HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 27, 2024

CRDB Bank kuwawezesha wanachama wa TAPEI kuboresha elimu katika shule binafsi

Dar es Salaam. Tarehe 27 Aprili 2024: Katika kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu nchini, Benki ya CRDB imeasaini mkataba wa ushirikiano na Chama cha Wawekezaji katika Elimu Tanzania (TAPIE) utakaowawezesha wanachama wake kupata mikopo nafuu ya kuboresha miundombinu na kuwezesha uendeshaji wakati wote.

Mkataba huo umesainiwa tarehe 27 Aprili 2024 kwenye mkutano mkuu wa 5 wa mwaka wa TAPEI uliofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt Doto Biteko na kuhudhuriwa na wadau wa elimu nchini.
Akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano mkuu huo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Benki inatambua changamoto wanazokutana nazo wamiliki binafsi wa shule hivyo imechukua hatua za kusaidia kuzitatua ili kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi kusoma na kujifunza.

“Ni ukweli usiopingika kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa lolote lile duniani kwani husaidia kujenga maarifa, ujuzi na kuongeza ufanisi hivyo kuwa kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi. Kwa kuyatambua haya yote, Benki ya CRDB imeiweka sekta ya elimu katika moja ya vipaumbele vyake vya uwezeshaji. Tunafanya hivi ikiwa ni sehemu za kusaidia jitihada za Serikali pamoja na wadau wa sekta hii kutoa elimu bora itikayozalisha rasilimali watu bora katika nyanja mbalimbali,” amesema Raballa.

Kwa kuzitambua changamoto zilizopo ukiwamo ukweli kwamba uendeshaji wa shule unategemea mapato yatokanayo na ada ambayo mara nyingi hukusanywa shule zinapofunguliwa hivyo kuwa na uhaba pindi zinapofungwa, Benki ya CRDB imewaletea mkopo wa uendeshaji ili kukidhi mahitaji yanayopaswa kulipiwa wakati mapato mengine yakisubiriwa indi muhula mpya utakapoanza.
Raballa pia amesema shule nyingi zipo kwenye maeneo ambayo hayajarasmishwa jambo linalowanyima wamiliki uwezo wa kukopa kutokana na kutokidhi vigezo vya dhamana hivyo Benki ya CRDB imewaletea suluhisho kwa kuwaruhusu kukopa fedha zitakazowezesha urasmishaji wa maeneo yao ili kupata hati ya wizara itakayowaruhusu kukopa ili kuimarisha biashara zao.

“Tunawaruhusu wamiliki wa shule kukopa mpaka shilingi milioni 10 kwa ajili ya kurasmisha maeneo ya shule. Fedha hizi ni kwa ajili ya kutafuta hati ya wizara hivyo kuyatambulisha maeneo yao ya kisheria. Vilevile, tunayo mikopo kwa dhamana zisizo rasmi yaani maeneo ya shule ambayo hayana hati. Benki yetu inamruhusu mmiliki kuja kukopa mpaka shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule. Tunaamini kwa utaratibu huu rahisi na rafiki, tutasaidia kuwezesha uwekezaji wa shule katika sekta binafsi,” amesema Raballa.
Wakati wamiliki wakipewa mkopo wa uwekezaji wanaoweza kuurejesha mpaka kwa miaka 7, Raballa amesema walimu na wafanyakazi wa shule binafsi nao wanaweza kupata mkopo kwa ajili ya kufanikisha mambo yao binafsi. Mikopo ya wafanyakazi hawa, amesema inajumuisha ‘salary advance’ ambao ni mahsusi kwa wale ambao mishahara yao inapitia Benki ya CRDB ambao wanaweza kupata mpaka asilimia 50 ya mshahara wao na wakalipa ndani ya siku 30 pamoja na mkopo wa binafsi unaofika mpaka shilingi milioni 100 zinazoweza kurejeshwa kwa mpaka miaka 8. 
 
”Kwa miaka mitatu iliyopita, kiwango cha mikopo ya eimu tuliyoitoa kwa kundi hili imekuwa ikiongezeka. Mwaka 2021 Benki yetu ya CRDB ilikopesha zaidi ya shilingi bilioni 78.66 ambazo zilipanda mpaka shilingi bilioni 86 mwaka 2022 na mwaka jana zikawa shilingi bilioni 97.17. Nitumie fursa hii kuweka wazi kwamba mikopo hii tunayotoa kwa wamiliki wa shule binafsi hasa wanachama wa TAPIE, inaweza kurejeshwa mpaka kwa miaka 7,” amesisitiza Raballa.

Kwa upande wake, rais wa TAPIE, Mahmoud Mringo amesema hadi sasa kuna zaidi ya shule 6,362 zinazojumisha za awali 2,364, za msingi 2,270 na sekondari 1,728 zinazomilikiwa na watu binafsi, mashirika ya dini na yasiyo ya dini, majeshi, na jumuiya za wazazi ambazo zimedahili takriban wanafunzi 1,020,772 kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita ambazo zimeajiri takribani walimu 59,445 na wataalamumwengine zaidi ya 100,000 wenye taaluma na ujuzi mbalimbali kama wahasibu, madereva, wasimamizi na walezi wa wanafunzi, walinzi na wapishi. Ajira hizi zimesaidia kuinua hali za kimaisha kwa watu husika na kupanua wigo wa kodi mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

“Ukitaka kujenga darasa, maabara au kuboresha miundombinu mingine ya shule, ni lazima uende kukopa benki lakini tatizo ni riba kubwa. Kujenga shule ndogo tu kwa sasa unahitaji walau shilingi bilioni 2 lakini kuwa na shule yenye kila kitu basi unahitaji shilingi bilioni 10. Ukizikopa hizi kutoka benki na ukalipa kwa riba iliyopo, itakuchukua miaka 20 ya kumaliza deni ambalo ni lazima lilipwe na mwanafunzi. 
 
Bado kuna kodi na tozo 16 ambazo shule inatakiwa kulipa. Haya mambo yote yanaifanya elimu yetu kuwa ghali na kusoma shule zisizo za serikali inaonekana ni anasa,” amesema Mringo akiiomba serikali iangalie namna ya kupunguza riba ya mikopo tozo pamoja na kodi.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko amepongeza juhudi za sekta binafsi kuchangia kuboresha elimu nchini kwamba zinaifanya jamii iwe na mchango zaidi katika kukuza uchumi. "Niwapongeze kwa ushirikiano na mkataba wa makubaliano mnayosaini leo na Benki ya CRDB. Ili kufanikisha mambo, ushirikiano na wadau wengine ni muhimu sana. Hivi mnavyofanya, ndio namna nzuri ya kukabiliana na changamoto zetu," amesema Dkt Biteko.  


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad