HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 13, 2022

NCHI NANE KUSHIRIKI KONGAMANO LA KISAYANSI, MAKAMU WA RAIS KUZINDUA

 MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuzindua kongamano la 31 la Kisayansi Mei 17, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) litakuwa kwa siku tatu Mfululizo Kuanzia Mei 17 hadi Mei 19 litajadili masuala ya Ushiriki wa Sekta mbalimbali katika Afya ikiwa na ajenda ya kuimarisha mifumo ya Afya kufikia huduma ya Afya kwa wote.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 13, 2022 jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya amesema kuwa huduma ya Afya kwa wote inamaanisha wananchi wote waweze kufikiwa na huduma mhimu za afya zinazohusisha uelimishaji kuhusu Afya bora, kinga, matibabu utunzaji wa dawa na hatimaye kuboresha maisha ya Mtanzania.

Amesema kuwa kongamano hilo litashirikisha wataalamu zaidi ya 300 kutoka taasisi mbalimbali za kitaifa wakiwemwo watafiti, watunga sera, wakuu wa taasisi za serikali, wakurugenzi wa Afya katika ngazi za halmashauri, Mashirika yasiyo ya kiserikali wadau wa kimataifa wa maendeleo wataalamu wa Afya na Wafadhiri.

Aidha amesema jumla ya maandiko 260 ya Kisayansi yanatarajiwa kuwasilishwa katika kongamno hilo kupitia mada ndogondogo zitakazohusu Magonjwa mbalimbali, vichocheo vyake ufanisi katika mfumo wa afya.

Pia amesema Mfumo wa afya katika maeneo ya magojwa ambukizi yanayoibuka na yanajitokeza upya baada ya kutokomezwa yatawasilishwa.

Tiba asili, usugu wa dawa katika tiba za magonjwa na mifumo ya udhibiti wa magonjwa yakiwemwo Kifua kikuu na Malaria kwa watu wazima na watoto, Afya ya mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi, Magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo mgonjwa sugu ya Mapafu, Kisukari, Shinikizo la damu na Saratani.

Mawasilisho mengine ni Changamoto za afya zitokanazo na janga la UVIKO 19, Lishe, afya ya Mama, Mtoto na Vijana, Magonjwa yasiyopewa kipaumbele yakiwemwo kichocho, Usubi, Matende na Mbusha, Minyoo tumbo na Vikope pamoja na Udhibiti na Usimamizi wa Tafiti za tiba.

Amesema kongamano hilo litaenda sambamba na Monesho yanayolenga kutoa ufahamu zaidi juu ya kazi zinazofanywa na Taasisi za afya, watoa huduma na wengine wa nje ya sekta ya afya na wadau wengine ni TMDA, MUHAS na NMB.

Kongamano hilo la Kisayansi la NIMR huwa na utaratibu wa kutoa tuzo mbalimbali zinazolenga kuthamini mchango wa kazi za watafiti wachanga, waliobobea na wabunifu ambao wanaleta mchango mkubwa katika kuboresha sera na mifumo mbalimbali ya utendaji kazi katika sekta ya afya ya kitaifa na kimataifa.

Kwa Upande wake Mkurugenzi, Mratibu wa Taarifa na Mawasiliano ya Kitafiti, Dkt. Ndekya Oriyo amesema kongamano hilo litahusisha watu mbalimbali kutoka Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Senegal, Norway, Uingereza, Ujerumani na Marekani.

NIMR imekuwa ikiratibu kongamano la Kisayansi tangu 1982 Kwa lengo la kusambaza matokeo ya tafiti za afya zinazofanywa na watafiti wa NIMR na wadau wengine waliopo ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad