HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 22, 2022

TTCL WAOMBWA KUSHIRIKIANA NA MASHIRIKA YA MAWASILIANO ZANZIBAR

 Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dk. Khalid Salum Mohamed ameliomba Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL - Corporation) kushirikiana na taasisi zinazosimamia mawasiliano Zanzibar ili kutatua changamoto za mawasiliano maeneo mbalimbali hasa kipindi hiki ambacho kumekuwa na ongezeko la watalii wanaotembelea vivutio anuai.

Waziri Dk. Khalid Salum Mohamed ameyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam alipokuwa katika ziara yake ya kuitembelea shughuli za TTCL na miundombinu yake kwa lengo la kujifunza na kuboresha ushirikiano wa taasisi hiyo na Zanzibar.

Alisema malengo ya Zanzibar ya baadaye ni kuwa na Uchumi wa Kidijitali Digital unaokwenda sambamba na uchumi wa bluu ambao pia unategemea teknolojia ya mawasiliano. "...Rasilimali kubwa itakayotufikisha katika uchumi wa bluu Zanzibar ni kufanya vizuri kwenye sekta ya uvuvi kutokana na kuzungukwa na bahari, sekta ya usafiri na usafirishaji mali, sekta ya masuala ya mafuta na gesi, masuala ya utalii hasa katika fukwe na bahari, na viwanda vinavyotokana au kutegemea sekta zilizotajwa hapo juu," alisisitiza Mhe. Dk. Khalid Salum Mohamed.

Alibainisha kuwa ujio wa filamu ya 'The Royal Tour' iliyotengenezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Hussein Mwinyi imechochea ongezeko la watalii Zanzibar kwa kiasi kikubwa ambapo idadi hiyo kubwa ya watalii inahitaji huduma za mawasiliano, hivyo kuona haja ya kujiandaa na kujipanga namna ya kuboresha zaidi eneo hilo la mawasiliano.

"...TTCL ni Shirika kongwe kwenye sekta ya mawasiliano na linaweza kutusaidia kiushauri na hata kuboresha huduma za mawasiliano, mfano kuna suala la kuiunganisha Pemba na Unguja kimawasiliano, tunafikiria kuiunganisha pia Tanga na Pemba kimawasiliano, kuiunganisha Dar es Salaam na Fumba-Unguja, tunataka maeneo yote haya yawe na mawasiliano ya uhakika na huduma za ziada za mawasiliano."

"...Tuna mipango pia ya kuanzisha Data Center maana tuliyo nayo ni ndogo, kuanzisha kituo cha kukuzia na kuboresha vipaji vya vijana wetu pia, eneo hilo pia tunaamini TTCL ndio wanaweza kusaidia kiushauri ili kufanikisha kutokana na uzoefu wenu," alisema.

Kwa upande wake TTCL ilibainisha nachangamoto inazozipata katika utekelezaji miradi ya jamii Zanzibar, ikiwemo vifaa vya miradi vinavyoingizwa kwa utekelezaji miradi ya mawasiliano kutozwa kodi mara mbili na VAT kutozwa kwa viwango viwili yaani asilimia 18 na 15, hivyo kuongeza gharama za huduma kwa mwananchi na kumuomba Waziri huyo kusaidia punguzo.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dk. Khalid Salum (kulia) akiwa katika ziara ya TTCL Makao Makuu ya Ofisi hizo.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dk. Khalid Salum (kulia) akiwa katika ziara ya TTCL Makao Makuu ya Ofisi hizo.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dk. Khalid Salum (wa pili kulia) akizugumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL- CORPORATION), Bw. Peter Ulanga (wa kwanza kulia) alipotembelea shughuli za TTCL katika ziara ya kikazi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad