HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 20, 2023

WARSHA YA TANO EACO YAWAKUTANISHA WADAU KUJADILI KUKITHIRI KWA TAKA ZA KIELEKTRONIKI


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) Dkt. Jabiri Bakari akizungumza wakati wa warsha hiyo na kueleza mpango mkakati wa Mamlaka hiyo utakaoanza mwezi Mei mwaka huu, Leo jijini Dar es Salaam.

*Tanzania yachangia tani milioni 260 ya taka za kieletroniki duniani, TCRA kuja na mkakati Mei


WARSHA ya Tano ya Shirika Mawasiliano la Afrika Mashariki (EACOA,) imewakutanisha wadau kutoka Nchi Saba wanachama na kujadili mikakati ya kupambana na kutokomeza taka za kielektroniki ambazo zimeendelea kukua kwa kasi katika Ukanda wa Nchi hizo na kuweza kupelekea athari za kiafya na kimazingira.

Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo ya siku tatu ya uhamasishaji usimamizi wa taka za kielektroniki iliyoandaliwa na kuratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) kama mwanachama wa EACO na kufanyika leo jijini Dar es Salaam, Tanzania Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema EACO imekuwa ikifanya mikutano kadhaa ambapo katika mkutano huo wa tano uliowakutanisha wadau kutoka nchi Saba umeangazia taka zinazotokana na vifaa vya kielektroniki ambalo ni tatizo linaloendelea kukua pamoja na mikakati ya kuziondoa.

"Tatizo hili la taka za kielektroniki linakua kwa kasi, watu wengi hawafahamu wapi wapeleke vifaa hivyo vikiharibika hivyo wanavitupa ambayo ni hatari zaidi kwani vingi hugeuka sumu na hata kujeruhi watu." Amesema.

Amesema mkutano huo ni muhimu kwa taifa kwa kuleta juhudi na jitihada za pamoja na kujadili namna bora ya kushughulikia taka hizo ambazo zimekuwa zikiongezeka kutokana na kukua kwa teknolojia na vifaa vingi kupitwa na wakati.

Akizungumza katika kongamano hilo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Afrika la Mashariki (EACOA,) Dkt. Ally Simba amesema taka za kielektroniki zimekuwa zikiongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na kukua kwa teknolojia na kufuatia hilo TCRA wamekuwa wadau wakubwa wa kuwakutanisha wadau na kujadili namna bora ya kupambana na kudhibiti taka za kielektroniki.

"Kutokana na kukua kwa teknolojia vitu vipya kama simu, redio na televisheni hununuliwa kila siku na baada ya muda huaribika na kuwa taka, pia tumekuwa tukipokea misaada ya vitu vinavyokaribia kuisha muda wake kutoka nje ya Nchi mwisho tunakuwa dampo baada ya vifaa hivyo kuharibika." Amesema.

Dkt. Simba amesema nchi wanachama kupitia mkutano huo watatoka na mikakati kupitia malengo ya miaka mitano ikiwemo kutoruhusu kupokea msaada wa vifaa vya kielektroniki vinavyokaribia kuisha muda wake wa matumizi na kutumia fursa zilizopo katika taka hizo kama madini yenye faida na kuteketeza taka zisizohitajika kwa kufuata sheria na matakwa ya mazingira.

Aidha amesema ukuaji wa taka za kielektroniki kwa Tanzania umeongezeka kutoka Tani 2000 mwaka 1998 hadi kufikia Tani kumi na Tisa elfu mwaka 2019 hali iliyopelekea kuchangia Tani milioni 260 duniani.

"Taka hizi zikitupwa ardhini huzalisha sumu na kuharibu ardhi na hazitakiwi kuchanganywa na taka nyingine hivyo kupitia kusanyiko hili tunategemea kubadilishana uzoefu na kubwa zaidi ni kujenga uelewa zaidi juu ya namna ya kukusanya na kuhifadhi taka hizi pamoja na kuzitumia kama fursa ya biashara." Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) Dkt. Jabiri Bakari amesema, TRCA kama msimamizi wa sekta ya mawasiliano madhumuni ya semina hiyo ni kufanyia kazi matokeo ya tafiti zilizofanyika na wadau mbalimbali kutoka Serikali za mitaa, wadau wa mazingira na watafiti kutoka Vyuo vikuu watajadili kwa pamoja na kutoka na njia sahihi katika eneo hilo la taka za kielektroniki.

"Kasi ya ukuaji wa taka za kielektroniki imeongezeka kutokana na kukua kwa teknolojia, vipo vifaa vinavyokuja vipya vingine feki na vile ambavyo vinakuja ikiwa muda wake umekaribia kuisha na vinaishia hapa ni vyema tukachukua hatua ili kupambana na kasi ya kuongezeka kwake." Amesema.

" Kwa kuonesha msisitizo katika hili mwezi Mei mwaka huu TCRA tutaanza programu ya kuhakikisha vifaa hivyo kabla ya kuingia nchini kazi inafanyika kuanzia kule vinakotokea ili kuiwezesha Mamlaka kusimamia Ecosystem ya taka hizi zikiwa Tanzania."

Pia amesema taasisi chache zimeelimika na zimeanza kufanya kazi hizo kwa kukusanya taka hizo na kuzitenganisha kwa kuzingatia matakwa ya mazingira na wanatumia fursa katika biashara na kuteketeza taka zisizo na matumizi kwa kufuata sheria na matakwa ya mazingira.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akizungumza wakati akifungua warsha ya 5 ya uhamasishaji wa usimamizi wa taka za kielektroniki iliyoandaliwa na kuratibiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TCRA,) na kueleza jitihada za haraka zinatakuwa kuchukuliwa ili kudhibiti ongezeko la kasi la taka hizo, Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano la Afrika Mashariki (EACOA,) Dkt. Ally Simba akizungumza wakati wa warsha hiyo na kueleza kuwa vifaa vya msaada vinavyokaribia kuisha muda wake wa matumizi kutoka nje ya Nchi vichangia kwa kiasi kikubwa kwa kuongezeka kwa taka za kielektroniki katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais anayeshughulikia mazingira Dkt. Omar Shajack akitoa salamu katika warsha hiyo na kuhimiza ushirikiano baina ya Nchi wanachama, Leo jijini Dar es Salaam.




Baadhi ya washiriki wakifuatilia warsha hiyo, Leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad