HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 20, 2024

MV CLARIUS YAPINDUKA NA KUZAMA MAJINI NDANI YA ZIWAVICTORIA,ILITIA NANGA BANDARI YA MWANZA KASKAZINI

NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA

MELI ya MV Clarius inayomilikiwa na Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL),leo imepinduka na kuzama majini ndani ya Ziwa Victoria katika Bandari ya Mwanza Kaskazini.

Meli hiyo inayofanya safari zake kati ya Bandari ya Mwanza Kaskazini na Kisiwa cha Ngoziba mkoani Kagera,ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 216 na tani kumi za mizigo, ilirejea Jumamosi alfajiri ikitokea kisiwani humo ikiwa na abiria na mizigo.
Pia,ilielezwa na chanzo makini kuwa meli hiyo ilipinduka Jumamosi (jana) majira ya usiku baada ya kutia nanga bandarini hapo ikisubiri kwenda Ukerewe.

Habari ambazo hazijathibitishwa zimedai MV Clarius ilikuwa ichukue nafasi ya MV Butiama Hapa Kazi Tu,inayofanya safari kati ya Mji wa Nansio na Jiji la Mwanza,inayodaiwa kusitisha safari kwa kinachodaiwa kukosa mafuta.
Aidha, meli hiyo ilifanyiwa matengenezo makubwa mwaka jana,hivyo tukio la kupinduka na kuzama majini ikiwa imetia nanga linazua maswali tata je, ni hujuma au ajali ya kawaida.


Tukio la kupinduka kwa MV Clarius, limetokea siku chache kuelekea maika 28 tangu meli ya MV Bukoba izame ndani ya Ziwa Victoria na kuua zaidi ya watu 800.

“Hebu fikiria hivi meli ingekuwa na abiria nini kingetokea ikiwa katikati ya ziwa,ina maana ingekuwa sawa na ajali ya MV Bukoba,”amesema Mathhew James, mkazi wa Kabuhoro.

Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL,Eric Hamissi akizungumza kwa simu kutoka eneo la tukio,amekiri kupinduka kwa meli ya MV Clarius na wamnafanya jitihada za kuinyayua kutoka majini.
“Hapa tunafanya jitihada za kuinyanyua meli itoke majini,lakini hakuna madhara kwa binadamu maana haikuwa na abiria wala mizigo ndani wakati inapinduka,”amesema.

Eric amesema kwa sasa ni mapema kubaini nini kilichotokea na kusababisha meli ipinduke,hivyo atatoa taarifa rasmi ya nini chanzo baada ya kuinyanyua.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MSCL,baadhi ya mitandao ya kijamii bila kuitaja ilikuwa inarusha taarifa za kupotosha na kuzua taharuki kwa jamii bila uthibitisho wa vyanzo vya kuaminika kuhusu tukuo hilo.


Wakati huo huo MSCL kupitia ofisa habari wake imetoa taarifa ya awali ya kupinduka kwa meli ya MV Clarius ikiwa katika gati la Bandari ya Mwanza Kaskazini.


Ofisa Habari wa MSCL Abdulrahman Ally,akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo,leo amesema meli hiyo bila kutaja sababu ilipinduka ikiwa imetia nanga katika gati la Bandari ya Mwanza Kaskazini.

“MV Clarius inayofanya safari kati ya Bandari ya Mwanza Kaskazini na Kisiwa cha Gonziba,ilirejea salama kutoka kisiwani humo Jumamosi asubuhi ikiwa na abiria na mizigo,iliwashushwa Kirumba kabla ya kuja kuegesha katika Bandari ya Kaskazini,”amesema.

Abdulrahman amesema Mei 19, mwaka huu, majira ya saa 10:00 alfajiri meli ikiwa imetia nanga bandarini hapo,walipata taarifa kutoka kwa walinzi wakieleza kuwa imelalia upande mmoja majini ikiwa gatini.

Ameeleza tangu saa 5:00 hadi saa 9:00 usiku, meli hiyo ilikuwa salama ikielea majini hivyo taarifa za kulalia upande mmoja kisha ikapinduka ziliwashangaza kwa kuwa haikuwa na abiria wala mzigo wowote ndani.

“Kutokana na sababu za kiusalama meli inaposhusha abiria na mizigo katika mwalo wa Kirumba hurejea Bandari ya Mwanza Kaskazini ama Kusini kwa maegesho na kujaza mafuta,inafanya safari kwa wiki mara mbili Jumatatu na Ijumaa,ikitokea dharura ya wingi wa abiria inaondoka Jumatano asubuhi,”amesema Abdulrahman.

Amesema tangu asubuhi wataalamu wa MSCL wanafanya jitihada za kuisimamisha meli hiyo katika hali yake ndipo ufanyike uchunguzi wa kubaini chanzo cha kulalia upande mmoja na kupinduka ambapo meli zingine ninaendelea kutoka huduma kwa wananchi.

Kuhusu madai kuwa Meli ya MV Butiama inayotoa huduma ya usafari kati ya Mji wa Nansio na Jiji la Mwanza kusitisha safari,amesema si ya kweli, kilichotokea ni kuchelewa kuondoka bandarini kwenda Ukerewe kulikosababishwa na kuchelewa kupata mafuta.

“Kama mnavyofahamu serikali inafanya mambo mengi yakiwemo ya ugavi na manunuzi kwa njia ya mtandao,hivyo juzi MV Butiama sababu ya mtikisiko wa internet ilichelewa kupata mafuta, baadaye ilisafirisha abiria na kurudi baada ya mtandao kutengamaa,leo ni kwa sababu ilikolalia MV Clarius,imeshindwa kutoka,”amesema.
Ofisa habari huyo amesema MV Clarius itakaposimamishwa kutoka mjini na uchuguzi ukafanyika taaraifa itatolewa kwa umma na kuwataka wananchi kupuuza uvumi na upotoshaji unaonafanywa na watu kwa maslahi na nia zilizojicha.
Meli ya MV Clarius (katikati) ikiwa imepinduka na kuzama majini ndani ya Ziwa Victoria,katika Bandari ya Mwanza Kaskazini leo.Kulia ni MV Butiama na kushoto ni MV Victoria.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad