HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 20, 2023

CMSA:MAZINGIRA MAZURI YALIYOWEKWA NA SERIKALI YAMEKUWA NA MATOKEO CHANYA KATIKA MAENDELEO YA SEKTA YA FEDHA

 
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) Nicodemus Mkama amesema mazingira wezeshi yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan yamekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 7.87 na kufikia Sh.trilioni 35,39 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023 ikilinganishwa na Sh. trilioni 32 kipindi kilichoishia Aprili 2022.

Aidha thamani ya uwekezaji katika Soko la Hatifungani (Hatifungani za Serikali na Hatifungani za Kampuni) imeongezeka kwa asilimia 16.53 na kufikia Shilingi trilioni 18.37 katika kipindi kilichoishia Aprili 2023, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 15.76 katika kipindi kilichoishia Aprili 2022.

Akizungumza Mei 19,2023 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Toleo la Nne la Hatifungani ya Kampuni ya TMRC katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Kamishna wa Usimamizi wa Deni la Taifa Japhet Justin aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dk.Natu El-Maamry , Mkama amesema kuorodheshwa kwa hatifungani ya TMRC kunafanya, Jumla ya thamani ya uwekezaji katika Soko la Hatifungani kufika Sh.trilioni 18.38 na jumla ya thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji kufika Sh.trilioni 35.40.

“Hivyo tunatoa pongezi kwa taasisi na wataalam wote walioshiriki katika kuwezesha mafanikio haya. Taasisi na wataalam hao ni pamoja na Bodi na Uongozi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bodi na Uongozi wa Soko la Hisa la Dar Es Salaam, Bodi na Uongozi wa Kampuni ya TMRC, Mshauri kiongozi wa Kampuni ya TMRC, Orbit Securities Company Limited, Mshauri wa Sheria, Abenry and Company Advocates, Mkaguzi na Mtoa Taarifa za Mahesabu, PriceWaterhouseCoopers (PWC).

Ninatambua kwamba, kazi hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini mmeweza kufanya kazi yenu vizuri na hivyo kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa. Hongereni sana!!

“Fedha zilizopatikana kupitia mauzo ya toleo la nne la hatifungani hii zitatumika kutekeleza Mpango Mkakati wa kutoa mikopo kwa benki zinazotoa mikopo ya nyumba kwa lengo la kuboresha makazi ya wananchi na kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Nyumba na Uendelezaji Makazi.

Kama mnavyofahamu, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuona kuwa Sekta ya Fedha inawezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo yenye lengo la kuchangia ukuaji na ustawi wa sekta binafsi; umma na uchumi wa nchi kwa ujumla. Hivyo basi, Hatifungani ya TMRC inatoa mchango mkubwa katika kutekelezwa kwa dhamira hiyo.

“Pia uorodheshwaji wa toleo la nne la hatifungani ya TMRC katika soko la hisa unawapatia fursa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale wanapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine; kujua thamani halisi ya hatifungani zao; na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizo, ambapo wawekazaji hao hupata riba kama faida itokanayo na uwekezaji huo.

Aidha, uorodheshwaji wa hatifungani za kampuni unaongeza utawala bora na ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni na kumwongezea mwekezaji wigo na fursa za uwekezaji. Hii inamsaidia mwekezaji kuwa na anuwai, jambo ambalo hupunguza athari za uwekezaji (Risk Diversification).,”amesema

Amefafanua uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya mitaji unachangia utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha); kuongezeka kwa akiba hapa nchini; kupanuka kwa uwekezaji unaoleta ongezeko la ajira; Mapato kwa njia ya kodi kwa Serikali na kuinua kipato cha watanzania kwa ujumla.

Hivyo ametoa mwito kwa benki za biashara, benki za wananchi, Kampuni za bima, binafsi na za umma kutumia fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuuza hisa na hatifungani kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ili kuongeza uwezo wa rasilimali fedha.

Mkama amesema masoko ya mitaji ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi wa Taifa kwa ujumla. Benki za biashara hapa nchini kama Benki ya NMB, CRDB, DCB, Exim, Standard Chartered na benki za nje kama Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na Benki ya Maendeleo ya Biashara Afrika (PTA-TADB) zimekuwa zikitumia masoko ya mitaji hapa nchini kuongeza rasilimali fedha, hivyo kuimarisha uwezo wa benki na taasisi hizo kutoa huduma kwa wateja katika sekta ya umma na sekta binafsi.

Ametoa rai kwa wadau wote wa masoko ya mitaji kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana katika kutekeleza mikakati ya kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini ikiwemo kuleta bidhaa mpya katika masoko haya ambazo zitaweza kuorodheshwa katika Soko la Hisa ili pamoja na mambo mengine kuwapatia wawekezaji taarifa mbalimbali kuhusiana na bidhaa hizo ikiwemo bei kwa namna iliyo wazi. “Hatua hii ni muhimu kwani, maendeleo ya masoko ya mitaji ni injini ya kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.”

Awali wakati anaanza kuzungumza kwenye hafla hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu huyo amesema uwepo wadau mbalimbali kwenye hafla hiyo akiwemo mgeni rasmi Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango ni uthibitisho wa dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira shirikishi, bora na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji yenye lengo la kukuza uwekezaji kupitia masoko ya mitaji na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla hapa nchini.

“Hii ni uthibitisho kwamba sekta ya fedha ina wadau wengi wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kujenga masoko ya mitaji endelevu, yenye ufanisi na hivyo kuchangia katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, kadiri Taifa letu linavyosonga mbele katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 unaolenga kujenga “Uchumi Shindani kwa Maendeleo ya Watu”, mahitaji ya rasilimali fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii na uchumi, hususani miundombinu yanaongezeka.

“Ili kufanikisha azma hii, kunahitajika uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya fedha, ikiwa ni pamoja na hatifungani za kampuni kama hatifungani hii ya TMRC. Aidha, uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya mitaji unachangia utekelezaji wa Sera za Fedha katika Uchumi na Sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi;

kuongezeka kwa akiba hapa nchini; kupanuka kwa uwekezaji unaoleta ongezeko la ajira; Mapato kwa njia ya kodi kwa Serikali na kuinua kipato cha watanzania kwa ujumla.CMSA iliidhinisha maombi ya kampuni ya TMRC kuuza toleo la nne la hatifungani lenye thamani ya Sh. bilioni 10 kwa umma, ikiwa ni sehemu ya Programu ya Hatifungani ya TMRC yenye thamani ya Sh. bilioni 120.

Idhini ilitolewa na CMSA baada ya TMRC kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya utoaji wa Hatifungani kwa umma yaani “Capital Markets and Securities (Guidelines for the issuance of Corporate Bonds,”amesema.

Aidha amesema Hatifungani hiyo imekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya Mitaji huku akifafanua mauzo ya toleo la nne la hatifungani ya TMRC yalifunguliwa Aprili 3 mwaka 2023 na kufungwa Aprili 24 mwaka 2023, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 11.28 kimepatikana, ikilinganishwa na Sh. bilioni 10 zilizotarajiwa kupatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 112.81.

Mkama amesema mauzo ya hatifungani hii yamekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya masoko ya mitaji na Sekta ya Fedha kwa ujumla hapa nchini, ambapo asilimia 68.6 ya wawekezaji walioshiriki ni wawekezaji wadogo wadogo (Retail Investors) na asilimia 31.4 ya wawekezaji ni Kampuni na Taasisi (Institutional investors). Aidha, asilimia 100 ya wawekezaji ni wawekezaji wa ndani.

Hatua hiyo ni muhimu kwani imewezesha utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha yaani National Financial Inclusion Framework wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha ikiwa ni pamoja na masoko ya mitaji. Hivyo, tuna kila sababu ya kuipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa TMRC pamoja na wadau wote walioshiriki katika kuwezesha mafanikio haya. Hongereni Sana!!.

“ Mafanikio haya yametokana na imani waliyonayo wawekezaji kwa kampuni ya TMRC na kwenye masoko ya mitaji hapa nchini. Pia ni matokeo ya elimu ya uwekezaji inayoendelea kutolewa kwa umma na wadau katika sekta ya fedha kuhusu fursa na faida za kuwekeza katika masoko ya mitaji. Aidha, mafanikio haya ni sehemu ya mazingira wezeshi yaliyotolewa na Serikali, ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi ya zuio kwenye hatifungani za kampuni kama ilivyo kwa hatifungani za Serikali.

“Vile vile, mafanikio haya yametokana na kushushwa kwa kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji kutoka Shilingi milioni moja hadi laki tano. Hatua hizi zina matokeo chanya katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha yaani Financial Sector Development Master Plan 2019/20 – 2029/30” wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu; na Mpango Kazi wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo yaani Alternative Project Financing (APF) Strategy wenye lengo la kuwezesha Serikali na Sekta Binafsi kupata rasilimali fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.”


Mgeni rasmi Kamishna wa Usimamizi wa Deni la Taifa Japhet Justin aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dk.Natu El-Maamry (wa nne kulia) akigonga kengele kuashiria uorodheshwaji rasmi kwa Toleo la Nne la Hatifungani ya Kampuni ya Utoaji mikopo kwa Mabenki na taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo ya nyumba Tanzania (TMRC) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Mgeni rasmi Kamishna wa Usimamizi wa Deni la Taifa Japhet Justin aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dk.Natu El-Maamry , akizungumza mbele ya Wageni mbalimbali waliofika kwenye hafla ya kuorodheshwa kwa Toleo la Nne la Hatifungani ya Kampuni ya Utoaji mikopo kwa Mabenki na taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo ya nyumba Tanzania (TMRC) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam iliofanyika jana.
OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Nicodemus Mkama akizungumza mbele ya Wageni mbalimbali waliofika kwenye hafla ya kuorodheshwa kwa Toleo la Nne la Hatifungani ya Kampuni ya Utoaji mikopo kwa Mabenki na taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo ya nyumba Tanzania (TMRC) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam iliofanyika jana.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC Ndugu Oscar Mgaya akizungumza mbele ya Wageni waalikwa mbalimbali waliofika kwenye hafla ya kuorodheshwa kwa Toleo la Nne la Hatifungani ya Kampuni ya Utoaji mikopo kwa Mabenki na taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo ya nyumba Tanzania (TMRC) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam iliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Nicodemus Mkama akimpongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC Ndugu Oscar Mgaya mara baada ya hafla ya kuorodheshwa kwa Toleo la Nne la Hatifungani ya Kampuni ya TMRC katika Soko la Hisa la Dar es Salaam iliofanyika jana.


Wageni waalikwa mbalimbali wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri katika hafla hiyo


Picha mbalimbali za pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad