HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 20, 2022

Wajasiriamali Nchini Hawajajiunga na Mifuko ya Uhifadhi wa Jamii, Bima ya Afya

 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt.Godbertha Kinyondo akizungumza  jijini leo Desemba 20, 2022 wakati wanapotoa matokeo ya utafiti uliofanyika kuanzia 2017 hadi yanaposambazwa kwa watu wa sekta ya usafiri na wajasiriamali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt.Godbertha Kinyondo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 20, 2022.

WAJASIRIAMALI wadogo wadogo nchini hawajajiunga na Mifuko ya Uhifadhi wa Jamii kutokana na uelewa mdogo wa mifuko hiyo na kupelekea kutopata unafuu pale anaposhindwa kufanya kazi yake.

Ameyasema hayo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt.Godbertha Kinyondo jijini Dar Es Salaam leo Desemba 20, 2022 wakati akitoa matokeo ya Utafiti wa sekta zisizo rasmi na hifadhi ya jamii ambapo amesema kuna umuhimu mkubwa wajasiriamali wadogo kujiunga na mifuko  ya hifadhi ya jamii yenye manufaa kwao hapo baadae.

Amesema Utafiti unaohusu wajasiriamali wadogowadogo na Uhifadhi wa Jamii waliianza mwaka  2017 na kilichowasukuma kufanya utafiti huo ilikuwa kuona jinsi wajasiriamali wadogowadogo wanaweza kujikimu katika uhifadhi wa jamii.

Aidha amesema katika utafiti huo wamefanya katika mkoa ya Dar es Salaam na Dodoma na sasa wamepata majibu ya utafiti ambapo wameyapata mwaka 2021 na wameandika  kitabu ambacho kipo kwenye tovuti pamoja na machapisho.

"Mpaka sasa bodaboda wameshaanza kuwa na uelewa kuhusu hifadhi ya jamii kwani wameshaanza kutafuta mikopo na wamekuwa wakikopesheka na hata wengine kuingia kwenye vikundi ambavyo vinawasaidia katika kujikimu kimaisha kupitia shughuli zao". Amesema 

Kwa upande wa Afisa Biashara wa jijini la Dar es Salaam, Nikasi Msemwa amesema utafiti huo ni muhimu kwani unaenda kutoa majibu mengi na makubwa katika jamii yetu, utafiti  huo umejikita katika kuangalia kesho wafanyakazi wa Sekta zisizorasmi na wale wenye kipatacho cha chini.

Amesema Pensheni itakuwa ni msaada kwao wanapokuwa wamezeeka lakini Bima ya Afya itaenda kutoa majibu kwa wajasiriamali pia kwa familia zao.

"Kwa kuwa tafiti hii ndo imetangazwa itakuwa imesambaa kwa watu wote kwahiyo zile taasisi ambazo ni wadau wataangalia fursa kwenye hii tafiti kwasababu kuna baadhi ya vitu, mfano hizi taasisi za kifedha zipo tayari kufanya jambo lolote lile lakini kama kuna tafiti kama huu uko tayari kuna uhakika taasisi mbalimbali kuingia". Amesema Msemwa

Afisa Habari Msaidizi wa Shirikisho la Vyama vya Waendesha Pikipiki (bodaboda na bajaji) Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Msisiri amesema bodaboda wengi hawafahamu nini maana ya hifadhi ya jamii, lakini kupitia Chuo cha Mzumbe, kwa kiasi kikubwa bodaboda wameanza kuwa na uelewa mpana juu ya kujiwekea hifadhi ya maisha yao.

"Bodaboda wote wameitikia wito na wako tayari kuanza sasa kuhifadhi, kutunza fedha zao lakini pia kujiwekea bima ya maisha za Afya, na kazi yote hii imefanywa na Chuo Kikuu cha Mzumbe". Amesema

Amesema kuwa baada ya mkutano huo wanatarajia Wafanyakazi wa Sekta ya Usafiri na Wajasiriamali watajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, watakata bima za afya pamoja na bima za vyombo vyao vya moto.
Afisa Biashara wa jijini la Dar es Salaam, Nikasi Msemwa akizungumza wakati Chuo Kikuu Mzumbe wakisambaza Matokeo ya Utafiti katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo Desemba 20, 2022.
 
Picha ya Pamoja.   
Baadhi wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwa katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad