Watakaotoa kauli mbaya kwa wagonjwa kuchukuliwa hatua kali - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 9, 2022

Watakaotoa kauli mbaya kwa wagonjwa kuchukuliwa hatua kali

 


Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kutoa kauli mbaya kwa wagonjwa, kuwatoza fedha kinyume na utaratibu,kanuni, sheria na uadilifu katika utumishi wa umma watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Onyo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya uadilifu kwa viongozi wa umma yanayotolewa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Dkt. Kisenge alisema JKCI imeandaa mafunzo hayo kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali kwa mujibu wa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi wa mwaka 2017 ukilenga kutekeleza mkakati wa Taifa wa kudhibiti uadilifu na mapambano dhidi ya rushwa awamu ya tatu ili watumishi wa umma washiriki kikamilifu na kwa vitendo kupambana na rushwa.

“Lengo la Taasisi yetu ni kuwa na watumishi wenye maadili mema na mfano wa kuigwa, Mtumishi mwadilifu atatumikia watanzania muda wote bila upendeleo, kujali hali zao wala kipato chao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma,”.

“Ninaamini mafunzo haya yatatuwezesha kujifunza namna ya kuishi kwa uadilifu katika kuhakikisha shughuli za serikali zinafikia malengo yaliyowekwa huku watumishi wakizingatia misingi ya uadilifu na maadili,” alisema Dkt. Kisenge.

“Ni matumaini yangu mafunzo haya yatawajengea uwezo wa kusimamia vyema maeneo yenu na kuwaongezea ari watumishi mnaowaongoza ili waweze kuwa na uadilifu mahala pa kazi na kuzingatia miiko ya kiutumishi na mwenendo mwema wa utumishi wa umma,”alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma George Mwendamseke alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuhakikisha viongozi wanatekeleza majukumu yao katika hali ya uadilifu, kujenga imani kwa wananchi, serikali na kuhakikisha kuwa hawajiingizi kwenye matatizo ya mgongano wa maslahi.

“Mafunzo tunayotoa yanahusu masuala ya kimaadili hususani eneo la maadili ya viongozi wa umma, kufahamu miongozo makatazo na nini cha kuzingatia katika kutekeleza majukumu ya kazi za kuwatumikia wananchi,”.

“Mafunzo haya pia yatahusisha mgongano wa maslahi kuhakikisha kwamba viongozi hawa wanatambua na kufahamu ni maeneo gani yanaweza kuwaingiza katika mgongano wa maslahi na kuweza kujikwamua nayo,” alisema Mwendamseke.

Mwendamseke alitoa wito kwa taasisi zote za umma kuhakikisha mafunzo kama hayo yanaandaliwa kwa viongozi wake kama ambavyo agizo la waraka wa mkuu wa utumishi wa umma ambao unataka elimu ya maadili itolewe kwa watumishi wote.

“Tunazikumbusha taasisi kuzingatia maelekezo ya viongozi kuhakikisha kwamba zinaandaa mafunzo ya kimaadili kwasababu maadili ni kinga ya maovu na husaidia katika kutoa huduma bora, kuboresha taasisi na kutekeleza mipango mikakati,” alisema Mwendamseke.

Naye Mkuu wa kitengo cha rasilimali watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abdulrahman Muya alisema Taasisi hiyo imeanza kutoa mafunzo hayo kwa viongozi na baadaye yatafanyika kwa watumishi wote.

“Tunategemea baada ya mafunzo haya tutaimarisha uadilifu kwa watumishi, kutokuwa na mazingira ya rushwa na kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa wetu kwani utekelezaji wa mpango mkakati wa kudhibiti uadilifu na mapambano dhidi ya rushwa mahali pa kazi ni sehemu ya utekelezaji wa Taasisi yetu,” alisema Muya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na viongozi wa Taasisi hiyo wakati wa kufungua mafunzo ya siku mbili ya uadilifu kwa viongozi wa JKCI jana katika ukumbi waTaasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa wakati wa mafunzo ya siku mbili ya uadilifu kwa viongozi wa Taasisi hiyo yaliyofanyika jana katika ukumbi wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Afisa uchunguzi kutoka Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa Umma Grace Kwambiana akiwafundisha viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) maadili ya watumishi wa umma wakati wa mafunzo ya uadilifu kwa viongozi wa Taasisi hiyo yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Picha na: Khamis Mussa

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad