HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 20, 2023

UFAFANUZI WA UWEPO WA HALI YA EL NIÑO KATIKA BAHARI YA PASIFIKI NA ATHARI ZAKE NCHINI

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa taarifa juu ya mwenendo wa uwepo hali ya El Niño katika bahari ya Pasifiki na athari zake nchini.

Imeeleza kuwa, El Niño ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na uwepo wa ongezeko la joto la bahari la juu ya wastani katika eneo la kati la kitropiki la bahari ya Pasifiki. Hali hii huambatana na athari mbalimbali ikiwemo ongezeko la mvua, joto na hali ya ukame katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Taarifa iliyotolewa leo Julai 19,2023 na TMA imeeleza kuwa ukubwa wa athari hizo unategemea nguvu pamoja na muda ambao hali ya El Niño itadumu, na pia inategemea hali na mwelekeo wa mifumo mingine ya hali ya hewa ikiwemo mwelekeo wa upepo na joto la bahari.

"Katika Bahari ya Hindi Kwa Tanzania, hali ya hii ya El Niño huambatana na vipindi vya mvua kubwa na za juu ya wastani na hivyo Mamlaka inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa ikiwemo El Niño" imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Imeelezwa kuwa, kwa ujumla mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuanza kujitokeza kwa El Niño, hali ambayo inatarajiwa kuimarika zaidi kuelekea mwishoni mwa mwaka 2023 huku uchambuzi wa awali wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa El Niño itakuwa na nguvu ya wastani.

Hata hivyo, athari za moja kwa moja hazijaanza kujitokeza katika maeneo ya nchi yetu kwa kipindi hiki cha Kipupwe lakini Mamlaka inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo mbalimbali ya hali ya hewa kwa ukaribu na kufanya uchambuzi wa kina utakaoainisha athari za El Niño katika mifumo ya mvua hususan msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba), 2023 na taarifa hiyo itajumuisha ushauri stahiki kwa sekta mbalimbali na itatolewa kabla ya kuanza kwa msimu.

Kwa upande mwingine, mamlaka imesema, msimu wa Kipupwe (Juni-Agosti), 2023 bado unaendelea huku vipindi vya upepo mkali pamoja na baridi vikieendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi.

"Hali ya baridi kali imeendelea kujitokeza katika maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi (ikijumuisha mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa) na maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kaskazini mashariki. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2023 kiwango kidogo zaidi cha joto la chini cha nyuzi joto 2.50C kimeripotiwa katika kituo cha Uyole, Mbeya mwanzoni mwa mwezi Julai.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad