HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 1, 2023

WARATIBU WA MIRADI YA UMEME VIJIJINI MKATENDE HAKI KWA WANANACHI NA KUTOIANGUSHA SERIKALI - WAZIRI MAKAMBA


Waziri wa Nishati, Januari Makamba amewaasa vijana walioajiriwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa nafasi ya Waratibu Miradi ya Umeme Vijijini kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi ili kulinda imani iliyooneshwa na Serikali kwao.

Akizungumza Jijini Dodoma Februari 28, 2023, Makamba amewataka vijana hao 136 waliofaulu usaili wa nafasi husika, kwenda kuwatendea haki wananchi walengwa ambao ni wa maeneo ya vijijini nchi nzima, kwa kuhakikisha kiu yao ya kufikiwa na umeme inatimizwa.

“Wale wenzenu ambao hawakubahatika siyo kwamba hawakuwa na vigezo. Takribani wote waliotuma maombi walikuwa na vigezo lakini kutokana na nafasi zilizohitajika kuwa ni 136 tu, ndiyo maana wachache wenu kutoka kundi hilo mkabahatika. Ichukulieni fursa hii adhimu kuchapa kazi na kudhihirisha hatukufanya makosa kuwachagua,” amesisitiza.

Akifafanua, amesema kazi ya kupeleka umeme vijijini inaendelea vizuri ambapo hadi sasa takribani asilimia 80 ya vijiji vyote Tanzania Bara vimeshafikiwa na umeme lakini pamoja na takwimu hizo nzuri, kumekuwepo na uzorotaji na uchelewaji wa kupeleka nishati hiyo kwa baadhi ya vijiji kutokana na usimamizi hafifu.

“Kwahiyo, ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hii kwa uzuri, ubora na viwango vinavyotarajiwa, Wizara kupitia REA tukaomba kibali maalumu serikalini, kuajiri Waratibu wa Miradi ya Umeme Vijijini katika kila Wilaya ili watusaidie na tunashukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia.

Amesema kazi nyingine watakayoifanya vijana hao ni kusaidia kutoa taarifa za haraka zaidi kwa wananchi, inapotokea changamoto ya uchelewaji mradi pamoja na kufanya mawasiliano na viongozi mbalimbali wa maeneo husika kuanzia ngazi ya Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri ili wawe wanajua wakati wote nini kinaendelea katika maeneo hayo.

“Nia yetu sisi ni kwamba tuharakishe utekelezaji wa kupeleka umeme vijijini ili kufikia Desemba 2023, vijiji vyote viwe vimefikiwa na umeme, kwa sababu tayari kila kijiji kina Mradi, bajeti ipo na wakandarasi wako eneo la kazi. Shida yetu ilikuwa ni utekelezaji wa kasi ambapo vijana hawa watatusaidia kuhakikisha kasi inakuwepo.”

Kwa muda wa siku mbili kuanzia Februari 27, 2023, Waratibu Miradi hao 136 walikuwa wakipatiwa mafunzo mafupi na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo yalilenga kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Vijana hao wameajiriwa kwa Mkataba wa miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad