Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MAMLAKA
ya Masoko ya Mitaji na Dhamana( CMSA) imezindua wa Hatifungani ya Benki
ya NMB ya miaka 10 yenye jumla ya thamani ya Sh.trilioni moja na mauzo
ya toleo la kwanza la hatifungani hiyo yenye mguso na matokeo chanya kwa
jamii.
Akizungumza leo Septemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam
wakati wa uzinduzi huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya
Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama amesema mamlaka hiyo ni taasisi ya
Serikali yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa
nchini.
Ameongeza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba
Hatifungani zinazouzwa kwa umma zinakidhi matakwa ya sheria, taratibu na
kanuni za uuzaji wa hatifungani kwa umma na kukidhi viwango vya
kimataifa.
"Agosti 31 2023, CMSA iliidhinisha Waraka wa Matarajio
wa Benki ya NMB kuuza Hatifungani ya miaka 10 yenye jumla ya thamani ya
shilingi trilioni moja (Tsh 1,000,000,000,000).
" Kwa mujibu wa
taratibu za masoko ya mitaji, CMSA inatoa taarifa rasmi kwa umma kuwa
Benki ya NMB imepata idhini ya CMSA kutoa hatifungani itakayotolewa
katika fedha za aina mbalimbali na hatifungani hii itakuwa na mguso na
matokeo chanya katika maeneo mbalimbali.
"Hatifungani hii inaweka
historia ya kuwa hatifungani kubwa zaidi (bigger ticket size) kutolewa
nchini Tanzania na katika Ukanda Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa
kuzingatia kuwa, Hatifungani hii inatolewa katika fedha za aina
mbalimbali, tunatarajia kuwa itachangia katika jitihada za kukabiliana
na upungufu wa fedha za kigeni hapa nchini, " amesema.
Amefefanua
idhini hiyo imetolewa na CMSA baada ya Benki ya NMB kukidhi matakwa ya
Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania;
Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani.
Pia
uwepo wa Muundo wa Hatifungani yaani Bond Framework ulioandaliwa na
benki ya NMB kwa kushirikiana na Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta ya
Fedha Barani Afrika (FSD Africa) na kukidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya
ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji.
Na hatimaye kupata ithibati
kutoka kwa kampuni ya Sustainalytics ya nchini Uingereza, yenye utaalam
kuhusu miradi endelevu kwa maendeleo ya jamii.
CPA Mkama amesema
mchakato wa kuidhinisha hatifungani unahusisha taasisi na wataalam
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mshauri kiongozi wa benki ya NMB, Absa
Bank Tanzania Limited; Kampuni ya Ushauri katika Masoko ya Mitaji, Orbit
Securities Company Limited; Mshauri wa Sheria, Rex Attorneys.
Pia
Mkaguzi na Mtoa Taarifa za Hesabu, KPMG; Taasisi ya Ushauri kuhusu
muundo wa Hatifungani, FSD Africa; na Taasisi ya utoaji wa ithibati
katika kukidhi matakwa ya miongozo ya jumuiya ya kimataifa katika masoko
ya mitaji, Sustainalytics.
Akieleza zaidi amesema mauzo ya toleo
la kwanza la Hatifungani hiyp iitwayo Jamii Bond kwenye soko la awali
yanafunguliwa leo hii Septemba 25, 2023 na yanatarajiwa kufungwa Oktoba
27, 2023, ambapo benki ya NMB inatarajia kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni
75 (na uwezo wa kuchukua ziada ya shilingi Bilioni 25).
Amesema
fedha zitakazopatikana kupitia hatifungani hii zitatumika kuwekeza
katika miradi endelevu kwa maendeleo ya jamii yaani sustainability
social projects. Baada ya muda wa mauzo kwenye soko la awali kukamilika,
hatifungani hii itaorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.
"Utoaji
wa hatifungani hii ni hatua muhimu katika ustawi na maendeleo ya Sekta
ya Fedha na uchumi hapa nchini kwani utachangia katika utekelezaji wa
Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo
la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekeleza
miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi
shindani kwa maendeleo ya watu.
Pia hatifungani hiyo inawezesha
utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaani
National Economic Empowerement Policy, kwani fedha zitakazo patikana
zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii, na
wananchi watakao wekeza katika hatifungani hii watalipwa riba, hivyo
kuinua vipato vyao.
"Maendeleo na mafanikio katika masoko ya
mitaji yanatokana na mazingira wezeshi na shirikishi ya kisera, kisheria
na kiutendaji yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza sera
ya uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa.
" Hivyo kuwa
chachu yenye matokeo chanya katika maendeleo na ustawi wa sekta ya
fedha, husan masoko ya mitaji.Kutokana na chachu hiyo, sasa tunashuhudia
utolewaji wa bidhaa mpya na bunifu," amesema.
Aneongeza NMB ni
miongoni mwa kampuni ambazo zimetumia fursa katika masoko ya mitaji,
ambapo mwaka 2008, CMSA ilitoa idhini kwa Benki ya NMB kuuza hisa kwa
umma na kuorodheshwa DSE.
Amesema katika mauzo hayo, NMB
ilifanikiwa kupata Sh.bilioni 224.9 sawa na asilimia 357 ya lengo la
kukusanya shilingi bilioni 63. Bei ya hisa za benki ya NMB imeongezeka
kwa asilimia 637 kutoka shilingi 600 kwa hisa wakati wa mauzo ya hisa ya
awali, hadi shilingi 4,420 kwa hisa, leo tarehe 25 Septemba 2023.
Aidha,
mwaka 2016, CMSA ilitoa idhini kwa Benki ya NMB kuuza hatifungani yenye
thamani ya Shilingi Bilioni 200. Hatifungani hii iliuzwa katika matoleo
manne yenye thamani shilingi bilioni 95 ambapo kiasi cha shilingi
bilioni 224.8 zilipatikana sawa na mafanikio ya asilimia 236.7.
"Kutokana
na mafanikio hayo, Benki ya NMB imeweza kutekeleza mikakati mbalimbali
iliyoleta mageuzi na mafanikio yenye tija katika utendaji wa benki na
kwa wanahisa wake. Haya ni mafanikio makubwa.
"Kabla ya kuuza
hisa na kuorodheshwa DSE, NMB ilikuwa ikipata hasara na hivyo kutoweza
kutoa gawio kwa mwanahisa wake yaani Serikali, " amesema CPA Mkama.
Uzinduzi
huo umehudhuriwa na Msajili Wa Hazina - Bw. Nehemiah Mchechu,
Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede; Afisa Mtendaji Mkuu wetu -
Bi. Ruth Zaipuna; Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana (CMSA) – CPA. Nicodemus Mkama; Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko
la Hisa la Dar Es Salaam (DSE) - Bi. Mary Mniwasa; pamoja na
wawakilishi kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kushoto), akipokea Waraka
wa Matarajio ya Programu ya Utoaji wa Hati Fungani ya Muda wa Kati (MTN)
kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, wakati wa uzinduzi wa NMB Jamii
Bond.
Wageni waalikwa kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA
Nicodemus Mkama akizungumza jambo mbele ya wagani waalikwa mbalimbali
wakati wa uzinduzi wa Hatifungani ya Benki ya NMB ya miaka 10 yenye
jumla ya thamani ya Sh.trilioni moja na mauzo ya toleo la kwanza la
hatifungani hiyo yenye mguso na matokeo chanya kwa jamii.
Monday, September 25, 2023
Home
HABARI
CMSA YAZINDUA HATIFUNGANI BENKI YA NMB YENYE THAMANI YA SHILINGI TRILIONI MOJA,SERIKALI YAPONGEZWA
CMSA YAZINDUA HATIFUNGANI BENKI YA NMB YENYE THAMANI YA SHILINGI TRILIONI MOJA,SERIKALI YAPONGEZWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment