HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 20, 2022

KWANINI MFUMO WA ETS NI SAHIHI KATIKA UKUSANYAJI WA KODI.

 
KUTOKANA na wakusanya kodi kukabiliwa na changamoto ya kujua viwango vya kweli vya kodi kwa uzalishaji uliopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifikiria kutafuta njia nyingine ya kisasa na sahihi ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Kazi ya kupata mfumo sahihi kukabiliana na changamoto hiyo ilipewa kampuni ya Uswisi, ya Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA). Kampuni hii ilikuja na mfumo wa stempu wa kielektroniki (ETS).

Kufanikisha utendaji wakeTRA iliweka awamu kadhaa za utekelezaji wa mfumo, ambapo katika awamu ya kwanza ya mfumo, iliyozinduliwa Januari 15,2019 stempu za kielektroniki ziliwekwa kwa kampuni 19 zinazozalisha bidhaa za pombe, mvinyo na vinywaji vikali nchini.

Awamu ya pili ya stempu za kielektroniki iliyoanza Agosti 1,2019 ziliwekwa kwenye bidhaa kama vile maji yaliyotiwa ladha tofauti na kwenye vinywaji vingine visivyo vya kileo.

Katika mahojiano Meneja Miradi wa TRA wa Mfumo wa ETS, Innocent Minja anasema lengo kuu la kutafuta mfumo mpya wa ukusanyaji kodi na uzinduzi wa ETS miaka mitatu iliyopita ni kulinda mapato ya serikali.

"Tulikuwa na changamoto kubwa ya ukusanyaji wa kodi kutokana na watu kutokuwa wa kweli na pia uwapo wa uzito katika ulipaji kodi kwa hiari.

“Awali tulilazimika kuweka maofisa wetu kuangalia uzalishaji na kuhakikisha watengenezaji wanatangaza viwango vya kweli vya uzalishaji. Hata hivyo, hali hiyo ilikuwa na changamoto nyingi na kuonekana kama vurugu tukahitaji suluhu mpya,” anasema Minja.

Minja anasema kutokana na baadhi ya wazalishaji kutokuwa wakweli kuhusu uzalishaji wao na hivyo kusababisha ushindani usio wa haki wa bidhaa zao sokoni na wale wanaosema kweli na kulipa kodi stahiki.

Minja anasema kwamba mfumo wa ETS katika kipindi cha miaka mitatu umeimarisha ulipaji wa kodi na hivyo kuimarisha ushindani wa haki sokoni.

"Hii imesababisha kila mtengenezaji wa bidhaa iliyomo kwenye mfumo kulipa kodi kwa haki," anasema Minja.

Ufungaji wa ETS umehakikisha kuwa TRA inapata data za uzalishaji kwa wakati (muda halisi) kutoka kwa watengenezaji.

"Hii ni kwa sababu ya kodi ya ushuru kwa bidhaa maalumu hutozwa kwa kwango cha uzalishaji hiyo kujua takwimu za uzalishaji ni muhimu."

Kama ilivyotarajiwa, kuanza kwa mfumo wa ETS uliambatana na uwapo wa vifungo vya usalama kwenye teknolojia husika na kurahisisha usimamizi wa kodi nchini.

“ Mfumo ulileta uwazi kwenye kodi hasa kwenye kodi ya ushuru, Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kodi ya kampuni na hatimaye kupunguza manung’uniko ya walipa kodi,” anasema Minja.

Anasema mchakato wa ufungaji ni endelevu haswa kutokana na viwanda kuendelea kuongeza viwango vya mitambo yao.

"Tayari tumeweka mfumo wa ETS kwa watengenezaji wote wanaostahiki wa bidhaa maalum. Takriban vifaa 135 vimefungwa kwenye viwanda vyenye mitambo inayojiendesha huku viwanda visivyojiendesha vikilazimika kuwasha mfumo huo kila wanapoanza uzalishaji,” anasema Minja.

Pamoja na kufanikisha uwekezaji wa mfumo mfumo wa ETS; mfumo huo umekuwa ni msaada mkubwa kwa wazalishaji na waingizaji wa bidhaa mbalimbali.

Mfumo huo pia umewezesha wazalishaji wa bidhaa kujua kiasi cha bidhaa zinazoingizwa sokoni kutoka nje, hivyo kusaidia kuwapatia taarifa wazalishaji wa ndani nini wakifanye ili kuhami bidhaa zao sokoni dhidi ya zile zinazotoka nje.

"Mfumo huu umeongeza uwazi, na kwa sasa, watengenezaji na waagizaji wa bidhaa zilizomo kwenye mfumo wanahakikishiwa usawa sokoni kwa kuwa kila mtu analipa ushuru wa kweli na sahihi wa bidhaa husika na kinyume na awali kabla ya mfumo."

Aliongeza kwamba ETS sio tu imerahisisha kadirio la makusanyo ya kodi, lakini pia mfumo umesaidia wazalishaji kutambua kiasi cha uzalishaji na muda ulitumika kuzalisha bidhaa husika. Pia imesaidia kujua changamoto zinazohusiana na mchakato wa uzalishaji na kutafuta suluhu za changamoto hizo. ETS ikitumika vizuri kwa usahihi malipo ya VAT pia yanakuwa sahihi na pia kurahisisha ukusanyaji na ulipaji wa kodi.

Pamoja na ufanisi uliowezeshwa na mfumo huo, TRA imesema imekuwa ikikabiliana na baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitumia stempu za kughushi.

“Tunawaomba wazalishaji, waagizaji na wananchi kwa ujumla, kutumia kwa dhati mfumo huo na kuepuka matumizi ya stempu za kughushi,” anasema Minja na kuongeza kuwa TRA inafuatilia kwa makini ufanisi wa mfumo huo pote nchini.

Kwa mujibu wa Minja Mamlaka huendesha kampeni kampeni za mara kwa mara kuelimisha wafanyabiashara jinsi ya kuzitambua stempu hizo za kugushi.

Afisa wa TRA, Bw. Chama Siriwa akitoa elimu kwa wananchi na kuhamasisha kutumia App ya Hakiki Stempu na kupakua app hiyo katika simu zao ili waweze kuhakiki vinywaji kabla ya matumizi.


Maofisa wahamasishaji wa program ya ETS - Hakiki Stempu wakitoa elimu kwa wafanyabiashara katika zoezi linaloendelea la kuhamasisha matumizi ya App hiyo katika sehemu mbalimbali nchini.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad