhimu sana kwenda kwa wakati na kukimbizana na mabadiliko haya makubwa ya tabianchi ambayo yanakuja na changamoto nyingi”, alieleza Dkt. Anne.

Aliongeza “ kama vile tunavyoona ukuaji wa teknolojia kwenye sekta zingine kama mawasiliano, usafiri na afya vivyo hivyo wanasayansi wetu duniani pia wanahangaika na kupata teknolojia mbalimbali za kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao hivyo ni muhimu kuwawekea mazingira mazuri ya wao kufanya kazi kwa kuwawezesha lakini kusaidia teknolojia nzuri walizonazo zinatoka maabara na kwenda kunufaisha jamii na Taifa”.

Dkt. Anne amesema wao kama wasimamizi wa teknolojia hizo nchini Kenya kazi yao sio kuzuia teknolojia nzuri za watafiti wao bali kuweka mazingira mazuri ya kuzikagua, kuzifuatilia kuhakikisha zipo salama kwa watu na mazingira na kuzipa nafasi ya kufika kwa wananchi na kuwanuifaisha.

Chama cha Wataalamu wa Sayansi za Mazao nchini CROSAT wameweka mada hiyo na mjadala huo uliowakutanisha wataalamu wabobevu kutoka Tanzania, Kenya na Ubelgiji kwa lengo la kupeana uzoefu kama wataalamu wa mazao na kujadiliana kwa pamoja kuona nafasi ya teknolojia hiyo kwenye kuboresha mazao na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hapa nchini.Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Deusdedith Mbanzibwa (Katikati) akizungumza kwenye jopo hilo, Kushoto ni Prof. Raphael Chibunda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine na Kulia ni mtaalamu kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa Mimea na Mazao ambaye amebobea kwenye masuala ya Sera, kanuni na miongozo ya bioteknolojia kutoka nchini Kenya Dkt. Anne Muia.Mtafiti Mkongwe wa Bioteknolojia nchini kutoka Chama cha Wataalamu wa Bioteknolojia Tanzania (BST) Dkt. Nicholous Nyange akieleza nafasi ya bioteknolojia katika kuboresha mazao na kuinu kilimo Tanzania.Mtaalamu kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa Mimea na Mazao ambaye amebobea kwenye masuala ya Sera, kanuni na miongozo ya bioteknolojia kutoka nchini Kenya Dkt. Anne Muia akieleza uzoefu wake kwenye masuala hayo duniani.Muongoza mjadala huo Dr. Ally Mahadhy kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam akiongoza mahadiliano kwenye  jopo hilo.




 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad