HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 1, 2022

RAIS SAMIA AAGIZA KUUNDWA KWA KIKOSI KAZI CHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

 

Na Khadija Seif,Michuzi Tv.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, ametaja mikakati mitatu mikubwa itakayotekelezwa haraka na serikali ya awamu ya sita kuhakikisha ndani ya miaka 10 kuanzia sasa nchi iweze kufikia asilimia 80 hadi 90 ya uwepo wa nishati safi na endelevu ya kupikia ifikapo 2032.

Akizungumza jana katika ufunguzi wa mjadala wa nishati safi ya kupikia uliofanyika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere nchini, Rais Samia alisema mjadala huo ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.

Amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuunda kikosi kazi, kutengwa kwa fedha mwaka ujao wa bajeti ya Wizara ya Nishati na kuanzishwa kwa Mfuko wa Nishati Safi na jambo la tatu taasisi zote za serikali zenye kuhudumia watu zaidi ya 300 zianze kutumia nishati mbadala ikiwemo gesi na kuachana na mtumizi ya kuni au mkaa.

Amesema nishati safi ya kupikia ni mjadala mpana, unaopaswa kuja na mawazo ya pamoja kwa kuwa suala hilo linaibua changamoto nyingi kwa jamii na ni lazima kama serikali ianze kuchukua hatua sasa.

''Japo tumejipa miaka 10 lakini hatupaswi kusubiri huko katika kutafuta ufumbuzi wa uwepo wa nishati safi ya kupikia. Naelekeza sasa suala hili tunalokwenda nalo si suala la muda mrefu bali ni suala la muda fupi na ni lazima tuanze sasa na kwa kasi kubwa.'' anasema.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuundwe haraka kwa kikosi kazi kitakachojumuisha sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kupatikane kwa mawazo ya pamoja na sio kila mtu anakuwa na mipango yake.

''Natambua suala la nishati safi ya kupikia ni jambo linalounganisha taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara mbalimbali kama Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Wizara ya Nishati, TAMISEMI, Maendeleo ya Jamii sasa nadhani sekta binafsi inapaswa kuwepo na wadau wa maendeleo'' amesema.

Amesema malengo na mategemeo yake ni kuhakikisha ndani ya miaka 10 aweze kumtua kuni mama kichwani na hilo anaamini litafanikiwa kama alivyofanikiwa katika sekta ya maji, ambapo zaidi ya asilimia 80 wananchi wanapata majisafi na salama.

''Kikosi hiki kiongozwe na Waziri Mkuu na kwa ngazi ya makatibu wakuu kiongozwe na Wizara ya Nishati. Lazima twende na nishati safi ya kupikia kwa maendeleo ya nchi na wanawake kwa ujumla'' amesema.

Pia, Rais Samia alisema kikubwa kinachotakiwa kwa sasa ni kuwa na mawazo ya pamoja na kubadilisha mtazamo wa wananchi kutoka katika matumizi ya kuni na mkaa na kwenda katika nishati safi na endelevu.

''Nina matumaini makubwa kikosi kazi cha taifa kitakuja maoni bora ili serikali iweze kuja na sera na mkakati wa pamoja wa nchi kuwa na nishati safi ya kupikia na ndio maana nataka kiunganishwe na sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo'' anasema.

Mkakati wa pili, Rais Samia alisema katika bajeti ijayo ya fedha kwa Wizara ya Nishati kutakuwa na ongezeko la fedha kwa ajili ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Nishati Safi ili kuleta mafanikio makubwa.

''Serikali pekee haiweze lazima kuwa na ushirikiano wa pamoja. Hivyo tutashirikiana ili kuwe na sera na mpango makakati mzuri, hivyo kuanzishwa kwa kikosi kazi litasiadia sana katika mipango ya serikali katika suala hili hususan katika ongezeko la bajeti''alisema.

Pia, alisema mkakati wa tatu ni kuzitaka taasisi zote za kiserikali ikiwemo shule, vyombo vya ulinzi na usalama, magereza kutumia nishati safi ya kupikia na kuchana na matumizi ya kuni na mkaa.

Amesema kuwezekana kwa mambo hayo, anamatumaini hadi ifikapo 2032 itasaidia kuwa na nishati safi na endelevu ya kupikia, ambapo aliagiza Wizara ya Nishati kuanza sasa na wasisubiri hadi ifikapo 2032.


Katika mjadala huo, Rais Samia alivutiwa na mijadala mbalimbali iliyokuwa inatolewa ikiwemo mwanasiasa maarufu nchini, Profesa Anna Tibaijuka, Daktari bingwa wa magonjwa ya kupumua, Dk. Pauline Chale na wataalamu wengine na kusema ni mjadala wenye mawazo bora na ya kujenga. 

Alisema amesikia suala la bei kuwa nafuu huku wengine wakidai mkaa ni bei rahisi kuliko gesi, lakini bei wengine wamedai kuwa gharama rahisi ya mkaa ni mbaya zaidi kutokana na madhara anayoyapata mwananchi.

''Suala hili ni jambo pana na linahitaji mawazo ya pamoja na sio serikali pekee. Lengo ni kuhakikisha suala linakuwa afforadabilty na pia kubadili mtazamo wa wananchi juu ya masuala haya'' alisema.

Rais Samia alisema anaipongeza Wizara ya Nishati kwa mjadala huu, umekuja wakati mwafaka ambao sasa duniani inahamisisha matumizi ya nishati safi na salama kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na nishati safi na kuachana na kuni na mkaa.

''Nawapongeza wote mlioshiriki. Nawapongeza mkutano huu ulipaswa kuwa zaidi ya elfu 100 lakini sasa kuna watu elfu 300, naelewa kumbi zetu haziwezi kuchukua watu wengi. Wawekezaji sasa changamkeni hii fursa kuhakikisha mnakuwa na kumbi zenu'' amesema.

Rais Samia alisema ukataji wa miti ni suala ambalo linaharibu mazingira na ripoti iliopo mikoa vinara ya ukataji miti iko Pwani, Morogoro, Tabora, Lindi na Ruvuma, ambapo misiti na miti.

''Pwani inaongoza kwa ukataji miti sana ndio chanzo cha uhaba wa maji ndani ya Jiji la Dar es Salaam na hili naagiza wakuu wa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Dawasa kukaa pamoja na Waziri Mkuu kuhakikisha wanaondoa watu wote wanaofanya shughuli zao katika vyanzo vya maji'' alisema.

Aliongeza ''Miti ina umuhimu mkubwa, watoto wanashindwa kufanya shughuli zao nyumbani kutokana na kutumia nguvu kubwa kukata kuni, utafutaji wa kuni unaleta vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa na kuchelewa kupigwa.''

Pia, alisema sasa ni wakati wa kubadilisha mtazamo wa watu wa upandaji miti na kila mkoa waanze mikakati ya kuangalia ni miti gani inamea zaidi hususan ya matunda na hilo aliwahi kutoa maagizo kwa kila mkoa kupanda miti milioni 1.5.

Rais Samia alisema nishati ya kupikia italeta suluhu ya mambo mengi katika jamii kwa kuwa ni suala linalopaswa kupewa kipaumbele katika miaka mitano mbele, ambapo sasa ni kubadilisha mitazamo ya watu kutoka hapa na kwenda mbele kwa kupata utatuzi wa jambo hilo.

Alisema ni lazima twende na nishati safi ya kupikia kwa maendeleo ya nchi, maendeleo ya jamii zetu na kukinga haki za wanawake. Wanawake wanafanya kazi nyingi kwa kujitolea bila malipo, kina mama wanasonga ugali na machozi yanamtoka lakini na wengine hata watoto wenyewe hawawatunzi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema wamejipanga kutumia mjadala huo kuja na mawazo mbadala ili kusaidia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kuwa suala hilo kila mtu analitumia.

Alisema kupika ni moja ya tukio pekee linalounganisha watu wa hali zote wa juu, kati na chini na jambo muhimu kwa kila mtanzania, Watanzania wengi hawajui na wala hawahoji aina ya nishati inayotumika katika kupika vyakula vinaliwa kila siku”.

Waziri Makamba alisema matumizi ya nishati ya tunayotumia kupikia yanahusishwa na madhara mbalimbali ya afya ikiwemo magonjwa ya mfumo wa upumuaji, uharibifu wa mimba na vifo vya watoto wachanga. 

''Takriban watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka nchini Tanzania kutokana na magonjwa yanayotokana na nishati chafu za kupikia zinazotumiwa majumbani ikiwemo kuni na mkaa. Wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa janga hili'' alisema.

Hivyo, alisema Wizara imeona kufanyike kwa mjadala wa kitaifa utakaofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam ili kuweka mikakati ya kisera, kiuchumi na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kama njia ya kulinda afya za wanawake.

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa Mjadala wa kitaifa wa Masuala ya Nishati Safi.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Akitoa maelekezo kwa Waziri wa Nishati.
EWaziri wa Nishati, January Makamba akizungumza wakati wa kufungua mjadala juu ya Masuala  ya Nishati Safi ya Kupikia. 



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad