HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 22, 2023

MAAFISA UDAHILI WA WAPONGEZA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO

Meneja wa Utahini na Utunuku wa Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Twaha Twaha akitoa maelezo kuhusiana na  utaratibu unaotumika kwa wanafunzi kujiunga katika  vyuo , jijini Dar es Salaam. MAAFISA Udahili 165 kutoka Vyuo mbali mbali vya Zanzibar na Bara vikijumuisha vile vya SAT, BTP na HAS leo tarehe 21 Julai,2023, wamepongeza juhudi za NACTVET kuwaandalia Mafunzo ya kuwajengea uwezo katika taratibu sahihi za udahili wa wanafunzi vyuoni na wasilishaji wa waombaji kwenye mfumo wa NACTVET na masuala ya utahini.


Akifungua rasmi mafunzo hayo ya siku moja, kwenye ukumbi wa mikutano wa NACTVET, Kanda ya Mashariki, Mkurugenzi wa Udahili, Utahini na Utunuku, Dkt. Marcelina Baitilwake amesema Maafisa udahili ndiyo wajenzi wa msingi wa hatma mwanachuo katika safari kutafuta maarifa kuanzia maombi ya kujiunga na chuo hadi anapohitimu.

Amekumbusha kwamba suala la udahili wa wanafunzi katika vyuo vyao ni muhimu lifanyike kwa kuzingatia miongozo ya NACTVET ili kuwasaidia waombaji kuwa na uhakika na taarifa zao kwenye Mfumo wa Baraza hatua kwa hatua.

Dkt. Baitilwake amewataka kuzingatia maelekezo ili kuondoa changamoto zinajitokeza kutokana na baadhi ya Maafisa udahili kutokuwa na weledi na umahiri kuanzia ngazi ya kuwadahili waombaji kwenye programu mbali mbali vyuoni, hali inayosababisha taarifa na matokeo ya baadhi ya wanavyuo kutothibitika kwenye Mfumo wa Baraza na hatimaye kusababisha usumbufu usio wa lazima.

Aidha, maafisa udahili hao wameipongeza NACTVET kwa maelekezo waliyopata kwenye mada mbali mbali zilizowasilishwa na wataalam wa Mfumo wa NACTVET na kuahidi kuyafanyia kazi yote waliyojifunza ili kuboresha huduma za udahili, uwasilishaji matokeo na uhamisho wa wanavyuo pindi wanapohitaji kufanya hivyo kwa kuzingatia matakwa ya Mfumo wa Baraza.
Mkurugenzi wa  Udahili, Utahini na Utunuku wa  Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt. Marcelina Baitilwake akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa maafisa udahili kuhusiana na kufuata kanuni na weledi wakati wa udahili wa wanafunzi na matokeo ya wanafunzi wanaojiunga  kwa mwaka wa masomo 2023/2024,  jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Maafisa Udahili wakiwa katika Mkutano ulioandaliwa na NACTVET jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad