HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 20, 2024

UNYANYAPAA , MITIZAMO HASI YA JAMII KIKWAZO CHA AJIRA ZA WATU WENYE ULEMAVU

Mwenyekiti wa SHIVYAWATA wilayani Nyamagana,Hamza Nyamakurura,leo akizungumza katika kongamano la watu wenye ulemavu.

Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake na Watoto wa CHAWATA Taifa, Jane Maira, leo akizungumza na waandishi wa habari nje ya koangamano la uchumi na maendeleo la watu wenye ulemavu.
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
SHIRIKISHO la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Wilaya ya Nyamagana,linatambua jitihada za serikali za kuboresha maisha ya Watanzania wakiwemo watu wenye walemavu, mitizamo hasi ya jamii na sekta binafsi kuwa walemavu hawawezi kufanya kazi licha ya kuwa na sifa na elimu ni kikwazo cha kutoajiriwa.

Mwenyekiti wa SHIVYAWATA wilayani humu,Hamza Nyamakurura amesema leo (mwishoni mwa wiki), katika Kongamano la Uchumi na Maendeleo la Watu wenye Ulemavu, lililofanyika katika Bwalo la Mgambo jijini Mwanza, likiwa na kauli ‘Hatutaki omba omba;Tunataka kazi’.

Amesema wanatambua serikali inavyoboresha maisha ya Watanzania wakiwemo watu wenye ulemavu,lakini hali zao za ulemavu zinawakosesha ajira sababu ya mitizamo hasi ya jamii na sekta binafsi kuwaona hawana uwezo wa kufanya kazi.

Nyamakurura amesema kazi ni kielelezo cha utu,inamwezesha mlemavu kufanya kazi na kupata ujira lakini mitizamo hasi ya jamii,walemavu wanaonekana hawawezi kufanya kazi na wao wenyewe kujiona hawana uwezo kumesababisha ugumu wa kuajiriwa,hivyo aliiomba jamii na sekta binafi iwe na mitizamo chanya,washindanishwe katika soko la ajira sababu ya sifa (vigezo),elimu,ujuzi na uwezo.

“Walemavu wameelimika lakini wananyanyapaliwa,tunataka hili liondoke wapewe ajira na fursa katika miradi ya kimkakati na katika masoko ili wafanye biashara wanufaike kiuchumi na kuboresha maisha yao.Mikopo ya asilimia mbili hii imewasaidia baadhi kuboresha maisha,”amesema.


Akifungua kongamano hilo,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwapa kipaumbele walemavu katika masuala mbalimbali yakiwemo ya elimu,afya,uwezeshwaji kiuchumi,huduma za marekebisho,michezo utamaduni na shughuli za kisiasa.

“Lengo la kongamano hili ni kuhamasisha walemavu kutambua haki washiriki katika maendeleo na kujiinua kiuchumi pia,kutambua changamoto na jinsi ya kuzitatua ili waondokane na utegemezi kwa kufanya kazi kama kauli mbiu yao ya ‘Tunataka kazi, Hatutaki omba omba’ inayofanana na ‘Kazi Iendelee’ ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Pia,serikali iko tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayotolewa na watu wenye ulemavu katika kongamano hilo kwa maslahi ya watu wenye ulemavu, inafanya jitihada wapate haki za msingi na ustawi wa maisha yao ya kila siku ndani ya familia zinazowazunguka.

Masalla amesema moja ya jitihada hizo ni kuhakikisha upatikanaji wa haki na huduma za jamii ikiwemo afya na elimu,pia imeimarisha mazingira ya kupatikana elimu kwa jamii ya walemavu ambapo mwaka 2022/23 ilitoa sh. bilioni 4.4 kununua vifaa saidizi vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa shule za msingi nsa sekondari.

Amesema changamoto ya ukosefu wa walimu wenye ujuzi wa kutumia lugha ya alama na kubuni nyenzo rahisi ya kufundishia na kujifunzia kwa viziwi,serikali imeliona hilo na sera ya elimu inakwenda kutatua na kuondoa kabisa changamoto hizo.Naye Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake na Watoto wa CHAWATA Taifa, Jane Maira amesema sheria ya ajira inataka asilimia tatu ya ajira kati ya watu 20 wawe ni wenye ulemavu lakini sekta binafsi bado haizingatii hilo ambapo serikali imeanza kuwashika mkono kwa kuwawezesha kutambua haki zao za msingi na fursa.

Nyamlanga Lwakatare amesema sekta binafsi ndiyo mwajiri wa watu wengi sababu serikali haiwezi kuwaajiri wote,hivyo alishauri kiundwe chombo huru cha kufuatilia ajira za walemavu kwa mujibu wa sheria ili asilimia tatu izingatiwe kati ya waajiriwa 20.

“Tunataka kuikumbusha jamii na serikali wajibu kwa wanayostahili walemavu hususani masuala ya uchumi na changamoto za walemavu, ngazi ya juu serikali imejitahidi shida iko chini katika utekelezaji wa sheria, mazingira yamekuwa magumu ambapo baadhi ya sekta binafsi zinabagua na zinakiuka sheria ya ajira namba 9 ya mwaka 2010,”ameeleza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira na Walemavu,Godfrey Chambo amesema,Tathmini ya Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya Watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 ilifanyika mwaka 2023 kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuzitatua kwa kushirikiana na wadau kwa mazingira ya sasa.
 Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla, leo akifungua kongamano la Uchumi na Maendeleo ya Watu wenye ulemavu wilayania Nyamagana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad