HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 11, 2023

Serikali Kujenga Minara 8 ya Mawasiliano Mlimba

 


Na Immaculate Makilika - WHMTH
HUDUMU za mawasiliano ni za msingi katika maisha ya wananchi kwa vile zinagusa nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Aidha, mawasiliano yanawezesha na kuhimili sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, uwekezaji na biashara, ajira, benki na utalii kwa kuziongezea ufanisi wa kiutendaji na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa moja kwa moja kupitia sekta hizo.

Ili kutimiza azma hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga minara nane ya huduma za mawasiliano katika Jimbo la Mlimba lililopo mkoani Morogoro.

Akizungumza juzi (Januari 9, 2023) katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kisegese, Kata ya Namwawala, Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, wakati alipokuwa katika ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma ya mawasiliano na kuzungumza na wananchi. Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa. Mhandisi Kundo Mathew amesema “Mheshimiwa Rais alielekeza kufanya tahmini ya mawasiliano katika jimbo hili ambapo takribani shilingi bilioni 2.4 zitatumika kujenga minara nane ya huduma za mawasiliano katika jimbo hili la Mlimba”.

Ameongeza “Minara nane yote itakayojengwa itakuwa na huduma za intaneti na hivyo mkawe walinzi wa hiyo minara kwa kuwa mawasiliano ni haki ya kila mwananchi na mtanufaika kwa kuinua uchumi kupitia biashara mtandao”.

Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Mheshimiwa Godfrey Kunambi amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha za ujenzi wa minara hiyo nane na kusema kuwa mara baada ya minara hiyo kuanza kutoa huduma wananchi wa jimbo hilo watanufaika kwa kutumia fursa mbalimbali za mawasiliano kwa kukuza uchumi wa wananchi wake.

Naye, Mratibu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kanda ya Pwani, Mhandisi Mwandamizi Baraka Elieza amesema katika zabuni itakayofunguliwa Januari 31, 2023, UCSAF itahakikisha wazabuni (makampuni ya simu) watakaoshinda wanafikisha mawasiliano katika kata hizi nane ndani ya Jimbo la Mlimba kwa ufanisi.

“Minara hii itawezesha kufikisha mawasiliano katika kata za Ching’anda, Chita, Signal, Kamweni, Kiberege, Masagati, Namwawala na Uchindile na hivyo kusaidia kuwa na mawasiliano ya uhakika”. Amesema Mhandisi Baraka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad