HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 11, 2022

RUWASA MKOA WA MTWARA ILIVYOJIPANGA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI

 


Na Muhidin Amri,
HAKUNA maendeleo yeyote katika nchi bila maji, na hii linatokana na umuhimu wake ndiyo maana kuna msemo maarufu unaosema kuwa maji ni Uhai.

Pamoja na harakati na mipango mingi ya Serikali kujenga na kuboresha huduma mbalimbali ili kuwaletea wananchi wake maendeleo,lakini huduma ya maji imepewa kipaumbele na msukumo mkubwa kwa kuwa ni kama Uti wa mgongo katika maisha ya kila siku ya binadamu.

Hili linathibitishwa na jitihada zinazofanywa na serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA,kwani tangu ilipoanzishwa miaka mitatu iliyopita imeonesha kwa vitendo ni jinsi gani huduma ya maji ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa jumla.

Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA mkoa wa Mtwara, ni taasisi iliyoko chini ya wizara ya maji ambayo imejipanga kuhakikisha maeneo iliyopangiwa kwa ajili ya kutoa huduma wananchi wanapata maji safi na salama.

Ikumbukwe kuwa,Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa michache hapa nchini yenye changamoto kubwa ya huduma ya maji safi na salama,hata hivyo wizara ya maji kupitia RUWASA imekuja na mikakati kabambe yenye lengo la kumaliza kabisa tatizo hilo.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damas anaeleza kuwa katika mkoa huo,wananchi wanaopata huduma ya maji kwa wakazi wa vijijini ni 672,672 sawa na asilimia 60.16 na mijini watu 282,945 sawa na asilimia 82.

Mhandisi Damas anasema, vyanzo vilivyoendelezwa katika mkoa huo kwa pamoja vinauwezo wa kuzalisha lita 21,186,300 kwa siku ukilinganisha na mahitaji ya lita 46,088,340 kwa siku sawa na asilimia 46.

Anasema,vyanzo vilivyopo vina uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo milioni 14,947 kwa mwaka na maji yanayotumika ni mita za ujazo milioni 2,661 kwa mwaka sawa na asilimia 17.80.

Akizungumzia hali ya utoaji wa huduma ya maji vijijini anasema,huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini imekuwa inaongezeka kwa kasi kidogo ikilinganisha na kasi ya ongezeko la watu na hali hiyo inatokana na uwekezaji mdogo uliokuwa unafanywa na serikali katika sekta ya maji.

Aidha anabainisha kuwa,Mkoa ulikuwa na lengo la kufikisha asilimia 64 ya utoaji wa huduma ya maji kwa wakazi waishio vijijini,hata hivyo katika kipindi husika hali imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 59.53(Mwezi Juni 2020) hadi kufikia asilimia 60.16.

Meneja Damas anasema,hatua hiyo inatokana na nguvu kubwa ya uwekezaji wa miundombinu ya maji unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza mipango mbalimbali katika mkoa huo.

Anasema kutokana na uwekezaji unaofanywa katika sekta ya maji mkoani Mtwara, ni matumaini ya RUWASA kwamba huduma ya maji itazidi kuongezeka hadi kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa miradi mingi imeanza kutekelezwa.

Damas anasema,katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi unaendelea kuboreshwa,RUWASA Mkoa wa Mtwara imendelea kuwezesha, kusimamia ujenzi na kukamilisha miradi ya maji vijijini katika maeneo mbalimbali ya wilaya husika kupitia fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji(NWIF)na mipango ya lipa kwa matokeo(P4R)na lipa kabla ya matokeo(PbR).

Anasema,katika Mwaka wa fedha 2021/2022 RUWASA Mkoa wa Mtwara imepanga kutumia jumla ya Shilingi bilioni 12,523,727,274.27 ambazo zitatumika kwenye ujenzi,ukarabati na upanuzi wa miradi mbalimbali na zinakwenda kupunguza kama sio kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wa wilaya hizo tano katika mkoa wa Mtwara

Anataja mgawanyo wa fedha hizo kwa kila wilaya kuwa Masasi (Sh.2,484,329,885.00)wilaya ya Mtwara(Sh.3,367,250,973.27 wilaya nyingine ni Nanyumbu iliyopata (Sh.2,132,694,811.00) wilaya ya Newala(Sh.2,079,857,372) na Tandahimba (Sh.2,459,594,233).

Hata hivyo anasema, pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini, bado kuna chagamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya maji katika maeneo husika.

Anataja changamoto hizo ni uwekezaji mdogo katika ujenzi wa miradi mipya na uboreshaji wa miradi iliyopo,uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibindamu,uchangiaji duni wa wananchi katika huduma wanayoipata na kukosekana kwa vyanzo vya uhakika vya maji katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mtwaraa hasa wilaya ya Nanyumbu.


MIKAKATI YA UTATUZI WA CHANGAMOTO NA KUONGEZA HUDUMA
Anasema,Serikali kupitia wataalam mbalimbali wa sekta ya maji katika mkoa wa Mtwara imejiwekea mikakati mbalimbali ya utatuzi wa changamoto zilizopo pamoja na kuongeza utoaji huduma ya maji kwa wananchi.

Anataja baadhi ya mikakati hiyo ni, kuiomba Serikali kuongeza bajeti ya uwekezaji wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali vijijini,pamoja na wafadhili na wadau mbalimbali wa uboreshaji wa sekta ya maji kwa jamii.

Mikakati mingine ni kusimamia na kuimarisha vyombo vya watumia maji vijijini kwa lengo la kusimamia,kuchangia na kuendesha miradi hiyo,kushirikisha wataalam husika na wananchi kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji, na kutoa elimu ya dhana ya umiliki wa miradi ya maji kwa jamii.

Anasema, kabla ya kuanzishwa kwa RUWASA hali ya Utekelezaji wa miradi ya maji ilikuwa mbaya licha ya Serikali kutoa fedha kwa wakandarasi na pia gharama ya miradi husika ilikuwa kubwa tofauti na uhalisia.

Anasema, kwa sasa hali ni tofauti baada ya RUWASA kuanza kutumia wataalam wake,hatua anayotaja imesaidia sana miradi mingi kukamilika kwa wakati,kupungua kwa gharama za utekelezaji na wananchi kuanza kupata huduma.

Anaipongeza serikali ya Chama cha Mapinduzi, kutoa fedha kwa Wizara ya Maji ili kutekeleza miradi katika maeneo mbalimbali ambayo imesaidia kupeleka na kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.

Anatoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara, kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji,vyanzo vya maji na mazingira ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija iliyokusudiwa.

Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha anasema, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 wametengewa jumla ya Sh.bilioni 2,082,694,811.00 2021,2022 kwa ajili ya kutekeleza miradi sita ya maji.

Mchucha anasema, fedha hizo zitumika kutekeleza miradi ambayo inahusisha utafutaji wa vyanzo vya maji,kufanya usanifu na ujenzi ambapo kati ya hiyo,miradi mitano ni mipya na imeanza kutekelezwa,na mmoja ni wa zamani unaofanyiwa ukarabati wa miundombinu yake.

Anataja mradi unaofanyiwa ukarabati utahudumia vijiji vya Chivikiti,Holola,Ndwika na Ulanga ambao changamoto kubwa ni kuzalishaji maji kwa kiwango kidogo.

Anasema mradi mwingine ni Mitumbati-Chilunda unaotekelezwa katika vijiji vya Mitumbati na Namijati kata ya Mkonona kwa gharama ya Sh.1,356,000,537 kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uvico-19.

Anasema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 518,000,000 ni za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 na Sh.838,000,537.8 ni za program ya lipa kwa matokeo(PfoR).

Meneja huyo anasema,mradi huo utawanufisha wakazi 3,285 wa vijiji vya Mitumbati na Namijati na chanzo chake ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 15,800 kwa saa moja kinachochimbwa katika kijiji cha Mitumbati.

Akizungumzia upatikanaji huduma ya maji katika wilaya ya Nanyumbu anaeleza kuwa, kwa sasa ni wakazi 76,343 tu kati ya 173,203 sawa na asilimia 44 ya wakazi wote ndiyo wanapata huduma ya maji safi na salama na wenye uhakika wa kupata kiwango cha msingi(Basic amount) cha lita za ujazo 25 kwa siku kupitia miradi inayofanya kazi.

Baadhi ya wakazi wa mkoa huo,wanaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwajengea mradi huo wa maji kwani kwa muda mrefu kilio kikubwa cha wananchi ni ukosefu wa maji safi na salama.

Issa Namwe mwenyekiti wa kijiji cha Mwindi wilayani Mtwara anasema,wananchi wa Mwindi hawakuwa na chanzo chochote za kupata maji, hivyo walilazimika kwenda kutafuta huduma hiyo kwenye vyanzo vya asili ambavyo havikutosheleza mahitaji yao jambo lililosababisha kero kubwa na baadhi ya watu kupigana ili kupata maji kutoka kwenye vyanzo hivyo.

Mkazi wa kijiji cha Chikama wilayani Masasi Rehema Mrope,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kuanza kutekeleza mradi wa maji katika kijiji chao kwa kuamini kuwa, utakapokamilika utawapunguzia adha ya kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji mtoni na katika vyanzo vingine vya asili.
Ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Mwindi kata ya Mbawala linalojengwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa wilaya ya Mtwara,tenki hilo ni sehemu ya mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Shilingi milioni 804,597,262.90 ambao utahudumia wananchi wa kata ya Mbawala wilayani Mtwara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad