Raisa Said,Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amewataka wakuu wa wilaya na maofisa lishe mkoani humo kufanya tathmini na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu suala la lishe.
Aidha amewataka maofisa lishe kutoa elimu kwa wajawazito kuhusu lishe bora na vyakula mbadala sahihi vya dawa za kuongeza damu ili aendelee kuwa salama katika kipindi cha ujauzito pindi anapokosa dawa za kuongeza damu katika kituo cha afya au hospitalini.
Malima amesema hayo jana jijini Tanga, katika kikao kazi cha kutathimini utekelezaji mkataba wa lishe kipindi cha nusu mwaka.
"Kuna maelekezo ambayo serikali imetoa, si maelekezo ya masikhara kuna siku mtakuja kuulizwa na ninyi wakuu wa wilaya ndiyo wenye kusimamia suala la lishe, mkakae na watu wenu wawape tafsiri na uelewa kuhusu lishe kisha tutakuja kujadili kwenye kikao kijacho kama hiki. Tusifike sehemu ambayo tutakuja kuulizwa suala la lishe.
"Mkishakuwa na uelewa wa pamoja ninyi maofisa wa lishe tunaomba mtuainishie uhusiano kati ya lishe na akili za darasani. Maana kama tunataka Tanga iwe na watoto wenye akili basi tuwe na lishe bora na kama mnashindwa kufikia malengo kwa sababu hamna fedha za kutosha mseme." alisema Malima.
Pamoja na mambo mengine, Malima alisema wanaotoa elimu ya lishe kuwaambia watu vyakula au matunda wanayokula yanawasaidia nini badala ya kuwasisitiza kula aina fulani za vyakula huku akiwataka wananchi mkoani hapa kutumia simu zao kuangalia na kujifunza masuala ya lishe.
Awali akitoa tathmini ya lishe ya Mkoa wa Tanga, Ofisa na Mratibu wa Lishe wa mkoa, Mwanamvua Zubeir alisema mkoa unakabiliwa na tatizo la udumavu ambapo asilimia 34 ya watoto chini ya miaka mitano wamedumaa ambapo alishauri halmashauri zote kuwekeza katika lishe kwa sababu lishe ndiyo msingi wa afya njema ya jamii lakini pia nguvukazi ya taifa lenye kuwa na maamuzi yenye kuzalisha.
"Tatizo la udumavu haliathiri tu kimo kwamba mtu ataonekana mfupi lakini maana yake hata ukuaji wa ubongo wake umedumaa. Udumavu unaathiri hata mtoto kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yake darasani akiwa mwanafunzi lakini hata akiwa mkubwa ubongo wake unakuwa hauna maamuzi mazuri ya busara katika jamii.
"Ukuaji wa ubongo unaanzia mtoto akiwa tumboni kwa maana kwamba ili tuwekeze kurekebisha suala la udumavu ni lazima tuwekeze katika lishe ya mama kuanzia anapokuwa .jamzito hadi mtoto atakapozaliwa na kufikisha miaka miwili, hizo tunahesabu ni siku 1,000 yaani kuanzia mimba inapotungwa hadi umri wa miaka miwili baada ya hapo tukimpa mtoto virutubishi tunaweza kurekebisha mambo mengine lakini si ulemavu. Kwa hiyo hiki ndiyo kipindi muhimu zaidi kuwekeza katika suala zima la afya ya mtoto," amesema
Hata hivyo Serikali kupitia Program Jumuishi ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya awli ya mtoto (PJT-MMMAM 2021/22-2025/26 ) Imeelezwa Jitihada za kushughulikia Hali ya lishe ya watoto nchini zimekuwa na mafanikio malubwa kupitia afua maalum za kuboresha lishe (Scaling Up Nutrition- Sun) ambazo ni harakati za kimkakati zinajumuisha wadau mbalimbali.
Japokuwa karibu watoto wote asilimia 96.6 wenye umri wa miezi 0-23 wamewahi kunyonyeshwa ,Bado ipo haja ya kuboresha Kwa kuanza kunyonyesha mtoto saa moja baada ya kuzaliwa ni asilimia 53.5. vilevile unyonyeshaji pekee wa maziwa ya mama Kwa watoto wa miezi 0-6 ni asilimia 58.
Pia Kuna upungufu mkubwa wa unyonyeshaji katikamwaka wa pili ,ambapo asilimia 92.2 ya watoto waliendelea kunyonyeshwa Kwa mwkaa wa kwanza ikishuka hadi asilimia 43.3 Kwa miaka miwili kama inavyopendekezwa. Wakati huo huo asilimia 92 ya watoto wenye umri wa kati ya miezi 6 hadi 8 walianzishiwa vyakula vya ziada Kwa wakati inafaa.
No comments:
Post a Comment