HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 2, 2023

UPELELEZI KESI YA MKURUGENZI TPA WAKAMILIKA

 

Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa, upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande na wenzake umekamilika.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na wakili wa serikali Mosie Kaima umeeleza hayo leo Machi 2, 2023 mbele ya ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

"Mheshimiwa, upelelezi wa kesi hii umekamilika na tupo kwenye hatua ya kuwasilisha nyaraka katika Mahakama Kuu' tunaomba kesi hii iahirishwe, amedai Kaima.

Mbali na Kipande washtakiwa wengine ni Peter Gawile (58) Ofisa Rasilimali Watu wa TPA, Casmily Lujegi (65) Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Mkazi wa Mbezi Makabe.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 4.2

Hakimu Rugemarila ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 27,2023 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Katikab kesi hiyo inadaiwa kati ya Oktoba Mosi,2014 na Oktoba Mosi 2020 jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama na kuisababishia TPA hasara ya Sh bilioni 4.2

Inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17,2015 washtakiwa wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04 .

Pia inadaiwa kati ya Oktoba Mosi 2014 na Oktoba Mosi,2020 maeneo ya TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha Bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo jambo lililosababisha TPA hasara ya USD 1.8 Sawa na zaidi ya Sh 4.2 bilioni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad