Kwa mara nyingine tena, Benki ya NMB imedhihirisha umahiri na ukubwa wake kiutendaji na kiundeshaji nchini baada yakufanikiwa kunyakuwa tuzo ya mwajiri bora barani Afrika – the Best Employer Brand Africa.
Ushindi
huo mkubwa ulipatikana wiki jana mjini Port Louis huko Maurituis ambako
NMB ilitunukiwa tuzo hiyo inayotambua umakini katika kuzingatia maslahi
na maendeleo ya wafanyakazi na waandaaji wake ambao ni taasisi ya ajira
ya Employer Branding Institute.
Akipokea nishani hiyo jana makao
makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa
NMB, Bw Filbert Mponzi, alisema tuzo hiyo ya nne ya mwajiri bora mwaka
huu, ni ushahidi mwingine wa jinsi taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini
inavyothamini wafanyakazi wake.
“Thamani ya wafanyakazi kwetu
sisi NMB ni kubwa sana kwani wao ndiyo rasilimali inayoongoza na chanzo
cha mafanikio yetu yote na tuzo mbalimbali ambazo tumekuwa tunazipata ,”
Bw Mponzi alisema baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Afisa Mkuu
Rasilimali Watu, Bw Emmanuel Akonaay.
Kiongozi huyo ambaye pia ni
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB aliongeza kuwa baada ya
kuongoza karibu kwa kila kitu nchini, sasa wameanza kupata mafanikio
barani Afrika.
Hii inatokana na NMB kuzingatia matakwa ya msingi
ya uongozi na uendeshaji taasisi hasa zile za fedha. Ushindi wa mwajiri
bora, alifafanua, unatokana na NMB kutambua umuhimu wa rasilimali watu
na kuwekeza katika maendeleo yake.
Mbali ya kuwa mwajiri bora,
pia NMB ndiyo benki bora na kiongozi nchini. Mwaka huu tu, NMB imeweza
kujikusanyia zaidi ya tuzo 20 za kimataifa ilizotunukiwa na majarida
yanayoheshimika duniani kama vile World Economic Magazine, Global Brands
Magazine, International Banker Awards na International Business
Magazine. Mwezi jana, NMB alinyakua tuzo tatu za mwajiri mahiri kutoka
kwa chama cha waajiri nchini (ATE) ikiwemo ile ya mwajiri bora wa mwaka
2022.
Bw Akonaay ambaye ndiye aliipokea tuzo ya Best Employer
Brand – Africa huko Mauritius tarehe 13 mwezi huu alisema tuzo hiyo ni
mwendelezo wa mambo makubwa ya NMB kwa mwaka huu.
Akizungumza
kabla ya kuikabidhi rasmi kwa Bw Mponzi, mtaalamu huyo wa ajira na
wafanyakazi alisema heshima waliyopata inazidi kuifanya NMB kutambulika
barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.
Kiongozi huyo aliongeza
kuwa ushindi walioupata unatokana na juhudi za bodi na menejimenti ya
NMB lakini zaidi wafanyakazi wa benki hiyo. NMB, alifafanua, imeonyesha
kuwa si tu taasisi inayoongoza kwa huduma za kifedha bali pia ni kinara
wa kujali maslahi ya wafanyakazi wake.
“Sisi tunaongoza si tu kwa biashara na huduma bora bali pia linapokuja swala la rasilimali watu,” alieleza.


No comments:
Post a Comment