HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 28, 2022

WANAFUNZI WAHITIMU KIDATO CHA SITA SEKONDARI YA WASICHANA MAKETE WATAKIWA KUTAMBUA KIDATO CHA SITA SIO MWISHO WA ELIMU YAO

Na Edwin Moshi, MAKETE.

Wanafunzi wahitimu wa kidato cha 6 katika shule ya sekondari ya Wasichana Makete (Makete Girl's) wametakiwa kutambua kuwa kila mmoja maisha yake anayapanga kutoka kichwani kwake kwenda kwenye moyo wake na wasikubali kidato cha sita kiwe ndio mwisho wao kielimu

Hali kadhalika wametakiwa kuwaripoti wazazi ama walezi ambao wanawataka wahitimu hao waolewe baada ya kuhitimu kwa kuwa ni kosa kisheria ili hatua zichukuliwe

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Makete Mstaafu Josephine Matiro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Kwanza ya kidato cha 6 katika shule hiyo ambayo ilianzishwa wakati wa uongozi wake na yeye akiwa miongoni mwa waliofanikisha uwepo wa shule hiyo

Matiro amesema wanafunzi hao wanapaswa kuwa na malengo ya juu zaidi pamoja na kufahamu kwamba kumaliza mitihani sio mwisho wa masomo bali ndio mwanzo wa masomo kwani wanatarajiwa kuendelea na masomo katika vyuo vikuu ama vyuo vingine mbalimbali hapa nchini

Amewasihi wanafunzi hao kwenda kuitangaza vema shule hiyo huko wanakokwenda kwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa pamoja na kuchukua mambo mazuri waliyofundishwa na walimu wao na wakayaishi huko wanakokwenda

Pia Matiro ameipongeza serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiboresha shule hiyo kwani imeendelea kuboreshwa tofauti na alivyoiacha wakati akiwa mkuu wa wilaya

Suala la shule hiyo kukosa gari ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili shule hiyo kama ilivyoelezwa kwenye taarifa fupi ya shule iliyosomwa na Mwl. Matinya, Makamu Mkuu wa Shule hiyo kwa niaba ya Mkuu wa shule pamoja na risala ya wahitimu kwa mgeni rasmi, ambapo imejibiwa na mgeni rasmi kwamba tayari halmashauri inalishughulikia suala hilo na litatatulika muda si mrefu
 
Baadhi ya wahitimu waliozungumza na mwandishi wetu akiwemo Marieta Yohana na Anna David mbali na kuahidi kufanya vizuri kwenye mitihani yao ili kuendelea kuitangaza vizuri shule yao, pia wanaimani changamoto zinazoikabili shule hiyo zitaendelea kutatuliwa na serikali.




 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad