Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WANACHAMA wa zaidi ya 200 wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake nchini (TWCC) wamepewa elimu ya ufahamu wa mabadiliko ya tabia nchi na athari za mazingira sanjari na kukabiliana na hali hiyo katika shughuli zao mbalimbali, kwa sababu ya hali hiyo imekuwa tishio ulimwenguni kote.
Akizungumza na Michuzi Blog, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi TWCC, Bi. Victoria Mwanukuzi amesema Wanachama hao wamepewa elimu hiyo ya mabadiliko ya tabia nchi ili kuepuka athari za mazingira ambazo zinaweza kutokea na kukwamisha shughuli zao mbalimbali za biashara.
“Mabadiliko ya tabia nchi yanaweza kuwa na athari hata kwetu sisi Wafanyabiashara, kwa mfano, Mtu anayetengeneza nguo aina ya Batiki mara nyingi anatumia ‘Chemical’ ambazo zinaweza kuwa na athari katika udongo endapo zitamwagwa bila utaratibu, na hivyo kusababisha mazao kutoota kwenye udongo wenye rutuba na miti isikue,” amesema Mwanukuzi
Aidha, Mwanukuzu amesema elimu hiyo ya mabadiliko ya tabia nchi itasaidia Wafanyabiashara hao kutoa elimu kwa wengine ili kuepuka athari mbalimbali za mazingira ambazo zinaweza kusababishwa na hali hiyo wakati wowote.
“Elimu ya mabadiliko ya tabia nchi, pia inaweza kutukosesha Mikopo na Misaada kutoka kwa Wahisani, kwa sababu tu, tumekosa elimu hii. Hata dunia inaona kuna umuhimu wa kutolewa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi ili kukabiliana na athari ambazo zinaweza kujitokeza,” ameeleza Bi. Mwanukuzi
Kwa upande wake, Mshauri ambaye amehusika kutoa elimu hiyo ya masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, Crispin Kapinga amesema wametoa elimu hiyo kwa Wafanyabiashara wa TWCC ili na wao wawe Mabalozi wazuri baada ya kupata elimu hiyo.
“Mabadiliko ya tabia nchi na athari za mazingira yanaweza kuathiri zaidi uzalishaji wa Malighafi mbalimbali ambazo zilitakiwa kuzalishwa kuwa bidhaa lakini mabadiliko hayo ya tabia nchi yanaweza kuathiri uendeshaji wa biashara,” amesema Kapinga.
No comments:
Post a Comment