HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 24, 2022

WANAVYUO KUNUFAIKA NA MRADI WA UBUNIFU WA 'INNOVERSITY PROJECT'

 


Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania H.E Nabil Hajlaoui akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mradi wa ubunifu wa ''The Next Phase of Academia Enterpreneurship ' Innoversity Project'' mradi ambao umefadhiliwa na ubalozi wa Ufaransa katika kusaidia taasisi za elimu ya juu katika kuinua ubunifu na ujasiriamali zaidi ya taaluma na utafiti, Leo jijini Dar es Salaam.


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

UBALOZI wa Ufaransa Nchini Tanzania umefadhili mradi wa ubunifu wa 'Innoversity Project' kwa miaka miwili unaowalenga wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (Arusha,) Chuo kikuu cha Sokoine (SUA,) na Chuo Kikuu cha Iringa kwa ruzuku ya Euro 570,000 kwa malengo ya kuimarisha Taasisi na nyenzo za elimu ya juu Tanzania, kusaidia safari ya ujasiriamali ya wanafunzi pamoja na kukuza ujasiriamali na ajira.

Mradi huo wa ubunifu na uvumbuzi uliofadhiliwa na Ubalozi wa Ufaransa nchini unatekelezwa na kampuni ya Sahara Ventures wataalam wa biashara na kilimo pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH.)

Akizungumza wakati akizindua rasmi mradi huo, Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania H.E Nabil Hajlaoui amesema kuwa mradi huo wa uvumbuzi unaunga mkono juhudi za Serikali katika kuvipa vyuo vikuu maarifa, zana na rasilimali za kukuza ubunifu, ujuzi wa kujiajiri na ujasiriamali na wanategemea matokeo chanya kwa kunufaisha Tanzania na nchi nyingine za Afrika.

''Licha ya kudumisha mahusiano bora yaliyopo baina ya Ufaransa na Tanzania pia tunatambua jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika masuala ya ujasiriamali na uvumbuzi na hata alipotembelea Paris alitembelea sehemu nyingi na kuzungumza namna ya kuleta ujuzi hapa nchini kwa manufaa ya watanzania hasa vijana.'' Amesema.

Balozi Nabil amesema, ndani ya miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huo vijana watumie kujijenga kimaarifa na kuweza kutengeneza biashara zitakazonufaisha taifa na jamii kwa kuzalisha ajira nyingi zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH,) Samson Mwela amesema, mradi huo wenye lengo la kuwezesha wabunifu na wajasiriamali umeweka mkazo katika sekta ya kilimo na ujasiriamali kwa vijana wa vyuo vikuu ili kutatua changamoto ya ajira.

''Serikali inatoa fedha nyingi kusaidia tafiti na bunifu kupitia COSTECH, mwaka huu imetoa bilioni 3.5 na mwakani tunategemea kupokea bilioni 5 zaidi niwatake vijana na wabunifu kutoka vyuo nufaika vya mradi huu wajitokeze kupitia mradi huu na miradi mingine mingi inayosimamiwa na COSTECH.'' Amesema.

Aidha amesema kuwa, kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa miaka mitano wa maendeleo uliolenga kutengeneza ajira nyingi zaidi kupitia ubunifu na uvumbuzi na mradi huo utaongeza nguvu zaidi katika kutatua changamoto ya ajira na kutengeneza biashara nyingi zitakazosaidia kukuza pato la taifa kupitia kodi.

''Mradi huu utanufaisha zaidi ya wanafunzi vijana 300 pamoja na wahadhiri na watafiti kutoka vyuo vikuu vitatu Tanzania, huu ni mradi wa kihistoria kwa kuwa kutakuwa na ubadilishanaji wa ujuzi kwa watanzania kwenda Ufaransa na vijana wa Ufaransa kuja Tanzania kujifunza zaidi.'' Amesema.

Mwele ameishukuru Serikali ya Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano wenye tija na Tanzania na kuahidi ushirikiano katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa asilimia 100.

Vilevile Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures Jumanne Mtambalike ambao ni watekelezaji wa mradi huo amesema kuwa,wamekuwa daraja la kuiweka Serikali na Ubalozi kupitia mawazo ya ubunifu kutoka kwa wanafunzi na wahadhiri ili kuhakikisha mawazo hayo yanafanyiwa kazi na kuleta tija kwa jamii ya sasa hasa kwa vijana na kuwataka wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizo.

Mradi huo utafanya kazi na vituo vya uvumbuzi vya vyuo vikuu na ofisi za kuhamasisha teknolojia ili kuhimiza zaidi uvumbuzi, ujasiriamali, uhamishaji wa teknolojia na biashara ya utafiti ili kuunda suluhisho jipya na fursa za ajira.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures Jumanne Mtambalike akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo na kuwataka wadau zaidi kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla, Leo jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH,) Samson Mwela akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo na kueleza kuwa Serikali inatambua juhudi za Serikali ya Ufaransa na itaendelea kushirikiana nao katika kuyafikia maendeleo zaidi, Leo jijini Dar es Salaam.Uzinduzi ukiendelea.


Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia uzinduzi huo.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad