OFISA
Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema benki hiyo
inayofuraha kupata idhini ya kutangaza programu yao ya Hatifungani ya
Jamii ya miaka 10 ambayo thamani yake ni Sh.trilioni moja na kufungua
dirisha la uwekezaji wa toleo la kwanza la hatifungani ya NMB Jamii
Bond.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa hatifungani hiyo
uliofanyika jijini Dar es Salaam Zaipuna amefafanua hatifungani ya NMB
Jamii Bond itakuwa ni ya miaka mitatu itakayo dumu hadi Novemba 2026.
Ameongeza wawekezaji kwenye hatifungani hiyo watajipatia riba ya asilimia asilimia 9.5 kwa mwaka, inayolipwa mara nne kwa mwaka.
"Kiasi
cha chini cha ununuzi wa hati fungani hii ni Sh.500,000 na inaweza
kununuliwa kwa kujaza fomu zinazopatikana kwenye matawi yote ya Benki ya
NMB, au mawakala wa Soko la Hisa la Dar es Salaam waliopewa leseni na
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
"Dirisha la
uwekezaji la hatifungani hii ya NMB Jamii Bond lipo wazi kuanzia sasa
hivi na mwisho wa kupokea maombi ya ununuzi ni Ijumaa 27 Oktoba 2023 saa
kumi na moja jioni."
Ameeleza baada ya hapo hatifungani hiyo
itaorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) kuwapa fursa
wale ambao hawakuwekeza kwa wakati iko wazi kwa umma, wakimaanisha
zinaweza kununuliwa na watu binafsi, makampuni na pia taasisi.
"Tumeweka
malengo ya kukusanya Sh. Bilioni 75, huku Mamlaka ya Masoko ya Mitaji
na Dhamana (CMSA) ikiruhusu ongezeko la mpaka Sh. bilioni 25."
Kuhusu
Toleo hilo la Kwanza amesema Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana
(CMSA) imeidhinisha uuzaji wa hatifungani ya dola za kimarekani million
10 ikiruhusu ongezeko la mpaka dola za kimarekani milioni tano na
kufanya kuwa na dola milioni 15, itakayouzwa kwa mashirika na wawekezaji
walioko nje ya Tanzania.
Zaipuna amesema hatifungani ya Jamii
ambayo imezinduliwa inalenga kukusanya fedha ambazo zitatuwezesha kutoa
mikopo inayolenga kuleta matokeo chanya kwenye jamii.
Ametoa
mfano wa mikopo hiyo ni mikopo kwa ajili ya miradi ya nishati mbadala,
kuzuia na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, usimamizi wa maji na maji
taka, usafiri safi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia
kuwapa nguvu wanawake na usawa wa kijinsia, nyumba za bei nafuu, usalama
wa chakula, huduma muhimu (afya na elimu), na Vijana.
Ametumia
nafasi hiyo kuwashukuru wote waliowaunga mkono na kusaidia hatifungani
hiyo kuingia sokoni. "Naomba kulishukuru shirika la Financial Sector
Deepening Africa (FSD Africa) kwa kuileta hatifungani hii katika soko.
"NMB
tumefanya kazi na FSD Africa ambao walitoa mchango mkubwa wa Kitaalam
katika mfumo wa hatifungani hii. Vilevile tulipata msaada wa Kitalaam
kwa ajili ya maoni ya upande wa pili (yaani Second party Opinion) kutoka
kampuni ya Sustainalytics.
"Niwashukuru Bodi na Uongozi wa
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bodi na Uongozi wa Soko
la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Benki Kuu ya Tanzania, Mshauri mwenza
ABSA Bank Tanzania Limited alieshirikiana na wataalamu wetu ndani ya
Benki ya NMB."
Wengine ambao amewashukuru ni Mshauri wa Sheria,
Rex Attorneys, Mtoa Taarifa za Mahesabu, KPMG na Dalali mdhamini, Orbit
Securities Limited pamoja na Msajili wa Hazina.Msajili
wa Hazina, Nehemia Mchechu (katikati), Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya
NMB, Ruth Zaipuna (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede (kulia) wakizindua kwa pamoja Hati Fungani
ya Jamii ya NMB 'NMB Jamii Bond' jijini Dar es Salaam leo Septemba 25,
2023.








No comments:
Post a Comment