HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 21, 2022

RC, RAS Tanga wakerwa usimamizi mbovu miradi ya halmashauri

 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kuwa na mkakati wa pamoja kuokoa mapato katika halmashauri hiyo.

Malima amesema hayo jana wakati akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wilayani Korogwe.

“Ukitosheka na kidogo kila siku unakuwa mdogo, madiwani tutamani vitu vikubwa na sisi hapa dhahabu yetu ni mkonge tuitunze kama chanzo cha mapato. Mapato yetu mwaka mzima Sh milioni 400 hamuoni haya, pambaneni halmashauri yenu iwe na fedha.

“Nawasihi madiwani kaeni kwenye nafasi ya kujielewa kuinusuru Korogwe, ukiangalia hoja za CAG ziko 38, zote hizo za nini na katika hizo za msisitizo ziko 15 hii inamaanisha kuna kitu hakiko sawa.

“Nitamuita mkurugenzi nitamuuliza kama ameshindwa kazi wala simsubiri Mheshimiwa Rais aje kuniuliza kama nimeshindwa kazi nitatenda kabla sijaulizwa. Matarajio yangu Korogwe Wilaya mtajipanga na mtakuja vizuri,” amesema Malima.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema alisema Halmashauri ya Korogwe ni moja ya halmashauri ambazo zimekuwa hazifanyi vizuri hususani kwenye usimamizi wa miradi na watendaji wake bado wanaendelea kufanya kazi kwa mazoea.

Alisema Machi mwaka huu ilifanyika tathmini ya utendaji kazi kwa halmashauri zote hapa nchini na katika mkoa wa Tanga kuna halmashauri tatu ambazo utendaji wake ulionekana  hauridhishi kulingana na vigezo vilivyoainishwa na kubainisha kuwa miongoni mwa hizo Halmashauri ya Korogwe Wilaya, Lushoto na Bumbuli na sababu ni hizo hizo usimamizi wa miradi na mambo ya asilimia 10.

“Sasa hapo waheshimiwa madiwani mtaona bado kuna watendaji ambao wanaendelea kufanya kazi kwa mazoea kwa sababu hawatekelezi wajibu wao ipasavyo, hawajali na mwisho wa siku wanasababisha halmashauri ya Wilaya ya Korogwe iingie kwenye matatizo kwa ajili ya watendaji wachache ambao mwaka 2020 wananchi waliwapa dhamana ya kusimamia halmashauri yao,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, aliwataka madiwani kuona kwamba wao ni sehemu ya kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe inafanya vizuri ambapo pia aliwataka kuripoti iwapo mtendaji anakwamisha miradi ya halmashauri hiyo.

“Nawashauri kusema kama mnaona kwamba huyu mtu anatukwaza na kuendelea kuwepo kwake sisi hatutafanikiwa lakini mkikaa kimya na ninyi mnakuwa ni sehemu ya hilo tatizo.

“Mkurugenzi na wewe usicheke na hawa watendaji wanaolega lega, taratibu zinakuruhusu kama mtumishi hawajibiki kwenye utumishi wa umma kama. Tunataka mwakani tukija basi muwe sehemu ya kupongezwa kutoka kwenye hali moja kuelekea nyingine," alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad