HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 18, 2023

TMA YAZIDI KUIMARIKA KATIKA MIAKA MIWILI YA MAMA SAMIA HUDUMA ZA HALI YA HEWA, MIUNDOMBINU UTABIRI SAFII

Moja ya vifaa vya kutambua matukio ya radi katika kituo cha K,ibondo, mkoani Kigoma.
Mtambo wa kupima hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga.
Kompyuta kubwa ya Kisasa ya kuchambua data za hali ya hewa (Computer Cluster).
Na Karama Kenyunko Michuzi TV
RAIS Samia Suluhu Hassan anatamiza miaka miwili ya kuiongoza Tanzania baada ya kifo cha Rais wa awamu ya tano, John Magufuli.

Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za hali ya hewa chini ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kukidhi mahitaji ya watumiaji Kitaifa na Kimataifa.

Uboreshaji huo umejikita katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa na ununuzi wa Rada za hali ya hewa huku viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa ujumla vimeongezeka na kufikia asilimia 88.5.

Katika msimu wa mvua za vuli 2022, viwango vya usahihi vilikuwa asilimia 94.1 ambapo viwango hivyo ni vya juu ya kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70.

Pia TMA imetekeleza mfumo wa kudhibiti ubora, kujenga uwezo kwa watumishi, kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo mkoani Kigoma, kuiwakilisha nchi kikanda na kimataifa katika masuala ya hali ya hewa na kuboresha utoaji wa huduma kwa lengo la kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Kaimu Mkurugenzi wa TMA Dkt. Ladislaus Chang'a amesema kuwa katika kipindi hicho serikali ilitenga fedha kiasi cha Sh bilioni 50 katika bajeti ya maendeleo kwa ajili ya ununuzi wa rada za hali ya hewa, kununua vifaa vya hali ya hali ya hewa, ukarabati wa vituo vya hali ya hewa pamoja na ujenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa cha Kanda ya Mashariki.

Amesema kuwa mamlaka hiyo ilinunua rada nne za hali ya hewa ambapo ufungaji wa rada mbili kwa mikoa ya Kigoma na Mbeya na kwamba kukamilika kwa rada hizo kutakamilisha lengo la muda mrefu la TMA kuwa na rada saba za hali ya hewa kwa nchi nzima.

Pia amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kununua kompyuta ya kisasa yenye uwezo mkubwa ambayo itaongeza uwezo wake katika kuchakata,kuchambua taarifa za hali ya hewa kwa muda mfupi na hivyo kuongeza uwezo wa mamlaka wa kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa haraka,ushahihi na kuboresha utabiri wa maeneo madogo madogo.

"Mamlaka imeendelea na uboreshaji wa miundo mbinu ya vifaa vya hali ya hewa kuendana na teknolojia na matakwa ya kimataifa ikiwemo kuondoa vifaa vyote vinavyotumia zebaki kwa kununua vifaa 15 vya kidigitali vya kupima mgandamizo wa hewa na vifaa 25 vya kidigitali vya kupima joto," alisema

Dkt. Chang'a anaeleza kuwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa ujumla vimeongezeka na kufikia asilimia 88.5, ambapo katika msimu wa mvua za vuli 2022, viwango vya usahihi vilikuwa asilimia 94.1.

Amesema viwango hivyo ni juu ya kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70.

"Ongezeko hili la usahihi wa utabiri unazifanya huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kuwa za uhakika na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta zote za kiuchumi na kijamii nchini zinazotegemea hali ya hewa. Kuongezeka kwa usahihi wa utabiri kumetokana na jitihada za serikali kuwekeza katika kusomesha wataalam wa hali ya hewa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuandaa utabiri pamoja na kuongezeka kwa mtandao wa vituo vya kupima hali ya hewa," amesema.

Vilevile anasema mamlaka hiyo inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) katika kutekeleza majukumu ya sekta ya hali ya hewa kwa shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo kufuatlia mabadiliko ya hali ya hewa yanayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.

Vifaa 20 vya kupima uchafuzi wa hewa vimenunuliwa na kufungwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuona kwa kiasi gani shughuli za kibinadamu zinavyoharibu mazingira.

Pia taarifa za hali ya hewa zimekuwa zikitumika katika kufanya upembuzi yakinifu wa athari za miradi na hivyo kusaidia katika utunzaji wa mazingira.

Matumizi ya Tehama
Mamlaka imekuwa ikitumia fursa ya kukua kwa Tehama kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma na pia kurahisisha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa.

Ameeleza kuwa TMA ilinunua vifaa na mitambo mbalimbali ya kupima hali ya hewa ambayo utendaji wake umerahisishwa kwa kutumia TEHAMA na hivyo kuweza kupima na kutuma taarifa za hali ya hewa katika Kituo Kikuu na Utabiri.

Pia kuundwa kwa mifumo mbalimbali iliyorahisisha shughuli za uendeshaji na utoaji wa huduma kwa watumiaji wa usafiri wa anga, watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu.

Mamlaka imeendelea kukidhi Viwango vya Ubora vya Kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga na hivyo anga la Tanzania kuendelea kuaminika kuwa salama.

"Katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mamlaka ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa na Kampuni ya Certech ya Canada juu ya utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora wa huduma “Quality Management Systems(QMS)” kwa mwaka 2021 na 2022 ambapo ukaguzi wa mwaka 2022 ulifanyika kuanzia Januari 14 hadi 21 Januari 2023. Katika kaguzi hizo ubora wa huduma zinazotolewa na Mamlaka katika seekta ya usafiri na usalama wa anga zilionekana kukidhi mahitaji ya wadau, jambo ambalo liliwezesha Mamlaka kuendelea kushikilia cheti cha ubora wa huduma tajwa cha ISO 9001:2015," anasisitiza

Mamlaka imeendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kufanya tafiti mbalimbali katika masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, jumla ya machapisho ya utafiti manne yaliandaliwa na kuchapishwa katika majarida ya kimataifa ya sayansi na wataalamu watano kutoka Zanzibar walishiriki katika tafiti hizo ambazo zimechangia katika kuboresha huduma zinanzotolewa na TMA.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad