HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 5, 2022

TEN/MET yataka ubora wa elimu ukidhi mahitaji ya wenye ulemavu

  

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Bw. Ochola  Wayoga

MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET), umetoa changamoto kwa wadau wa elimu nchini kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha mabadiliko ya elimu yanayofanywa yanakidhi mahitaji ya kundi la watu wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola  Wayoga mwishoni mwa wiki kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye ulemavu inayoadhimishwa kila Disemba 3, amesema wadau na Serikali wanapaswa kuwekeza zaidi katika utambuzi wa mapema wa ulemavu tofauti kwa watoto kwa ajili ya kuwasaidia.

Alisema katika kuwasaidia zaidi kundi hilo la watu wenye ulemavu ipo haja ya kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa lugha ya ishara, ambayo imekuwa ikigusa zaidi mawasiliano kamili kwa watoto wenye ulemavu ili kuchochea hoja ya kujenga jamii jumuishi.

"Wadau wa elimu kwa kushirikiana na serikali tuendelee kutoa vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili kuhakikisha watoto wote walio shuleni wanapata nyenzo za kujifunzia kulingana na mahitaji yao,"

"Utoaji wa elimu kwa wote lazima uungwe mkono na vifaa na miundo msingi, shule za serikali na za kibinafsi lazima zifuate viwango vya vifaa vinavyohitajika kusaidia ujifunzaji kwa wote, hii ikiwa pamoja na msaada wa ushauri nasaha kwa walezi, wazazi na watu wenye ulemavu kutolewa ili kuondoa au kupunguza unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu,"  alisema Bw. Wayoga.

Aidha aliiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha inapata takwimu za uhakika za idadi sahihi ya watu wenye ulemavu, aina za ulemavu walionao, umri na jinsia katika ngazi ya taifa, mkoa na wilaya ili kurahisisha namna ya kuwahudumia pale inapobidi.

Alibainisha kuwa juhudi za Serikali za kutoa elimu bila malipo kwa wote lazima ziendane na ubora wa elimu unaokidhi mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu, ikiwa pia ni pamoja na kutoa ruzuku ya matibabu, ukarabati na vifaa vinavyotumika kwa watu wenye ulemavu ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini.

Hata hivyo aliongeza kuwa TEN/MET na wadau wake itaendelea kuunga mkono elimu jumuishi kwa walemavu kwa kutoa masuluhisho ya kuleta maendeleo jumuishi katika elimu na pia kukuza utambuzi wa haki za watu wenye ulemavu ili kundi hilo lisisahaulike kwenye maendeleo ya elimu kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad