WANAOAJIRIWA SERIKALINI NI LAZIMA KUPATA MAFUNZO CHUO CHA UTUMISHI KABLA YA KUANZA KAZI-Mchengerwa - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 19, 2021

WANAOAJIRIWA SERIKALINI NI LAZIMA KUPATA MAFUNZO CHUO CHA UTUMISHI KABLA YA KUANZA KAZI-Mchengerwa

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akionyesha baadhi ya nyenzo zitakazotumiwa na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania mara baada ya kuizindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Florens Turuka.Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma kabla ya kuzindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzindua Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) kwa kuzindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania mara baada ya kuzindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam. Waliokaa wa kwanza kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Florens Turuka.


Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
SERIKALI imewataka Waajiri wote katika taasisi za umma nchini kuhakikisha Watumishi wanaoajiriwa kwenye taasisi zao wanapata mafunzo elekezi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kabla ya kuanza kazi ili kufikia azma ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitaka Utumishi wa Umma kuwa uliotukuka.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.

Mhe. Mchengerwa amesema, mafunzo watakayoyapata watumishi hao yatasaidia kuwajenga kimaadili, kutambua na kuiishi miiko ya Utumishi wa Umma, kujua mwelekeo wa Serikali, kuwa na mienendo sahihi inayotakiwa katika Utumishi wa Umma na kuwajengea uzalendo kwa taifa.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa Watumishi wa Umma kuwajenga kiutendaji kwasababu leo hii ukipita kwenye taasisi za umma utabaini baadhi ya Watumishi hawako hai kiutendaji kwa sababu ya kukosa mafunzo elekezi ambayo yangewajengea nidhamu ya utendaji kazi,’’Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, ukosefu wa mafunzo kwa Watumishi wa Umma yanasababisha baadhi ya Watendaji na Watumishi kutoelewana kwasababu binafsi hali inayofanya baadhi ya Watendaji kutowapangia majukumu watumishi walio chini yao hivyo taifa linakosa mchango wao wakati Serikali inawalipa mshahara.

Katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa amewataka Waajiri kuzingatia taratibu za kushughulikia masuala ya nidhamu ili kulinda haki za Watumishi wa Umma.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza na Wajumbe wa Bodi, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Chuo cha Utumishi wa Umma kina jukumu kubwa la kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Umma na kuwaandaa wanaoingia kwenye Utumishi wa Umma ili wawe na mwenendo bora.

Ameongeza kuwa, Chuo hicho hakitakiwi kushindana na vyuo vingine kwasababu hata wahitimu wa vyuo vingine wanapaswa kujengewa uwezo kiutendaji na chuo hicho pindi wanapoingia kwenye Utumishi wa Umma.

Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Florens Turuka amesema Bodi yake inatambua dhamana kubwa waliyopewa na Serikali katika kuhakikisha Chuo kinatoa mafunzo yatakayojenga Utumishi wa Umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.

Dkt. Turuka amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo pamoja na Mhe. Waziri Mchengerwa kwa kuwateua Wajumbe wa Bodi yake ambapo ameahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii, juhudi na weledi ili chuo kitimize majukumu yake kikamilifu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad