HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 1, 2023

DC OKASH AWAASA WATENDAJI KUWATUMIKIA WANANCHI KWA KWENDA NA KASI YA RAIS SAMIA

  Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

HALMASHAURI ya wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani ,imepokea pikipiki sita kutoka Serikalini kwa ajili ya kuondoa changamoto ya usafiri kwa watendaji kata, ambao wakati mwingine wanashindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na baadhi ya maeneo kutofikika kirahisi.

Akikabidhi Pikipiki hizo kwa watendaji kata hao, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Halima Okash aliwaasa watendaji kuwatumikia wananchi,kwa kutoka Ofisini na kwenda kwenye Maeneo Yao kujua kero zao na kuzitatua.

"Serikali inatambua majukumu na changamoto za watendaji, katika suala zima la usafiri ili kuwarahisishia wafike maeneo ya Vijijini na yaliyo pembezoni mwa miji ,kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao" ,twende na Kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan ili tusimkwamishe"

"Niwaombe mkazitunze na kuzifanyia kazi mliyotumwa na sio kuzitumia kwenye safari zilizo nje ya wajibu wenu wa kazi ,mkawatumikie wananchi na kuleta matokeo chanya ya kimaendeleo" Changamoto ni maeneo mengine kuwa mbali na kushindwa kufikika kirahisi ,Sasa nendeni mkafanye kazi "alieleza Halima.

Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo,Shauri Selenda alieleza , Pikipiki sita zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kuwarahisishia usafiri watendaji kwenye kazi zao.

Alieleza ,huo ni mgao wa awamu ya kwanza ,kata zipo 11 hivyo watazigawa katika kata ambazo Zina vijiji vilivyo ndani ,vilivyo na umbali mrefu na awamu ya pili zitaelekezwa kwenye kata zilizobakia.

Selenda alizitaja kata zilizofanikiwa kupata mgao wa kwanza ni pamoja na Kilomo, Zinga, Makurunge, Fukayose,Yombo na Kerege.

Katika hatua nyingine, Halmashauri ya Bagamoyo, imedhamiria kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya maji, barabara,na kuweka Mazingira mazuri ili kuvutia wawekezaji na watalii kwenye Mji huo mkongwe.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo , Mohammed Usinga ,alitoa maelekezo ya baraza la madiwani na kuitaka Wakala wa misitu( TFS)Bagamoyo kutenga fedha kati ya makusanyo yake makubwa inayokusanya ili kudhibiti uchafuzi wa fukwe (bahari) na kusaidia na Halmashauri.

Alisema ,kwasasa  watalii wamekuwa wakikutana na mpangilio mbovu wa fukwe kwa wafanyabiashara na uchafuzi wa fukwe Hali ambayo inaondoa utulivu kwa watalii.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Selenda alieleza ,ipo mipango mkakati ya kuweka maeneo maalum ya kupaki magari , na kupanga wafanyabiashara waliopo pembezoni mwa fukwe .

Hata hivyo,Selenda alieleza , kwasasa wamejipanga kuendelea kuweka Mazingira mazuri ya kuvutia watalii BADECO beach iwe ya kisasa na tayari wamepata wawekezaji,kati ya wawekezaji hao yupo ambae ameshajinasibu kuwekeza kwa milioni 449 ,hali itakayosaidia kuongeza mapato ya halmashauri.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad