HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 11, 2022

LUDEWA KUANZA UVISHAJI NG'OMBE HERENI ZA KIDIGITALI

 



Na. Damian Kunambi, Njombe


Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Andrea Tsere amewaagiza Viongozi wote wa ngazi ya kata na vijiji kutoa elimu kwa wafugaji wa ng'ombe juu ya zoezi la uvishaji hereni kwa mifugo hiyo ili kuweza kutambua idadi yao katika wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkuu huyo ameongeza kuwa hereni hizo zitasaidia kujua afya ya mifugo,uhitaji wa maeneo ya malisho na kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji hivyo amewataka wafugaji kuonyesha ushirikiano wao ili kufanikisha zoezi hilo.

Amesema katika zoezi hilo kwa asilimia kubwa limegharamiwa na serikali hivyo kwa upande wa wafugaji watapaswa kugharamia hereni ambayo gharama yake haipungui shilingi 1500.

"Wafugaji mnapaswa kuunga mkono zoezi hili kwakuwa lina faida kubwa sana kwenu, kwani changamoto nyingi zinazohusiana na mifugo zitakwenda kumalizika", Amesema Tsere.

Ameongeza kuwa endapo ng'ombe atavaa hereni atakuwa ameunganishwa katika mfumo wa computer ambao utawezesha kujua afya yake, eneo alilopo na hata ikitokea anaibiwa inakuwa rahisi kupatikana.

Sanjari na hilo pia amewataka wafugaji wa ng'ombe kufugia mifugo yao kwenye mazizi badala ya kuwaacha milimani wakijichunga wenyewe kitu ambacho huleta uharibifu wa miundombinu ya barabara, maji na mfugaji hupoteza mavuno mengi yanayotokana na ng'ombe.

Amesema mifugo hiyo inapokuwa peke yake porini inakosa uangalizi wa karibu hasa wanapokuwa na watoto (Ndama) kwani ndama hao hupoteza maisha kwa kutumbukia katika mitaro na magonjwa mbalimbali.

"Kuacha ng'ombe porini tunapoteza mazao ya mifugo yetu, mbolea na hata maziwa ambayo tungeweza kuyatumia kwa afya ya binadamu tunayaacha yananyonywa na sungura huko maporini", Amesema Tsere.


 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad