HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 11, 2022

Wadua-Utaratibu wa kupokea wanafunzi wa Vyuo Vikuu kutoka nje kutoka nje uboreshwe

 

Wahitimu wakiwa katika mahafali katika moja ya vyuo vikuu nchini yaliyofanyika hivi karibuni. (Picha: Makaktaba)

Na Mwandishi Wetu
WATAALAMU na wadau wa elimu ya juu wamewaomba viongozi wa serikali kuanzisha utaratibu maalum utakaoviruhusu vyuo vikuu nchini kuwapokea wanafunzi kutoka vyuo vya nje kusoma kozi ya shahada Tanzania.

Kwa sasa ni wanafunzi wenye alama za ufaulu sawa na elimu ya sekondari ya juu (Kidato cha Sita) tu wanaruhusiwa kusoma kozi ya shahada nchini, kwa mujibu wa aya 3.1.3 na 3.1.7 za Kiongozi cha Viwango na Mwongozo (Toleo la Tatu) cha Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Mabingwa na wadau wa elimu ya juu wanaona kigezo cha ulinganifu kilichowekwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kama “kikwazo” kwa wanafunzi kutokab nchi za nje —kama vile Kenya, Sudani Kusini, Nigeria, India, Ghana na nchi nyingine nyingi duniani zinavyotumia mifumo tofauti ya elimu ya sekondari.

“Wanafunzi hawa wanahitaji kozi maalumu (kozi daraja) ya kuwafanya wawe na elimu yenye linganifu na elimu ya sekondari ya juu (Kidato cha Sita) ili waweze kupokelewa kwenye vyuo vikuu vya hapa nchini,” alisema Bw Musa Rajab, bingwa wa masuala ya elimu, hivi karibuni.

Kwa sasa ni Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) ndicho kilichoruhusiwa kutoa kozi ya msingi kwa wanafunzi wa Tanzania wanaotaka kujiunga na elimu ya chuo kikuu, lakini walikosa alama chache tu kuweza kuwa na sifa za kujiunga na masomo ya elimu ya juu moja kwa moja.

Mabingwa na wadau wa elimu hawaridhishwi na utaratibu unaoruhusu OUT pekee kutoa kozi ya msingi, huku wakizisihi taasisi za serikali "kufanya marekebisho ya kimkakati" ya Kiongozi cha Viwango na Mwongozo wa TCU na kuweka kipengele kitakachoruhusu vyuo vikuu nchini kutoa kozi ya msingi kwa ajili ya wanafunzi kutoka nchi za nje ambao wamesoma kwenye mfumo tofauti na Tanzania.

“Marekebisho kama haya siyo jambo geni. Nchini Uganda, ambako mfumo wake wa elimu ya sekondari ya juu unafanana na wa Tanzania, baadhi ya vyuo vikuu vimeongeza kozi ya msingi inayodumu kwa mwaka mmoja kwenye mitaala yake kuwaruhusu wanafunzi kutoka vyuo vya nje kuweza kusoma nchini humo. Hali hii imechangia kuongeza fedha za kigeni nchini Uganda na kupanua wigo wa elimu ya juu nchini humo," alisema Bw Mulusali Komba, mdau wa elimu, akiongeza kwamba "nchi nyingi duniani zina utaratibu tofauti tofauti unaoruhusu wanafunzi kutoka nchi za nje kujiunga na kozi ya shahada, ingawa wanafunzi hao walihitimu masomo kutoka katika mifumo tofauti ya elimu."

Marekebisho ya taratibu za usahili, kwa mujibu wa wadua, yatakuwa na manufaa mengi kwa Taifa, ikiwa ni pamoja na kutangaza utalii wan chi kupitia elimu ya juu, ongezeko la fedha za kigeni kwa, na kuharakisha utekelezaji wa agenda ya Kitaifa ya Elimu Juu inayolenga kuinua viwango na ubora wa elimu ya juu Tanzania kufikia kiwango cha kimataifa.

Aya 2.21.4 ya Viwango na Mwongozo wa TCU unavitaka vyuo vikuu Tanzania kuwa na uwiano wa kuanzia asilimia 5 wa wanafunzi wa kimataifa, kwa lengo la kutimiza lengo la Ajenda ya Taifa ya Elimu ya Juu na moja ya kigezo muhimu cha kuweka katika matabaka ya vyuo kikuu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kiongozi cha Takwimu Muhimu za TCU kilichotoka hivi karibuni (Jedwali 13, 14, na 15), vyuo vikuu vyote vya Tanzania kwa pamoja katika mwaka wa masomo 2020/21 vimeandikisha jumla ya wanafunzi wa kimataifa 303 kutoka Afrika Mashariki na nchi zingine, ambayo ni sawa na asilimia 0.19 ya wanafunzi wote 157,101 waliojiandikisha kwenye kozi ya shahada, ambayo ni chini ya Kiwango cha TCU cha asilimia 5.

“TCU ikiruhusu wanafunzi kutoka nchi za nje waliosoma kwa mfuo tofauti wa elimu ya sekondari kupata kozi ya msingi au kozi daraja kama matayarisho ya kujiunga na mfumo wa elimu ya juu nchini, idadi ya wanafunzi kutoka nje ya nchi itaongezeka na utaratibu huu utaongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya elimu ya juu na ushindani wa kimataifa wa vyuo vyetu,” alisema mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Alipotafutwa, Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Charles Kihampa amesema “taratibu na kanuni za kusahili wa wanafunzi kutoka nje ya nchi upo, na vyuo vikuu vinajua. Taratibu hizi zimewekwa na vyuo vyenyewe kupitia kwa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vishiriki. Kama kuna wazo kwamba vyuo vyetu kuruhusiwe kuendesha kozi maalum za msingi kwa wanafunzi kutoka nje ya nchi, swala hilo linapaswa kupelekwa kwenye Kamati husika kujadili na kisha kuleta mapendekezo kwa TCU.”

“Kuhusu hoja kwamba wanafunzi wa kigeni ni wachache katika vyuo vyetu, nadhani hilo ni swala na vyuo vyenyewe. TCU kazi yetu ni usimamizi tu…ni jukumu la vyuo husika kutangaza vyuo vyao kwa nguvu ili kuvutia wanafunzi wengi sana kutoka nje ya nchi,” ameongeza Prof. Kihampa.

Akitoa maoni, mtaalaam wa Elimu ya Juu, Bw. Andrew Moses amesema katika mazingira ya ushindani mkubwa wa elimu ya juu Tanzania and duniani kote, TCU haipaswi kubaki na jukumu la kusimamia tu, inapaswa kutengeneza mazingira ya kuvisaidia vyuo vya Tanzania kuweza kupata wanafunzi kutoka nje na kutuoa elimu yenye viwango na ubora ili kukabiliana na ushindani wa kimataifa.

“Mbali na hilo, majukumu ya TCU (kwa mujibu Sheria ya Vyuo Vikuu--Universities Act Cap. 346, Kifungu cha 5(1) yako katika maeneo matatu—kusaidia, kushauri na kusimamia. Kwa mantiki hiyo, TCU wanapaswa kuwa wabunifu, kuchukua mawazo yenye tija kutoka kwa wadau kutoka sekta binafisi na umma, na kutengeneza mazingira yatayaboresha uendeshaji na utoaji wa huduma ya elimu ya juu katika vyuo vikuu kwa faida ya nchi ya Tanzania.”

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad