HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 19, 2021

WANANCHI KUHAMA KIJIJI KUKOSA UMEME NA MAJI




NA YEREMIAS NGERANGERA ..NAMTUMBO
WANANCHI wa kijiji cha Mbimbi kitongoji cha Nambanje kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamedhamiria kuhama kijiji kutokana na sababu ya kukosa huduma ya maji na umeme katika mtaa wao kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mbimbi Yustus Nyoni aliwaambia waandishi wa habari akiwa ofisini kwake kuwa kitongoji chake kimoja kinachoitwa Nambanje katika kijiji hicho wananchi wake wamedhamiria kuhama kijiji hicho kutokana na kukosa umeme na maji katika kitongoji chao kwa muda mrefu huku vitongoji vingine vikiwa na huduma hizo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Nambanje Batlazali Ngonyani alidai wananchi wa kitongoji chake walikubaliana katika kikao cha kitongoji hicho kuwa wahame kijiji hicho na kwenda kijiji cha Namabengo ili waweze kupata huduma muhimu za maji na umeme kama wananchi wengine .

Ngonyani alisema malalamiko yao ya kudai umeme na maji ni ya muda mrefu lakini hakuna kinachoendelea kwa sasa na ndipo wananchi wa mtaa huo kwa pamoja na katika kikao chao cha kitongoji walikubaliana kuhama kijiji cha mbimbi na kwenda kijiji cha Nambabengo.

Salum Nachundu kaimu meneja Ruwasa pamoja na kukiri kuwa kitongoji hicho kukosa maji alidai miundombinu ya maji iliharibiwa na mkandarasi aliyekuwa anatengeneza barabara ya Namabengo –Mbimbi na kilichotakiwa kijiji kufuatilia fidia kwa mkandarasi aliyeharibu miundombinu hiyo na kuirudisha kama mwanzo ili wananchi wa kitongoji hicho kiweze kuendelea kupata maji.

Nachundu ambaye pia ni mlezi wa kata ya Litola na fundi mfuatiliaji wa kata hiyo alidai kitongoji hicho kinakosa maji kutokana na bomba linalopeleka maji katika kitongoji hicho kukatwa na mkandarasi aliyekuwa anatengeneza barabara ya Namabengo mpaka mbimbi .

Mtendaji wa kijiji cha Mbimbi Bernadeta Luambano pamoja na mambo mengine alithibitisha kuwa wananchi wa kitongoji cha Nambanje wanahitaji kuhamia kijiji cha Namabengo kutokana na kukosa maji na umeme katika kitongoji chao

Kwa mujibu wa meneja wa Tanesco wilaya ya Namtumbo Philipo Joseph Komu alidai kitongoji hicho hakijafanyiwa upembuzi yakinifu na akakiri kupokea malalamiko ya wananchi wa kitongoji cha Nambanje yaliyowasilishwa kwake na mtendaji wa kijiji cha Mbimbi.

Kitongoji cha Nambanje kimepitiwa na nguzo za umeme kutoka kijiji cha Namabengo lakini kitongoji hicho hakijapata umeme huku vitongoji vingine vya kijiji cha mbimbi vimepatiwa umeme na kuibua hasira baada ya kuona umeme umepita katika maeneo ya kitongoji chao lakini wakiishia kuutazama ukipita na kutumiwa na vitongoji vingine vya kijiji chao.

Kijiji cha Mbimbi kipo katika kata ya Litola kikiwa na vitongoji sita na kati ya vitongoji hivyo vitongoji vitano vimepatiwa huduma ya umeme na maji lakini kitongoji cha Nambanje pekee katika kijiji hicho kimekosa huduma ya maji na umeme na kufikiria kuhama kijiji hicho ili kwenda Namabengo kufuata huduma za maji na umeme.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad