Kesi dhidi ya kufanyia uchunguzi kifo cha Stela aliyefia kituo cha polisi yazidi kupigwa kalenda - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 10, 2023

Kesi dhidi ya kufanyia uchunguzi kifo cha Stela aliyefia kituo cha polisi yazidi kupigwa kalenda

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imeshindwa kuanza kutekeleza amri yake ya kufanyia uchunguzi chanzo cha kifo cha Stella Moses aliyefia mahahabusu ya Kituo cha Polisi Mburahati mwaka 2020 kufuatia upande wa Jamuhuri kuwasilisha pingamizi la awali.

Katika pingamizi hilo, dhidi ya kesi namba 3,2022 wajibu maombi ambao ni Mkuu wa Jeshi la Polisi na wenzake wanaiomba mahakama isifanye chunguzi huo mpaka pale maombi waliyoyawasilisha yatakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.

Mapema wakili wa mleta maombi, Peter Madeleka alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya utekelezaji wa amri iliyotelewa mahakamani hapo Februari 17, 2023 ya kufanyika kwa uchunguzi wa kifo cha Stella ambaye anadaiwa kufa katika mazingira ya kutatanisha.

Amedai kwa kuwa akidi imetimia kwa maana yq wazee wa baraza watatu kwa ajili ya kushuhudia shughuli ya ufukuaji wa mwili na kufanyika kwa uchunguzi wa mwili huo ili kubaini sababu za kifo hicho.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema amepinga hoja hiyo akidai kwamba Februari 17 mwaka huu, walifungua shauri jipya la uchunguzi namba moja la mwaka 2023 wakitaka uchunguzi wa kesi hiyo usifanyike kwanza mpaka shauri lao hilo jipya litakaposikilizwa.

"Ninanafahamu kwamba mahakama ilitoa amri kuhusu kufanyika kwa uchunguzi lakini tunaomba anaomba kusikilizwa kwa shauri hili jipya kwanza ndipo utekelezaji wa amri yake ufuate.

Hata hivyo Wakili Madeleka ameiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo kwa sababu halina mashiko na linalenga kuipotezea mahakama muda wake. kwamba upande wa serikali haukutaja kifungu cha sheria ambacho kimekiukwa kwa kuwepo kwa shauri hilo mahakamani.

Akirejea kesi ya James Rugemalira dhidi ya DPP amesema Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya hiyo iliamuru kwamba ili pingamizi likubaliwe mahakamani linatakiwa kutaja kifungu cha sheria iliyovunjwa.

"Ibara 107 A na B ya Katiba imebainisha kuwa mahakama ni chombo huru na kwamba katika kutekeleza majumu yake katika mashauri ya jinai na madai italazimika kuzingatia masharti ya katiba na ya sheria za nchi na mpaka mahakama inatoa amri ya kufanyika kwa uchunguzi inatambua kwamba kuna kesi inayohitaji kufanyika kwa uchunguzi kwa sababu ya kifo cha mazingira ya utata na yenyewe ina mamlaka ya kusikiliza na kutoa amri.

"Mpaka leo tuko hapa maana yake kesi ipo mbele yako muheshimiwa na umeisikiliza na kutoa amri hivyo kilichobaki ni utekelezaji wa amri ili kujua sababu za kifo...mahakama haijawahi kufanya uchunguzi na sababu hazijajulikana,’’ alidai Madeleka.

"Kama mahakama ingekuwa imefanya uchunguzi na sababu zikajulikana, maombi hayo ndio yangeletwa mahakamani kwani mpaka sasa kesi hiyo haijafika kikomo" ameongeza.

Alidai maombi yaliyowasilishwa mahakamani yameletwa kinyume na sheria kifungu cha 4, 12 cha Sheria ya Uchunguzi wa Kifo na kwamba kama shauri hilo lipo linakiuka katiba.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Mrema alidai sheria haiwazuii kuleta pingamizi na kwamba wana uwezo wa kuwasilisha pingamizi hata kama kesi inakaribia kutolewa hukumu.

‘’Nakubaliana na hakimu kwamba shauri hili limesikilizwa na kukamilika na amri iliyoombwa imesikilizwa na ndio maana amri imetoka. Lakini kwa kuwa uchunguzi haujafanyika tunasisitiza kilichoombwa ni amri ya kufanya uchunguzi na kwa mujibu wa maombi yetu ipokee kama mambo ya kufikirika ambayo yamewasilishwa,’’ amedai Mrema.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 17, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi dhidi ya mapingamizi hayo.

Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020, akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Mburahati alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa anahitajika huko polisi wakidai kuwa mtuhumiwa huyo alijinyonga.

Hata hivyo, wanafamilia hawakukubaliana na maelezo hayo badala yake wakaomba ufanyike uchunguzi huru kujiridhisha chanzo cha kifo chake wakati Jeshi la Polisi likishinikiza mwili wa marehemu uzikwe.

Shauri hilo lilifunguliwa na shemeji wa marehemu, Emmanuel Kagongo, kwa niaba ya familia ya marehemu dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspekta Jenerali wa Polisi – IGP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam (ZPC) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika hati ya maombi hayo ya jinai mchanganyiko namba 3 ya mwaka 2022, aliomba mahakama hiyo iridhie kufanya uchunguzi huru ili kujua ukweli wa mazingira ya kifo cha ndugu yao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad