Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimedhamiria kuwa mstari wa mbele kwenye kufanya tafiti mbalimbali kwa kutumia teknolojia ya Bioteknolojia ili kusaidia kupata majibu ya kisayansi kuhusu faida na hasara za teknolojia hiyo nchini kwa kutumia wataalamu wa ndani.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akizungumza kwenye jopo la watafiti wabobevu wa teknolojia hiyo kutoka Tanzania, Ubelgiji na Kenya kweye mkutano wa Chama cha Wataalamu wa Sayansi za Mazao Tanzania (CROSAT) jijini Dodoma wakati wa mjadala maalumu ulioangalia mchango wa Bioteknolojia kwenye uboreshaji wa mazao, mtazamo wa kidunia kwenye sayansi za bioteknolojia kwenye uboreshaji wa mazao.
“Sisi kama Chuo tegemeo la nchi kwenye masuala ya Tafiti za kilimo na sayansi zinazoendana na kilimo tumeshapeleka maombi serikalini ili Chuo chetu kiwe moja ya vituo vya umahiri vitatu vinavyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya kufanya tafiti za bioteknolojia ili tusaidie nchi kubaini ukweli kuhusu teknolojia hiyo kwa undani ili iweze kusaidia nchi” , amesema Prof. Chibunda.
Amesema kuwa Tanzania na nchi zingine za Afrika kutopiga hatua kwenye matumizi ya teknolojia hiyo kunatokana na kutoifahamu na kauli za vitisho vya baadhi ya watu wanaopinga hali iliyopelekea Tanzania kujiwekea sheria na kanuni ngumu ambazo zinawafunga mikono watafiti wake kushiriki kikamilifu katika kuitumia na kuleta maendeleo ya watanzania na Taifa katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
“Ni maombi ya wanasayansi kwamba muda umefika sasa wa nchi zetu za Afrika na Tanzania ikiwemo kuangalia upya tunawezaje na sisi kushiriki kwenye hii teknolojia kama ambavyo tumeambiwa na wenzetu wa Ubelgiji kuwa nchi za Marekani, China, India lakini pia tumeona nchi za Ulaya japo hawalimi sana mazao yatokanayo na teknolojia ya Uhandisi jeni lakini ni watumiaji wakubwa kwa kuwa wanaagiza kutoka katika nchi zinazolima na wanatumia kwa manufaa ya nchi zao”, ameeleza Prof. Chibunda.
Aliongeza “ Kwa hiyo mimi wito wangu na Chuo chetu kitakuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba katika kuanza na kufanya utafiti ili tuone hata kama tunasema kuna madhara basi madhara hayo tuyadhihirishe kwa kazi ambayo imefanywa na watu wetu wenyewe badala ya kutegemea maneno ya kuambiwa au kutegemea tafiti ambazo zinafanywa nje ya mazingira yetu”.
Awali akitoa wasilisho lake Prof.Marc Heidje kutoka Taasisi ya Flemish ya Bioteknolojia (VIB) ya Ubelgiji amesema kufuatia ongezeko kubwa la watu duniani, kupungua kwa maeneo ya kilimo kutokana na makazi, mabadiliko ya tabianchi na uhitaji mkubwa wa chakula kulisha watu hao nchi nyingi duniani zinatumia teknolojia hiyo na kusaidia kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo.
“Teknolojia hii sio risasi ya shaba kwenye kutatua changamoto zote za kilimo bali ni teknolojia nzuri inayorahisisha uzalishaji wa mbegu kwa kupata sifa zinazohitajika kwa haraka ukilinganisha na njia za kawaida na hakuna mtu ambaye alishawahi kutoa ushahidi na kuthibitika kuwa ameyapata kutokana na kutumia mazao yanayotokana na teknolojia hiyo”, alisema Prof. Marc.
Aliongeza “Kuna maneno mengi ya uzushi ya kutisha watu kuwa nchi za Ulaya hazilimi wala kula mazao yatokanayo na teknolojia ya uhandisi jeni lakini niwathibitishie kuwa ubelgiji tunalima na tunaingiza mazao hayo kwa wingi kutoka nchi zinazolima na nchi nyingi za ulaya zinalima na kuagiza kwa wingi sana mazao hayo kwa ajili ya chakula cha binadamu na mifugo”.
Mkutano wa mwaka huu wa Chama cha Wataalamu wa Syansi za Mazao Tanzania (CROSAT) umeanza kwa mkutano wa kisayansi uliobeba kauli mbiu isemayo “Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia teknolojia za uzalishaji wa mazao” na kufuatia na Mkutano mkuu wa Mwaka na umewakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibubda wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari nje ya mkutano huo mara baada ya mjadala huo wa Bioteknolojia kwenye mkutano wa CROSAT jijini Dodoma.
Prof.Marc Heidje kutoka Taasisi ya Flemish ya Bioteknolojia (VIB) ya Ubelgiji akitoa wasilisho lake kwenye mkutano huo.
Rais wa Chama cha Wataalamu wa sayansi za Mazao CROSAT Prof. Kalunde Sibuga akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania TOSCI bwana Patrick Ngwediagi akichangia kwenye mjadala huo.
No comments:
Post a Comment