HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 9, 2022

Mashtaka 33 yamfikisha kizimbani Mkurugenzi UDART

MKURUGENZI wa Kampuni ya Huduma za Usafirishaji wa Mabasi yaendayo kasi, (Udart), Robert Kisena na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 33 yakiwemo ya kutakatisha fedha, na kuisababishia hasara Serikali ya Sh 5.2 bilioni.


Washtakiwa hao wamesomewa kesi mbili tofauti za uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Godfrey Issaya na Hakimu Mkazi Mku Pamela Mazengo leo Mei 9, 2022

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na jopo la mawakili watano wandaamizi wa Serikali wakiongozwa na Pius Hilla akisaidiana na Jackline Nyatori, Ester Martin, Iman Mitumemingi na Upendo Temu wamewataja washtakiwa wengine mbali na Kisena kuwa ni Charles Newe (48) Mkurugenzi wa Udart, mfanyabiashara John Samangu (66) na Mtunza fedha Tumaini Kulwa (44).

Mbele ya Hakimu Issaya, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Jackline Nyantore amedai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 18 yapo ya kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa, Kisena, Newe na Kulwa, mashtaka manne ya kughushi, mashtaka manne ya kuwasiliana nyaraka za uongo, mashtaka nane ya utakatishaji fedha na moja la kuisababishia hasara mamlaka hiyo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Agosti Mosi na Agosti 30, 2015, waliongoza genge hilo la uhalifu ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na kujipatia Sh bilioni 4. 5 kutoka katika mradi wa Shirika la usafirishaji Dar es Salaam ( DART) fedha ambazo zilikuwa katika akaunti ya Shirika hilo iliyopo benki ya NMB tawi la Benki House.

Katika shtaka la kuisababishia hasara mamlaka, inadaiwa, kati ya Juni Mosi 2015 na Aprili 30, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa Wakurugenzi wa UDART kwa nia ovu walisababishia Shirika hilo hasara ya sh. bilioni 5.2

Aidha mbele ya Hakimu Mazengo, washtakiwa Kisena, Newele, Samangu na Kulwa ambapo wanakabiliwa na mashitaka 15 yakiwemo ya kuisababishia UDART hasara Sh milioni 750.

Washitakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu ambapo wanadaiwa walitenda kosa hilo katika nyakati tofauti kati ya Mei 25 na Julai 10, mwaka 2016 maeneo tofauti Jijini Dar es Salaam, ambako waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh milioni 750 kutoka akaunti ya UDART iliyoko katika benki la NMB tawi la Benki house.

Pia washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kughushi ambayo ni matatu na kuwasilisha nyaraka za uongo matatu na utakatishaji fedha tisa

Katika mashitaka ya kughushi wanadaiwa mshitakiwa Kisena, Newe na Kulwa wanadaiwa Mei 26, mwaka 2016 Jijini Dar es Salaam, kwa udanganyifu walighushi fomu inayoitwa fund transfer request wakijalibu kuonyesha kwamba UDART imehamisha kiasi Cha sh. milioni 750 kutoka akaunti yake iliyoko Benki ya NMB kwenda akaunti inayomilikiwa na Kampuni ya Long way engineering Ltd iliyoko Benki ya KCB kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mabasi na uzio eneo la Kimara, Kivukoni, Ubungo na Moroco, wakati wakijua sio kweli

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo umeishakamilika na wameomba wapewe muda kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ili hatua nyingine zinazofuata ziendelee

washtakiwa hao, wamerudishwa rumande hadi Mei 23, mwaka huu kesi hizo zitakapojwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad