HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 2, 2023

Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe Waaswa kuwekeza zaidi katika Maendeleo ya Kitaaluma na Kitalaamu


Mlau wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Hawa Petro Tundui (aliyebeba rungu), akiongoza maandamano ya kitaaluma kuelekea uwanja wa mahafali, wakati wa Sherehe za Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya.

Mkuu Wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein akiimba mwimbo wa Taifa kabla ya  kuanza  Sherehe za Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu Mzumbe  Ndaki ya Mbeya.

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Eliza Mwakasangula, akizungumza wakati wa Sherehe za Mahafali ya 22 ya Chuo KIkuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya.

Mwenyekiti Wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahya - Othman, akitoa hotuba kwa hadhara iliyohudhuria sherehe ya Mahafali ya 22 Ndaki ya Mbeya.


Wahitimu wa Shahada ya Umahiri wakiimba wimbo wa Afrika Mashariki katika  kitabu cha mahafali.

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein ameuasa Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuwekeza zaidi katika maendeleo ya kitaaluma na kitalaamu katika kuharakisha maendeleo ya chuo kwa kujenga mahusiano na taasisi za elimu za ndani, Afrika Mashariki na nchi za jirani ili kujiimarisha zaidi kitaaluma, kitaalamu na kiuchumi.

Mhe. Dkt. Shein ameyasema hayo katika Mahafali ya 22 ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya yaliyofanyika tarehe Novemba 30,2023 katika viwanja vya Wangari Maathari Courtyard Ndaki ya Mbeya ambapo wahitimu 1,295 katika ngazi mbalimbali za kitaaluma wakiwemo Astashahada, Stashada, Shahada ya Kwanza/Awali na Shahada za Umahiri walitunukiwa stahili zao.

Mhe. Shein ameushauri uongozi wa chuo kuzidisha kiwango cha ushirikiano na sekta binafsi na mashirika ya umma ili kugundua changamoto zao ambazo wanaweza kuzitatua kwa kununua matokeo ya utafiti na shauri za elekezi za kitaalamu ili ziwasaidie kuimarisha bidhaa na huduma zao.

Amesema kupitia tafiti hizo chuo kitaanzisha na kuwa na chanzo cha fedha kwa kutumia mbinu hizo kitakuwa kimeisaidia serikali katika kuleta maendeleo katika wananchi wake.

“hatuwezi kujua fursa gani tunaweza kuzipata lazima tuingie na tuzifungue na pia tuzifatilie hizi sekta binafsi na za umma kwa sababu fursa ni kama ua tena lile lililofumba mtu hawezi kujua uzuri wa ua lilofumba mpaka ua hilo lichanue ndipo utakapo fungua na kudhihirisha sifa zake” Alisisitiza Mheshimiwa Shein.

Aidha Mhe. Dkt. Shein ameutaka uongozi wa Chuo kuwa wabunifu katika ulimwengu wa sasa unaobadilika kwa kasi. Amekitaka chuo kubuni mbinu mbalimbali zitakazowezesha kwenda sambamba na matakwa ya maendeleo ili kuinua sifa ya chuo na kuweza kuinua maisha na hadhi ya watu wanaohudumiwa.

Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mkazo mkubwa na kipaumbele katika sekta ya elimu hapa nchini lakini pia kuendelea kuboresha miundombinu ya chuo Kikuu Mzumbe na kwamba siku za mbeleni kitaweza kupiga hatua kufika anga za kimataifa.

“Fanyeni tafiti na kubuni teknolojia mpya ambazo zitaendana na wakati wa sasa, ajira zina ushindani na wasomi wanaongezeka, serikali imetimiza wajibu kwa kuweka miundobinu katika vyuo vya elimu ya juu haifai kukata tamaa, bali kujiamini na kujituma ndio siri ya maendeleo na dunia ya sasa inahitaji kupambana kwani ajira ni za kupambania hivyo jiongezeeni elimu ili kufungua milango mingine,"amesema Dkt. Shein.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Saida Yahya-Othman amewaasa wahitimu hao kutumia maarifa waliyopata kwa kutafuta na kujipatia ajira kwa bidii na pindi watakapoipata basi wafanyekazi kwa kiwango cha kupaa.

Pia amewaasa kuongeza maarifa kwa kutafiti, kutafakari na kuchambua, wakati wote wakizingatia ukweli bila kuyumbishwa na mtu yoyote katika kutekeleza hayo, wasimame kidete kutetea haki, hasa za wanyonge, kukosoa inapobidi, huku wakizingatia heshima na utu wa wengine.

Aidha amewaasa kuishi kwa kipato halali, bila ya kupinda au kuvunja sheria, huku akitoa rai kuacha mapato ya haraka yajayo bila kufanya kazi au kufuata sheria.

Awali Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Mwegoha akizungumzia upande wa Taaluma amesema kuwa kwa mwaka wa masomo wa 2022/23, Chuo kilisajili jumla ya wanafunzi 13,718 kuanzia ngazi ya Astashahda hadi Shahada ya Uzamivu. Kati yao 8,608 walisajiliwa katika Kampasi Kuu; 3,411 Ndaki ya Mbeya na 1,699 Ndaki ya Dar es Salaam. Baadhi ya hao, ndiyo waliohitimu katika mahafali hayo.

Kwa upande wa utafiti na kujenga uwezo wa wanataaluma, katika mwaka wa masomo wa 2022/23, Chuo kimeendelea kutekeleza jumla ya miradi 17 ya Utafiti inayofadhiliwa na wadau mbalimbali wa maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, Elimu, sayansi na Teknolojia, Biashara na Ujasiriamali kwa vijana, Uchumi, Sheria na Haki za Binadamu, pamoja na Miradi saba ya utafiti inayofadhiliwa na Chuo.

Akizungumza kuhusu Ushirikiano na Taasisi na Vyuo Mbalimbali Ndani na Nje ya Nchi, Prof. Mwegoha alisema kuwa Chuo Kikuu Mzumbe katika kuboresha ushirikiano wake na Taasisi mbalimbali za Elimu ya Juu na Mashirika mbalimbali ya kimataifa, kimejipanga kupanua wigo wa ushirikiano na Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa, kama sehemu ya kutekeleza Dira ya Chuo.

Prof. Mwegoha aemesa Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu kama Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Tanzania (Higher Education for Economic Transformation, (HEET)) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kama mkopo kwa Serikali ya Tanzania.

"Tayari tumeanza utekelezaji wa mradi huu ambao lengo lake ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kuhakikisha kuwa programu katika Vyuo Vikuu zinaendana na soko la ajira. Chuo Kikuu Mzumbe kimetengewa Dola za Kimarekani milioni 21 kwa ajili ujenzi wa majengo ya kufundishia ambapo miradi hii inachukua 79.2% ya fedha zote za mradi, Kupitia mitaala na kutengeneza mitaala mipya iendane na soko la ajira, Kuboresha TEHAMA na miundombinu yake, kuboresha uhusiano wa Chuo na wadau wa nje, Kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Chuo kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kampasi Mpya Tanga.” Alisisitiza Prof Mwegoha

Kwa Mbeya Chuo kimejizatiti kuanza ukarabati wa mabweni ya wanafunzi na kukarabati viwanja vya michezo wakati tukijipanga kuanza mradi mkubwa Iwambi, na hii itategemea sana upatikanaji wa fedha.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad