HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 22, 2023

Harmonize, Mario kupamba matamasha ya Kili Marathon mjini Moshi

BARABARA zote mkoani Kilimanjaro, hususan Moshi Mjini, zinaelekea katika viwanja vya Moshi Club na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mwishoni mwa wiki, ambapo wasanii nguli wakiwemo Harmonize na Mario watarajiwa kupanda majukwaani kunogesha mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zinazotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matukio hayo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema maandalizi yote yamekamilika na wasanii hao wawili wataongoza safu ya wasanii mbalimbali wanaotarajiwa kutumbuiza wakati wa tukio hilo la kimataifa mwishoni mwa wiki.

"Sisi kama waandalizi tuko tayari na tunatazamia tukio la mwaka huu tunapoadhimisha msimu wa 21 wa Kilimanjaro marathon, litakuwa ni la kihistoria na ambalo litakumbukwa kwa muda mrefu", alisema na kuongeza, kwa kawaida tukio hili huambatana na burudani za kusisimua.

Amesema Harmonize atatumbuiza katika Klabu ya Moshi (Moshi Club) Ijumaa Februari 24, 2023 wakati Mario anatarajiwa kutumbuiza siku ya Jumapili Februari 26, 2023 baada ya mashindano ya Kili Marathon. Alitoa wito kwa wakazi wa Moshi na wageni kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha la Kili Marathon ili kuwa sehemu ya tukio hilo la kihistoria.

Aidha Kikuli amesema kutakuwa na burudani ya kipekee katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi ambapo mbio za marathon zinatarajiwa kutafanyikia.

"Burudani itaanza mara baada ya programu rasmi ya mbio za Kili Marathon kumalizika ili watakaohudhuria tukio hilo wapate kufuatilia na kuburudika na burudani inayotarajiwa kutolewa na wasanii watakotumbuiza siku hiyo", alisema.

Wasanii watakaotumbuiza katika uwanja wa MoCU, kwa mujibu wa Pamela ni pamoja na, Billinais, Lordeyes, Conboi, Saraphina na Machalii Watundu kutoka Arusha.

Katika hatua nyingine, waandaaji wa mbio za Kilimanjaro International Marathon wamewakumbusha wanaotarajiwa kushiriki mbio hizo ya kuwa siku ya mwisho za kuchukua namba na vifaa vya ushiriki ni siku ya Alhamisi, Februari 23 kati ya saa 6 mchana na saa 11 jioni na Ijumaa Februari 24 kati ya saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni ambapo Jumamosi Februari 25, zoezi hilo litafanyika kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 11 jioni, eneo la uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Waandaaji hao wamewataka washiriki hao kuzingatia muda uliotangazwa ili kuepuka usumbufu na pia wametoa wito kwa wale wanaochukua namba na vifaa hivyo kwa niaba ya marafiki au ndugu zao kuhakikisha wanakuwa na nakala za vitambulisho vyao au barua za ridhaa kutoka kwa washiriki halisi waliowatuma zinazowaruhusu kuchukua namba na vifaa kwa niaba yao.

"Ni matumaini yetu kuwa washiriki watajitokeza kwa wingi katika eneo la kukusanyia namba na vifaa kwa vile hakuna namba au vifaa vitakavyotolewa siku ya tukio", ilisema taarifa ya wandaaji na kuongeza kuwa wale ambao hawakukusanya namba zao na vifaa Dar es Salaam na Arusha bado wanaweza kufanya hivyo mjini Moshi kwa tarehe zilizoelezewa.

Wadhamini wa mwaka huu ni pamoja na wadhamini wa wakuu Kilimanjaro Premium Lager kilomita 42, Tigo kilmita 21km (Half Marathon), Grand Malt kilomita 5 za kujifurahisha, ambapo wadhamini wa meza za maji ni pamoja na TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na wasambazaji rasmi Surveyed Plots Company Limited (SPC), Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles, KK Security na Keys Hotel. Kili Marathon huandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions Limited.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad