HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 4, 2024

YAPI MERKEZI YATOA MSAADA WA SIKU YA EID KWA MAMA MWANA ORPHAN CENTRE

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Yapi Merkezi, ambayo ni Mkandarasi Mkuu wa Reli ya umeme (SGR), imetoa msaada kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Mama Mwana kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu yao ya kujitolea kwa Jamii. Mchango huo umelenga kutoa mahitaji muhimu kwa watoto wanaoishi katika kituo hicho kwa wakati wa sikukuu zijazo za Eid El fitir.

Kampuni hio imetoa msaada wa bidhaa mbalimbali ikiwemo chakula, vifaa vya usafi, mafriji , nguo za Eid ikiwa ni sehemu moja ya kuwapa faraja watoto hao katika kipindi hiki cha sikukuu.

Bi Amisa Juma, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Yapi Merkezi, alitoa shukrani zake za dhati kwa kupata fursa ya kusaidia Kituo cha Watoto Yatima cha Mama Mwana. Alisema, "Yapi Merkezi ina nia ya dhati ya kuleta matokeo chanya katika jamii tunazofanyia kazi. Tunapokaribia msimu wa sikukuu ya Eid, ni jukumu na Furaha kwetu kutoa msaada kwa Kituo cha watoto yatima cha Mama Mwana na kuleta tabasamu kwenye nyuso za hawa watoto wanaostahili."

Bi Juma aliongeza zaidi, "Mchango wetu unaakisi tunu kuu za Yapi Merkezi nazo ni ukarimu, na uwajibikaji wa kijamii.

Tunatumai kupitia mchango huu, tunaweza kuwapa faraja na furaha watoto wa kituo cha Mama Mwana, huku tukiendelea kuwakumbusha kuwa wana haki ya kuthaminiwa na kutunzwa, pamoja na kuhimiza zaidi Makampuni mengine ya kiserikali na kibinafsi kuendelea kufariji Jamii hizi.

Hafla ya kukabidhi msaada huo, iliyoambatana na furaha na shukrani, ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Menejimenti na wafanyakazi wa kampuni ya Yapi Merkezi wakiongozwa na Bw. Levent Doruck, kama Afisa Mkuu wa Fedha wa kampuni iyo, ambaye aliwasilisha dhamira ya dhati ya kampuni hiyo ya kuendelea kusaidia juhudi zinazoendelea za kuboresha mazingira ya watoto yatima au wanaoishi katika hali ngumu.

Mlezi mkuu wa kituo cha Mama Mwana Bi Saada Omar, alitoa shukran zake za dhati na kupongeza kampuni ya Yapi Merkezi kwa moyo na ukarimu wao , huku akiendelea kusisitiza faida na umuhimu wa michango hiyo kwa ustawi wa Watoto hao.

Yapi Merkezi imeahidi kuendelea kukuza ushirikiano na kituo cha Watoto Yatima cha Mama Mwana, ikisisitiza dhamira yake ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na mipango ya maendeleo ya jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad