SERIKALI KUTOA TUZO KWA WASANII INA MAANA GANI? - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 20, 2021

SERIKALI KUTOA TUZO KWA WASANII INA MAANA GANI?

 


ADELADIUS MAKWEGA–MBEYA.

Juzi serikali imetoa tuzo za filamu nchini Tanzania katika kilele cha tuzo kilichofanyika Mkoani Mbeya huku Waziri mwenye dhamana na Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akiwa mgeni rasmi na viongozi kadhaa wa kiserikali na Bunge wakishiriki. 

Tukio hilo liloshirikisha watazamaji zaidi ya 400 walioweza kuingia ukumbini huku Watanzania zaidi ya milioni 50 waliweza kulifuatilia kupitia Azam TV katika chaneli yake ya Sinema Zetu 103. Tukio hilo lilifanyika usiku wa Disemba 18, 2021 Mkoani Mbeya. Je linatoa taswira gani kwa maendeleo ya filamu nchini?

Ipo mitazamo mbalimbali lakini hii ni miongoni mwayo;

Kwanza, linatoa nafasi ya wasanii wa filamu nchini kutambuliwa na serikali na hiyo kutoa nafasi kwa anayeshinda kuweza kutambulika kitaifa na kimataifa kuwa yeye ni msanii bora katika tasnia hiyo. Ushindi huo unampa nafasi aliyeshinda kuwa bora zaidi na zaidi

Pili, yule anashinda anapata wasaa wa kuweza sasa kushindana kimataifa na hiyo inafanya yeye kujifua zaidi na kuweza kuona namna wasanii wa filamu wa kimataifa wanavyofanya kazi, tuzo ya serikali inamuongezea kujiamni zaidi. Kwa mfano ilitamkwa wakati wa ujio Dkt Fasi Khuramm kuwa inawezekana Tuzo za Oscar WWF kufanyika Tanzania mwaka 2023, hii ni nafasi kubwa na muhimu kwetu katika Sekta ya Sanaa.

Tatu, Tuzo hizo zinatoa nafasi ya kuongeza soko la filamu kitaifa na kimataifa na msanii na taifa kujipatia kipato kupitia kazi hizo. Hii inaweza kuwa kama ilivyo kwa mataifa makubwa kama Marekani.

Kwa mfano muigizaji wa filamu Mmarekani mwenye asili ya Canada ndiye aliyevunja na rekodi ya kuwa mwigizaji tajiri zaidi duniani kwa mwaka 2020 ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo, kulingana na orodha ya utajiri ya jarida la Forbes. Pia inasemekana kwamba mapato yake ni dola milioni 87.5 kwa mwaka, makubaliano yake ya hivi karibuni yakiwa ni dola milioni 23 ya kufanya filamu na mtandao wa Netflix. Dwayne Johnson alifuata nyayo za baba yake Rocky na kuwa bondia.

 

Alikuwa na mafanikio makubwa kwenye ubondia kabla ya kugeukia uigizaji, na kuwa nyota kwenye filamu ya Scorpion King, Fast & Furious 6 na kampuni ya Jumanji.

Baby Madaha ambaye ni miongoni mwa wasanii waliokuwepo katika kilele cha tuzo hizo Jijini Mbeya anasema kuwa mafanikio ya Wamarekani katika hilo ndiyo shabaha yao.

“Mimi nilipokuwa naingia katika tasnia hii nilikuwa na ndoto kubwa ambayo sasa naona inakaribia kutimia kwa serikali kuingia moja kwa moja kutoa tuzo hizi.”

Nne, kufanyika kwa tuzo hizo kuliambatana na watu zaidi 150 wakiwamo wasanii 90 kutembelea vyanzo mbalimbali vya utalii wa ndani viivyokuwamo katika mikoa ya Songwe na Mbeya mathalani Kimondo cha Mbozi. Kitendo hicho kimetoa fursa ya kuongeza kipato cha utalii wetu wa ndani, kwa hoteli mikahawa.

Isitoshe Watanzania wengine kupata nafasi ya kuvitambua vivutio hivyo vya utalii wa ndani ambayo vingi havifahamiki sana lakini kuwajengea Watanzania tabia ya kutembelea vivutio hivyo.

Tano, kutokana na kilele cha tuzo za filamu sasa kufanyika katika mikoa kinatoa nafasi ya kila mkoa kushiriki lakini kila mkoa kuwahamasisha wasanii wake kushiriki mashindano haya nadhani hata kwa mwakani matarajio ya idadi ya kazi zitakazoshiriki mashindano zitakuwa nyingi.

Sita, mashindano haya yanatoa nafasi ya wafanyabishara mbalimbali kuweza kutangaza kazi zao katika kilele hicho inatoa nafasi ya wafanyabiashara wa mikoani kuwafahamu wasanii wote kwa kina na hilo litasaidia mno hata wasanii kuweza kuwapata wafadhili wa ndani ambao wanaweza kufanya kazi nao.

Saba, mashindano hayo mara baada ya mzunguko utakapomalizika katika mikoa yote kama inavyotarajiwa na wengi panaweza pakawepo na picha halisi ya mikoa ipi ambao itakuwa imefanya vizuri zaidi na hilo linaleta ushindani mkubwa katika mizunguko yote ya mbele.

Nane, kilele cha tuzo za filamu kinajega mahusiano ya karibu baina ya wasanii na viongozi wa taifa letu katika ngazi za mikoa na kiwilaya ambapo mara nyingi ni wasanii wachache sana wanaweza kuzunguka katika maeneo yote ya taifa letu hilo linaleta umoja na udugu.

Tisa, katika tukio hili runinga ya Azam ilishiriki vizuri kuuhabarisha umma hiyo inatoa nafasi ya ushindani kwa vyombo vya habari zaidi katika mashindano yajayo ambapo nina hakika vyombo kadhaa vitaomba kurusha mubashara tukio hilo. Atakayeshinda anaweza kujipatia wadhamini ambapo chombo hicho kinaweza kujipatia fedha na kusaidia kukua kwa vyombo vyetu vya habari.

Kumi, kufanikiwa kwa mashindano ya tuzo za filamu kunatoa nafasi ya mashirikisho mengine ya sanaa, michezo na utamaduni kujifunza zaidi na yenyewe kuanza kujipanga na kuja na tuzo zao au kushawishi taasisi za umma na binafsi kutoa tuzo hizo pia. Hivyo tuzo za filamu nchini kuwa chachu ya maendeleo ya sekta zote tatu yaani Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Hayo ni baadhi tu mambo machache lakini vipi ushiriki wa makundi mengine mathalani uwepo wa viongozi wa kidini na kisiasa kutoka vyama vya upinzani kwani ndani ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ni jambo la jamii nzima ya Watazania. Nina hakika tamasha lijalo ushiriki wa makundi hayo utakuwepo. Kwani Watazamaji wa filamu wanashuhudia kila mara waigizaji hao wakiigiza nafasi za wanasiasa na viongozi wa dini sasa na wao waalikwe pia katika kilele cha tuzo hizo.

Naweka kalamu yangu chini kwa leo, tukutane tena katika tuzo za filamu zijazo panapo majaliwa ya Mungu.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad