HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 9, 2022

WANANCHI WASHINDWA KUVUNJA MILANGO YA JELA

 Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

TUNAWEZA kusema! Wananchi, Yanga SC wameshindwa kuvunja Milango ya Jela baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na Maafande wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons SC katika mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC Premier League) uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Tanzania Prisons SC imeilazimisha sare ya tatu mfululizo Yanga SC ambayo kabla ya mchezo huo imetoka sare na timu za Simba SC, Ruvu Shooting FC katika kindumbwe ndumbwe hicho cha Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu huu wa 2021-2022.

Yanga SC waliingia kuwakabili Prisons kwa lengo la kupata ushindi na kufuta wimbi la sare lililokuwa linawakabili, ambazo walipata katika michezo hiyo miwili iliyopita, lakini Maafande hao wa Magereza walifanikiwa kuwazuia vilivyo Wananchi ambao safu yao ya ushambuliaji ilikuwa ikiongozwa na Mshambuliaji mahiri, Fiston Kalala Mayele.

Akizungumza baada ya mtanange huo, Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Cedric Kaze amesema hawawezi kuwa na furaha kutokana na kukosa alama tatu muhimu katika michezo mitatu mfululizo. Kaze amesema Mashabiki wa timu hiyo na Viongozi waendelee kushikamana ili kuhakikisha wanapata ushindi katika michezo inayofuata katika Ligi hiyo.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons SC, Patrick Odhiambo amesema waliingia kwa lengo la kupata alama tatu muhimu dhidi ya Yanga SC lakini kutokana na hali ya mchezo na kukabiliana na timu bora, amesema wanashukuru kupata alama hiyo moja katika mchezo huo.

Katika mchezo huo licha ya kuwaongeza, Wachezaji Heritier Makambo, Dennis Nkane, Faridi Mussa, Yanga SC walishindwa kupata bao katika mchezo huo na kupata sare ya tatu, hata hivyo Wananchi wanafikisha alama 57 na michezo 23 wakiendelea kuongoza Ligi hiyo ya NBC, huku kukiwa na tofauti ya alama 11 na Simba SC, wakati Tanzania Prisons wakifikisha alama 23 wakiwa na michezo 23 wakisogea nafasi ya 14 kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi hiyo.
Mshambuliaji wa Yanga SC, Saido Ntibazonkiza akijaribu kumtoka Mlinzi wa Tanzania Prisons, Nurdin Elfadhili (mwenye Jezi nyeupe) katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, timu hizo zilitoka sare ya 0-0.
Mshambuliaji wa Yanga SC, Fiston Mayele akijaribu kumtoka Mlinzi wa Tanzania Prisons SC, Vedastus Mwihambi katika mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara ambapo timu hizo zilitoshana nguvu ya sare ya 0-0 katika dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, katika mchezo huo Mayele alikosa Penalti kwenye dakika ya 38 baada ya kuipaisha juu ya lango la Tanzania Prisons.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad