HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 20, 2021

AHADI ZA UJENZI WA BARABARA MANYARA ZIMESHAWASILISHWA

 


Na Mwandishi wetu, Babati
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Manyara, RAS Caroline Mthapula, amesema wameshafikisha taarifa ya ahadi zote za ujenzi wa barabara zilizotolewa na wagombea urais kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Mthapula ameyasema hayo kwenye kikao cha bodi ya barabara cha mkoa huo (RCC) kilichofanyika mjini Babati.

Amesema ahadi zote za miradi yote ya ujenzi wa barabara za lami zilizoahidiwa na wagombea urais wameshawasilisha Serikalini kwa ajili ya utekelezaji wake.

"Niwatoe hofu viongozi na wananchi juu ya barabara zote zilizoahidiwa kujengwa wakati wa kampeni za uchaguzi kwani sisi kama mkoa tumeshawasilisha zote," amesema.

Meneja wa wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mkoani Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema ilani ya uchaguzi mkuu wa CCM 2020 inatambua miradi nane wanayoihudumia.

Mhandisi Rwesingisa amesema miradi hiyo imegawanyika kwenye makundi mawili ya ujenzi mpya wa kiwango cha lami na ukamilisha au kuanza upembuzi yakinifu.

Amesema miradi miwili ambayo usanifu wake umekamilika ni barabara ya Arusha - Kibaya - Kongwa ya urefu wa kilomita 430.

"Serikali imetenga sh300 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 kwa barabara ya Orkesumet - Mirerani kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina," amesema.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Hanang' Mhandisi Samweli Hhayuma amesema hayati John Magufuli na Rais Samia Suluhu walitoa ahadi ya ujenzi wa kilomita 10 za lami Katesh na barabara ya lami ya Mogitu - Haydom.

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Daniel Sillo amesema TANROADS na TARURA wanapaswa kuandaa bajeti zao mapema ili kuwasilishwa kwa wakati.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay amesema ahadi ya ujenzi wa barabara ya kilomita 190 Karatu - Mbulu - Haydom - Singida na kilomita 10 za lami Dongobesh na Haydom hazijatekelezwa zote.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, Paul Zacharia Isaay amesema  ujenzi wa barabara ya Karatu - Mbulu- Singida utarahisha usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad