HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 19, 2023

Watu 420 wapimwa moyo Manyara

 

 Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone Kayandabila akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi (Echocardiogram – ECHO) mwananchi wa Manyara aliyefika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) kwa ajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH na kumalizika leo Mkoani Manyara.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Wamara akimpima kipimo cha kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) Glory Ifunya aliyefika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) kwa ajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH na kumalizika leo Mkoani Manyara.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimfanyia uchunguzi mwananchi wa Manyara aliyefika katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) kwa ajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH na kumalizika leo Mkoani Manyara

Na: Mwandishi Maalum – Manyara
JUMLA ya watu 420 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalum ya siku tano iliyoanza tarehe 15 Mei 2023 na kumalizika leo katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH).

Kambi hiyo iliyofanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) imewahudumia watu wazima 390 na watoto 30.

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone Kayandabila alisema katika kambi hiyo wametoa rufaa kwa wagonjwa wa moyo 99 ambapo kati yao wagonjwa 10 walikuwa watoto na wagonjwa 89 walikuwa watu wazima ili waweze kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Sababu za kutoa rufaa kwa wagonjwa hao ilikuwa ni pamoja na matatizo mbalimbali yanayotokana na athari za magonjwa ya shinikizo la juu la damu, sukari kuwa juu, mishipa ya damu kuziba pamoja na valvu za moyo kutokufanya kazi vizuri”,

“Magonjwa mengine tuliyokutana nayo wakati wa kambi hii ni matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo kutokufanya kazi vizuri na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kwa watoto yaani matundu kwenye moyo”, alisema Dkt. Johnstone

Aidha Dkt. Johnstone alitoa wito kwa wagonjwa waliopewa rufaa kufika JKCI ili waweze kupatiwa matibabu kwa haraka kupunguza athari zitakazoweza kujitokeza kama hawatapata matibabu kwa wakati.

Naye Mganga Mfadhiwi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara Dkt. Catherine Magali amewapongeza madaktari bingwa wa moyo kutoka JKCI kwa kutoa huduma kwa wananchi wa Manyara kwani huduma hizo ni muhimu kufanyika mara kwa mara.

“Kuwapata watu 99 rufaa kwa wiki moja sio kazi ndogo, mmefanya kazi ya ziada kwani watu hawa wangeendelea kuishi tu huku bila ya kujua yakuwa walihitaji matibabu ya haraka kuokoa maisha yao”, alisema Dkt. Catherine

Dkt. Catherine ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya wanawake MRRH alisema mwanzo wa ushirikiano uliojengwa katika kambi hiyo uendelee hata pale Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara itakapowahitaji tena mabingwa hao kutoka JKCI wasisite kushirikiana nao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad