HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 21, 2022

WAKUFUNZI ‘LAW SCHOOL OF TANZANIA’ KUFUATILIWA

 

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akipokea taarifa ya Kamati ya Kutathimini mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania) kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kushoto) anayeshuhudia (wa kwanza kulia) ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza wakati akipokea taarifa hiyo, Dkt. Ndumbaro amesema Wizara inaenda kufanyia kazi Taarifa hiyo iliyowasilishwa kwake baada ya kufanya kazi yake kwa siku 30.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tathmini ya Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), Dkt. Harrison Mwakyembe akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Makondo na Wajumbe wengine, Waandishi wa Habari (Hawapo pichani).

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KAMATI ya Tathmini ya Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) imesema imewasilisha majina ya Wakufunzi waliotajwa kwa Uongozi wa juu wa Taasisi ili uweze kufuatilia mienendo yao.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo tuhuma za vitendo vya rushwa, uonevu, upendeleo katika utungaji au usahihishaji wa Mitihani wa Wakufunzi hao na kupelekea kufeli kwa idadi kubwa ya Wanafunzi wa Taasisi hiyo Kundi la 33 la mwaka wa masomo 2021-2022.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, Mwenyekiti wa Kamati, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema endapo tuhuma hizo zitaendelea Wakufunzi hao wahamishiwe katika Idara zingine za Serikali ili kulinda taswira ya Taasisi.

Kupitia taarifa hiyo, Dkt. Mwakyembe amesema Kamati inaona kuwa ni wajibu wa Taasisi kuweka mazingira rafiki kwa Wanafunzi katika Taasisi hiyo sanjari na ukarabati wa Miundombinu ya Taasisi ili kuwa na mazingira bora kwa Wanafunzi hao kujisomea na kufaulu masomo yao vizuri.

Aidha, Kamati hiyo imebaini kuwa Taasisi hiyo ya ‘Law School of Tanzania’ hakuna Mahakama ya kufundishia kwa vitendo kwa Wanafunzi wanaosoma hapo, Dkt. Mwakyembe amesema Mahakama iliyojengwa katika Taasisi hiyo bado inatumiwa na Mahakama Kuu ya Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na kushindwa kutoa mchango kwa Wanafunzi wa Taaluma ya Sheria wanafanya mafunzo yao kwa vitendo.

“Kamati inatoa rai kwa Wizara na Mahakama ya Tanzania kuitafutia Divisheni hiyo ya Mahakama Kuu mapema iwezekanavyo sehemu nyingine ili kuruhusu kwa ushirikiano na Mahakama ya Tanzania kuanzishwa kwa Mahakama ya Wilaya itakayotumika kikamilifu katika kuimarisha mafunzo ya uanasheria kwa vitendo LST”, imeeleza Kamati

Kamati hiyo yenye Wajumbe Sita waliokuwa chini ya Mwenyekiti, Dkt. Mwakyembe imewasilisha taarifa hiyo kwa Waziri Dkt. Ndumbaro baada ya kuwepo mjadala mkubwa nchini kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya Mitihani ya ‘Law School ya Kundi la 33 la mwaka 2021-2022, mapema mwezi Oktoba.

Katika matokeo hayo, Wanafunzi 633 wa Kundi hilo walifanya Mitihani hiyo, Wanafunzi 26 walifaulu Mitihani katika mkao wa kwanza, Wanafunzi 342 walifaulu baadhi ya masomo na wana fursa kurudia Mitihani ya masomo walioshindwa, Wanafunzi 265 walifeli Mtihani mzima na wanaweza kuanza upya mafuzo wakiwa tayari.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad